Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, Azindua Boti ya Uokozi na Uzamiaji ya KMKM Bandari ya Mkoani Kisiwani Pemba.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, akikata Utepe kuashiria Uzinduzi wa Boti ya Uokoaji na Uzamiaji wa KMKM,kushoto Mkuu wa KMKM Zanzibar Hassam Mussa Mzee, kulia Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ. Mhe. Haji Omar Kheri.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi DK. Ali Mohamed Shein, amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejidhatiti kuwaokoa wananchi wake kutokana na ajali zinazotokea baharini kwa kununua vifaa vya kisasa vinavyokwenda na wakati uliopo.
Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kukuimarisha kwa kukipa vifaa vya kisasa vya uzamiaji na uokozi kikosi cha KMKM, ili kukabiliana na ajali zinazotokea baharini sambamba na kuimarisha usalama katika miji ya Unguja na Pemba.
Dk Shein aliyasema hayo, katika uzinduzi wa Vituo vya Uokozi vya KMKM kwa niaba ya Vituo vya Uokozi KMKM Kibweni na Nungwi ambapo hafla hiyo ilifanyika huko katika Bandari ya Mkoani kisiwani Pemba.
Maelezo hayo aliyatoa mara baada ya kuzindua boti ya uokozi sambamba na kituo cha uzamiaji na uokozi kilicho chini ya kikosi cha KMKM huko katika Bandari ya Mkoani Pemba, ikiwa ni sehemu ya shamra shamra za miaka 55 ya Mapinduzi Zanzibar, yalioasisiwa mwaka 1964.
Rais Dk. Shein alisema kuwa baada ya Zanzibar kukumbwa na majanga kadhaa yanayotokea baharini, mnamo miaka ya 2011 na 2012 Serikali ilidhamiria kutafuta mradi mkubwa kwa lengo la kununua vifaa vya kisasa vya uokozi, ili kukabiliana na ajali za majini.
Alieleza kuwa, ununuzi wa vifaa hivyo, ikiwemo boti zenye vifaa vya kisasa ni utekeleza wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 hadi 2020, sambamba na utekelezaji kwa vitendo wa azma ya Mapinduzi ya matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inataka kuona kila mwananchi anaeishi kwenye mitaa, anaishi kwa usalama na amani hata akiamua kusafiri iwe nchi kavu, bahari au angani awe na utulivu na uhakika wa safari yake anayokwenda.
Alisiositiza kuwa Serikali, inataka kuona kuwa usafiri wa aina zote unaimarika, ndio maana imekuwa ikitumia fedha nyingi ili kuhakikisha kuna kuwa na usafiri wa uhakika wakati wote.
“Ndio maana tumeamua kuwa na mradi huu wa Zanzibar salama, ambao unahusisha ujenzi wa vituo sita vya uokozi, ununuzi wa boti za uokozi, mafunzo kwa wapiganaji, wananchi na vifaa vya kisasa ili usalama upatikane,”alieleza.
Katika hatua nyengine, Rais Dk. Shein alisema kuwa Serikali ililamizika mnamo mwaka 2013/14 kubuni mradi huo wa Zanzibar salama, na utekelezaji wake ukaanza mwaka 2015 kwa lengo la kuhakikisha uwepo wa uokozi wa uhakika na wa kisasa.
“Kila mmoja ni shahidi kuwa, tulipata msiba mzito mwaka 2011 wa Mv. Spice Islander sasa kwa tukio hilo, tulipata funzo pale tulipokosa namna ya kuwaokoa wenzetu waliozama, lakini sasa tumeshapata vifaa vya kisasa,”alieleza Dk. Shein.
Alieleza kuwa pamoja na kuwepo kwa boti na vifaa vya kisasa vya uokozi, Serikali pia, inayo meli maalum ya kuzimia moto baharini, ambapo yote hayo ni kuhakikisha wananchi wanaotumia usafiri wa bahari, wanakuwa salama.
Rais Dk. Shein alisema kuwa zipo boti nyengine ndogo ndogo zenye mwendo wa kasi, ambazo zote hizo ni sehemu ya mradi huo ambao ulianza utekelezaji wake mnamo mwaka 2015.
“Naomba wananchi niwambie kuwa, serikali yetu imeshajipanga vya kutosha tena kwa kuwa na vifaa vya kisasa, na wazamiaji watakuwa na boti yao maalum, ambayo inatarajiwa kuwasili mwezi huu, ambayo inawezo wa kwenda mwendo kwa kasi,”alisisitiza.
Aliongeza kuwa, sehemu ya pili ya mradi huo mkubwa ni uwekaji wa kamera maalum za kutunza usalama CC-TV ambapo kwa sasa katika eneo la Mji mkongwe pekee, zimeshafungwa 687 mbali na maeneo mengine ya mji wa Zanzibar.
“Kwanza tumeshaanza kwa Mji Mkongwe na miji mengine ikiwemo ya Pemba, itawekewa kamera hizo endapo uchumi utaruhusu kwa hapo baadae,”alieleza Dk. Shein.
Kuhusu uwepo wa vikosi vya JKU, KMKM, KZU, KVZ, na Chuo cha Mafunzo Zanzibar, alisema vikosi vipo kwa mujibu wa katiba na sheria za Zanzibar na wala haviendeshwi kwa matakwa ya mtu.
Alisema kuwa kikosi cha mwanzo kilichoanzishwa kilikuwa ni KMKM wakati huo wakiitwa wanamaji, na vinaendeshwa kwa mujibu wa sheria za kuanzishwa kwa vikosi hivyo.
“Wale wanaodhani kuwa vikosi hivyo vipo kwa bahati mbaya na vinajiendesha wapendavyo wao, sio sahihi bali wanakwenda kwa mujibu wa sheria wala havishirikiani na wanaoharibu amani na utulivu,”alisisitiza Dk. Shein.
Awali akisoma taarifa ya kiufundi Mkuu wa KMKM Zanzibar Komodoo Hassan Mussa Mzee, alisema ujenzi wa vituo vya uzamiaji wa uokozi Zanzibar, unagusa moja kwa moja maisha ya wananchi wote wa Zanzibar.
Alisema mradi huo, umejumuisha majengo, ununuzi wa boti za uokozi na vifaa mbali mbali vya kisasa vya uokozi na vya mawasiliano, ambapo ni jambo muhimu katika harakati za uokozi.
“Unakusudia kuwa vituo sita vya uokozi ambapo ni pamoja na Mkoani, Wete na Msuka kwa Pemba ambapo vyengine ni Kibweni, Nungwi na Kizimkazi kwa Unguja,”alieleza.
Komodoo Hassan alisema kuwa kati ya vituo hivyo sita ambavyo tayari vishakamilika hadi hivi sasa ni vituo vitatu ambavyo ni Kibweni, Nungwi na Mkoani Pemba, ambapo kila kituo kinatarajiwa kuwa na boti za wazamiaji, vifaa kamili na mitambo kwa ajili ya kazi ya uokozi.
Katika hatua nyengine Komodoo huyo alisema, mradi huo wanauona kama ni utekelezaji kwa vitendo wa malengo ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, ambapo kwa mwaka huu yanatimiza miaka 55.
“Tunaahidi kuwa majengo, vifaa na boti tutavitunza na kuvilinda kwa nguvu zetu zote, ili kuhakikisha mradi huo mkubwa unafikia malengo yaliokusudiwa ambayo ni kuwaokoa wananchi wetu,”alifafanua.
Mapema Katibu Mkuu wa Wizara ya Nchi afisi ya Rais, Tawala za Mikoa, serikali za mitaa, Idara Maalum za SMZ Zanzibar,  Radhia Rashid Haroub, alisema mradi huo ulitengewa Shilingi za Kitanzania bilioni 5.9 hadi kumalizika kwake, ingawa gharama ziliongezeka kutokana na mahitaji na ongezeko la thamani vya vifaa.
Katibu Mkuu huyo alieleza kuwa, mradi huo una maeneo makuu manne, ikiwa ni pamoja na kujenga vituo sita vya uokozi Unguja na Pemba, kununua boti na vifaa vyake, kununua vifaa vya mawasiliano na mafunzo kwa askari na wananchi.
Aidha, alieleza kuwa, vituo viwili vilivyokamilika vya Kibweni na Mkoani Pemba, vimegharimu shilingi milioni 966.8, ambapo ujenzi wa vituo hivyo, ni sehemu ya utekelezaji wa malengo la Mapinduzi ya Zanzibar.
“Katika ununuzi wa boti mbili za uokozi, serikali imegharimu TZ Shilingi bilioni 12.5, ambapo pia, kuna ununuzi wa nguo maalum za uokozi, mitungi ya gesi, mashine ya kutengenezea gesi na vifaa vya kutumia, wakati wa uokozi chini ya bahari ambapo vimegharimu shilingi milioni 500,”alifafanua.
Mapema Rais Dk. Shein alizindua boti maalum ya uokozi kwa kituo cha KMKM Mkoani na kisha kukifungua kituo kipya cha uokozi bandarini hapo ambapo katika uzinduzi wote huo alipata maelezo kutoka kwa viongozi wa kikosi cha KMKM pamoja na uongozi wa Mamlaka ya Bahari Kuu.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa na Serikali pamoja na wananachi ambapo pia, Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd nae alihudhuria.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.