Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, akiitikia dua wakati wa kumaliza hafla ya futari iliofanyika nyumbani kwake Kibele Wilaya ya Kati Unguja ikisomwa Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh.Omar Saleh Kabi.baada ya kumaliza hafla hiyo.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed
Shein ameungana pamoja katika futari maalum aliyoiandaa yeye na familia yake
kwa ajili ya wananchi mbali mbali wakiwemo majirani zao huko katika makaazi
yake Kibele, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.
Hafla hiyo ya futari
ilifanyika katika viwanja vya nyumbani kwake Kibele na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Makamo wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, viongozi wa dini, Serikali, vyama vya
siasa, wananchi wa kijiji hicho pamoja na vijiji vya jirani.
Mke wa Rais wa
Zanzibar Mama Mwanamwema Shein nae aliungana na viongozi wa kike wa Kitaifa, wanafamilia
pamoja na wananchi mbali mbali wakiwemo majirani zake katika hafla hiyo ya
futari maalum waliyoiandaa.
Akitoa neno la
shukurani kwa niaba ya Alhaj Dk. Shein pamoja na familia yake, mwanafamilia Mohamed
Ali Shein aliwashukuru waalikwa wote waliofika katika hafla hiyo na kufutari.
Katika maelezo yake, Mohamed
Shein alieleza kuwa familia hiyo imefarajika sana kwa waalikwa hao kukubali
mwaliko huo na kufika kwa wingi katika futari hiyo maalum waliyoiandaa.
Aidha, Alhaj Dk. Shein
aliwaombea dua kwa Mwenyezi Mungu wananchi wote na viongozi waliohudhuria
katika futari hiyo kuendelea kupata neema na baraka za Allah hasa katika
kipindi hichi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Alhaj Dk. Shein na
familia yake wamekuwa na utamaduni wa kila mwaka katika mwezi Mtukufu wa
Ramadhani kuandaa futari maalum na kuwaalika wanakijiji, majirani pamoja na
waalikwa wengine wakiwemo viongozi wa Serikali, dini na vyama vya siasa, futari
ambayo hufanyika huko katika makaazi yake Kibele, Mkoa wa Kusini Unguja.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment