Habari za Punde

UNFPA Yatowa Pongezi Kwa Juhudi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akimsikiliza mgeni wake Mwakilishi wa UNFPA  Nchini Tanzania Ms.Jacqueline  Mahon wakati wa mazungumzo alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo kwa ajili ya kumsalimia Rais

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe Dk. Ali Mohamed Shein, alifanya mazungumzo na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) Bibi Jacqueline Mahol aliyefika Ikulu Mjini Zanzibar kwa ajili ya kuzungumza na Rais.

Katika maelezo yake Rais Dk. Shein alilipongeza Shirika hilo la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA), kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuhakikisha huduma za jamii zinaimarika zikiwemo huduma za afya.

Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa Shirika la UNFPA limekuwa na uhusiano na ushirikiano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa muda mrefu na tokea wakati huo limekuwa likifanya juhudi katika kusaidia miradi mbali mbali ya maendeleo.

Alieleza kuwa juhudi kubwa zimechukuliwa na mafanikio yanaonekana katika kupunguza vifo vya akina mama na watoto kwa mashirikiano ya pamoja kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Washirika wa maendeleo likiwemo Shirika hilo la UNFPA.

Nae Mwakilishi huyo wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA), Bibi Jacqueline Mohan alitoa pongezi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Shein katika kuimarisha miradi ya maendeleo pamoja na kuwapatia huduma wanawake na watoto.

Mwakilishi huyo aliahidi kuwa Shirika lake litaendelea kuziunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kupambana na umasikini, kuwaletea maendeleo wananchi wake sambamba na kutekeleza Malengo na Mikakati yake iliyoiweka kwenye MKUZA III.

Katika maelezo yake, Mwakilishi huyo alitumia fursa hiyo kuipongeza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanikisha vyema Mkutano wa 39 wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) pamoja na kupelekea lugha ya Kiswahili kupitishwa kwua lugha rasmi ya nne itakayotumika katika Jumuiya hiyo.

Aidha, Mwakilishi huyo alitumia fursa hiyo kutoka pole kwa ajali ya gari la mafuta iliyotokea hivi karibuni huko Morogoro na kusabisha vifo pamoja na majeruhi kadhaa.

Pia, kiongozi huyo alipongeza juhudi za Zanzibar katika kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2020 sambamba na mafanikio makubwa yaliopatikana katika usajili wa vizazi kwa asilimi 71 na kueleza kwua (UNFPA), inajivunia mafanikio hayo yaliopatikana hapa Zanzibar.

Hivyo, Shirika hilo limmeahidi kuendelea kuiunga mkono Zanzibar na kutoa misaada yake zaidi kwa kuendeleza miradi mbali mbali ambapo pia, Shirika hilo limeahidi kutoa msaada wa gari za mbili za kubebea wagonjwa (ambulances).

Pia, Shirika hilo limeeleza azma yake ya kuanzisha kampeni juu ya kukinga vifo vya watoto wachanga na wazazi na kuahidi kuzidisha mashirikiano katika sekta mbali mbali za maendeleo na huduma za kijamii ikiwemo sekta ya afya, elimu na nyenginezo.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.