Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Raius wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi Atembelea Miradi ya TASAF Zanzibar.


Balozi Seif  kati kati akiwa pamoja na Naibu Waziri Ofisi yake Mh. Mihayo Juma N’hunga kushoto yake na Mkurugenzi Uratibu Nd. Khalid Bakar Kulia yake wakikagua maeneo mbali mbali ya Kituo cha Afya cha Kiyanga kinachotarajiwa kuanza kutoa huduma muda wowote kuanzia sasa.
Na.Othman Khamis.,OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema uamuzi wa Wananchi wa Kiyanga wa kuchaguwa ujenzi wa Kituo cha Afya kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {TASAF} ni wabusara katika kujisogezea huduma za Msingi za Jamii katika eneo lao.
Alisema Ujenzi wa Kituo hicho unakwenda sambamba Sera ya Serikali kupitia Wizara ya Afya ya kuwasogezea Wananchi huduma za Afya katika masafa yasioyozidi Kilomita Tano.
Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati akizungumza na Wananchi wa Shehia ya Kiyanga baada ya kukikagua Kituo cha Afya kilichojengwa kupitia Miradi ya Tasaf ambacho tayari kimeshamaliza ujenzi wake kikisubiri kutoa huduma za Afya kwa Wananchi mbali mbali wa eneo hilo pamoja na yale ya jirani.
Alisema Serikali Kuu haina pingamizi ya maamuzi yanayotolewa na Weananchi wake katika kujichagulia Mradi unaofaa kwa maendeleo na Ustawi wao kupitia mfumo wa kujungwa mkono kupitia Miradi ya Tasaf hapa Nchini.
Balozi Seif  akiwa Kiongozi Mkuu anayesimamia uratibu wa shughuli za Maendeleo ya Jamii zinazotekelezwa kupitia Mfuko wa Tasaf  Visiwani Zanzibar  aliwashauri Wananchi wa maeneo hayo ya Kianga kukitumia Kituo hicho kwa kupima Afya zao.
Alisema yapo maradhi mengi yanayowakumba Wananchi na hatimae kusababisha upotevu wa Maisha ambayo yanaweza kudhibitiwa  iwapo Wananchi watajenga Utamaduni huo wa kupima afya zao.
“ Mwananchi anapojua mapema matatizo ya afya yake inakuwa rahisi kujikinga kwa kutumia ushauri anaopewa na mhudumu wa Afya”. Alisisitiza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Balozi Seif  alikubaliana na wazo la Mwakilishi wa Jimbo la Mwera ambae pia ni msaidizi wake katika masuala ya Serikali Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mh. Mihayo Juma N’hunga la kuutaka Uongozi wa Uratibu wa Ofisi yake na Halmashauri ya Wilaya ya Magharibi “A”  kuhakikisha kwamba Kituo hicho kinaanza kutoa huduma za afya  ndani ya Wiki Mbili kuanzia sasa.
Aliwapongeza wasimamizi wote waliojitolewa kutenga muda wao kwa ajili ya kujitolewa kwenye Ujenzi wa Kituo hicho cha Kisasa kitakachosaidia Huduma za Afya kwa Wakaazi wengi wa Wilaya ya Magharibi “A”.
Alisema itapendeleza kuona Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo inawapa nafasi ya mwanzo Wasimamizi hao kufanya kazi kwenye Kituo hicho jambo ambalo litawapa uchungu wa Uzalendo wa kuendelea kukitunza ili kidumu kwa muda mrefu.
Akitoa Taarifa ya Ujenzi wa Kituo hicho cha Afya cha Kiyanga, Mkurugenzi wa Uratibu wa SMT na SMZ  kutoka Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Khalid Bakar Amran  alisema Kiyanga ni miongoni mwa Shehia 126 za Unguja zinazotekeleza Miradi ya Kaya Maskini.
Nd. Khalid alisema Mradi wa Ujenzi wa Kituo hicho ulioibuliwa na Wananchi wenyewe wa Kiyanga Mnamo Mwezi Mei Mwaka 2018 umekuja kufuatia  changamoto zilizokuwa zikiwasumbua za upatikanaji wa huduma za Afya.
Alisema Uongozi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania Tasaf  umeridhia maamuzi hayo ya Wananchi wa Kiyanga na kuchukuwa hatua zinazostahiki za kusimamia Mradi walioridhika nao wa huduma za Afya.
Mkurugenzi Khalid alifafanua kwamba licha ya ujenzi huo kukumbwa na changamoto za upatikanaji wa Mchanga na kupanda kwa bei ya Saruji lakini bado Ujenzi wake ulipungua gharama baada ya Wananchi wenyewe kuamua kujitolea na hatimae Ujenzi wake kugharimu jumla ya shilingi Milioni 174,150,284/- hadi kukamilika kwake.
Akitoa shukrani zake mwakilishi wa Jimbo la Mwera ambae pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa ZanzibarMh. Mihayo Juma N’hunga alisema Jimbo hilo halikuwa na Kituo cha Afya cha Serikali kwa kipindi kirefu.
Mheshimiwa Mihayo alisema tatizo hilo lilipelekea Wananchi wa maeneo hayo kufuata huduma za Afya  masafa ya mbali ya Mwera, Kizimbani au kupelekwa Mjini Moja kwa moja jambo ambalo lilileta hatari hasa kwa akina mama wajawazito.
Alisema wakati inapotokea Kampeni za Chanjo kwa Watoto watendaji wa zoezi hilo hulazimika kutoa huduma hiyo katika Nyumba za Watu Binafsi au Magofu ya Nyumba jambo ambalo lililoleta masikitiko makubwa kwa Wananchi hao.
Mwakilishi huyo Jimbo la Mwera aliwahakikishia Wananchi wake kwamba Uongozi wa Jimbo hilo uko katika Mkakati wa kutaka Kujenga Skuli ya Ghorofa kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo kwa lengo la kuwaondoshea usumbufu Wanafunzi wa Jimbo hilo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.