Habari za Punde

RC kuwashughulikia wazee watakaozembea malezi ya watoto

Na.Haji Nassor -Pemba.
SERIKALI ya Mkoa wa Kusini Pemba, imesema kuanzia sasa, baada ya mtoto kudhalilishwa yataangaliwa mazingira na kama yataonyesha mzazi amezembea kwenye malezi ataanzwa yeye kuchukuliwa hatua za kisheria kabla ya kutafutwa mtuhumiwa.
Alisema wapo baadhi ya watoto hubakwa au kulawitiwa kwa sababu tu ya uzembe wa wazazi, ikiwemo kuwaachilia muda mkubwa nje hasa nyakati za usiku.
Mkuu wa Mkoa huo, Hemed Suleiman Abdalla alisema wapo watoto wamekuwa wakiranda randa ovyo nje ya nyumba zao, kwa kwenda kwenye masomo ya ziada, huku wazazi wakiwa hawana ushughulikiaji na kisha hapo hujitokeza wahalifu kuwadhalilishaji.
Hemed alitoa karipio hilo hivi karibuni mjini Chakechake, alipokuwa akizungumza na masheha, wanaharakati wa kupamba na udhalilishaji kwenye uzinduzi wa mradi wa kupinga udhalilishaji na ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto, unaoendeshwa na Jumuiya ya Tumaini Jipya ‘TUJIPE’ Pemba.
Alisema wapo baadhi ya wazazi wakati mwengine, hutumia muda mwingi kukesha hasa nyakati za usiku kusherehekea harusi na kuwafungia ndani watoto, jambo ambalo humpa mwanya mdhalilishaji kufanya apendavyo.
Alieleza kuwa, baada ya kutokezea hilo, familia huhamia vituo vya Polisi kulalamikia jambo hilo ambalo ni jambo jema, ingawa mazingira kama yakibainika kwamba kuna na uzembe wa wazazi, nao watafikishwa mbele ya vyombo husika.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa wa kusini Pemba, katika kudhibiti vitendo hivyo vya udhalilishaji, alisema mwananchi atakayeonyesha televisheni  nje, Sheha wa shehia husika ajiondowe mwenyewe kwenye nafasi hiyo, kabla hajakutana nae uso kwa uso.
Alisema tayari alishawataka masheha kulisimamia hilo tokea zamani, hivyo kwa sasa hana tena nasaha na Sheha ambaye eneo lake atakamatwa mwananchi akionyesha tv nje, sheha huyo ajiondowe mwenyewe.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa wa kusini Pemba Hemed Suleiman Abdalla, alikumbusha marufuku nyingine ndani ya mkoa huo ya kuwakataza wanaume makaka poa kuwapamba maharusi wa kike, ni ya kudumu, hivyo familia yoyote itakayobeza hilo, atakwenda naye sambamba.
Alifafanua kuwa, kama hiyo kwao ni sehemu ya ajira, basi wajipange kutafuta ajira nyingine, lakini sio kwa wanaume, kuwapamba maharusi wa kike, kwani ni kinyume na maadili.
Aliongeza kuwa, anaelewa kuwa baadhi ya viongozi wanahusika na hilo, ndio maana anapotoa matamko ya kulaani, hupokea ujumbe na taarifa nyingine, ingawa alisema hilo halimkwazi.
Mratibu wa Mradi wa kupinga udhalilishaji kwa wanawake na watoto kutoka Jumuiya ya Tumaini Jipya Pemba, ‘TUJIPE’, Tatu Abdalla Msellem, alisema lengo ni kujua sababu ya kuendelea kwa matendo hayo ndani ya jamii.
Alisema TUJIPE baada ya kupewa mradi na the foundation for civil society wenye thamani ya shilingi milioni 40, sasa wanachohitaji ni ushirikiano kuanzia wananchi wa shehia tano hadi ngazi ya taifa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.