Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Wazee wa CCM Wilaya ya Kati Unguja katika ziara yake, mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Kituo cha Walimu Dunga Mkoa wa Kusini Unguja.
MAKAMO
Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema kuwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (
CCM) Wazee bado hawajapitwa na wakati.
Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati alipofanya mazungumzo
na Wazee wa CCM wa Wilaya ya Kati Unguja huko katika Ukumbi wa Kituo cha Walimu
Dunga, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja akiwa anahitimisha ziara zake za
kukutana na Wazee wa Unguja na Pemba.
Makamo huyo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar alisema kuwa CCM
inaendelea kuwajali, na kuwathamini Wazee kwani wazee walitambuliwa tokea
wakati wa kudai uhuru chini ya chama cha ASP na waliweza kushirikia bega kwa
bega hadi kupatikana uhuru huo.
Alieleza kuwa kwa kawaida ndani ya chama hicho wanaowaandaa
vijana na viongozi ni Wazee hivyo kuna kila sababu ya kuwaenzi kuwatunza na
kuwathamini wazee kutokana na umuhimu wao mkubwa walionao katika jamii.
Rais Dk. Shein aliahidi kuendelea kufanya kazi na wazee
sambamba na kushirikiana na viongozi wote wa chama hicho wakiwemo wa Jumuiya zote
za chama hicho, Wawakilishi na Wabunge ambao wananguvu kubwa katika jamii.
Alisema kuwa kila Wilaya katika Wilaya za Zanzibar zina
historia yake lakini Wilaya ya Kati ina historia kubwa tokea ASP kwani ilikuwa
ndio ngome ya chama hicho na hivi sasa CCM.
Rais Dk. Shein alieleza historia ya akina mama jinsi
walivyopambana katika kudai uhuru wa Zanzibar na hatimae kuruhusiwa kupiga kura
kwani walikuwa hawakupata fursa hiyo.
Rais Dk. Shein pia, alitumia fursa hiyo kuahidi kukutana na
Jumuiya zote za CCM za Wilaya zote za Unguja na Pemba kama alivyofanya kwa
Wazee.
Aliwapongeza wazee kwa kushirikiana na Serikali yao
sambamba na kusimamia amani, utulivu, mshikamano na mapenzi kwa wananchi na
wanaCCM wengine jambo ambalo limepelekea Zanzibar kuwa salama.
Makamo mwenyekiti huyo wa CCM alisisitiza haja ya kuyaenzi,
kuyalinda na kuyaheshimu Mapinduzi ya Januari 12, 1964 kwani ndio yaliyoikomboa
Zanzibar pamoja na kuulinda na kuudumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Nae Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Abdalla Juma Mabodi
alisema kuwa alama anayowaachia Chama ni kuwepo kwa Baraza la Wazee la Makao
Makuu ya CCM Kisiwandui.
Alitoa pongezi kwa wazee wa Wilaya ya Kati kwa mashirikiano
makubwa wanayoyatoa huku akitoa pongezi kwa ushirikiano wa viongozi wa chama
uliopo katika Wilaya ya Kati.
Rais Dk. Shein aliahidi kwamba kwa muda mfupi ujao
changamoto ya ukosefu wa walimu wa Sayansi hapa nchini itaondoka kutokana na mikakati
maalum iliyowekwa na Serikali ya kuwasomesha walimu ndani na nje ya nchi.
Nao Wazee wa Wilaya ya Kati Unguja kupitia Baraza lao la
Wilaya ya Kati kwa namna ya kipekee waliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar ya Awamu ya Saba anayoiongoza
Rais Dk. Shein kwa uwamuzi wake wa kizalendo wa kuwapelekea huduma mbali mbali
za kijamii.
Wazee hao wa Wilaya ya Kati walieleza kuwa suala zima la
Pencheni Jamii ya kila mwezi wanayoipata wazee wapatao 1977 wa Wilaya ya Kati
jambo ambalo kwao ni faraja ambayo
hawakuitegemea.
Walieleza kwamba fedha hizo zinawasaidia kufanya shughuli
ambazo zinawainua kiuchumi na kuachana na utegemezi kwani hayo ndio madhumuni ya
ASP chini ya uongozi wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar Hayati Mzee Abeid Amani
Karume.
Kwa upande wa sekta ya afya, wazee hao walieleza kuwa
wanafaidika na ujenzi wa vituo vipya vya mama na mtoto katika Shehia ya Umbuji,
Mwera, Kiboje Mkwajuni, Bambi na Tunguu.
Aidha, kwa upande wa sekta ya elimu wazee hao walieleza
kuwa wamefaidika kwa kiasi kikubwa kupitia sekta hiyo kutokana na kujengewa
skuli za Sekondari za kisasa katika
Shehia ya Uroa skuli ya ghorofa, skuli ya Uzini, Tunguu pamoja na maabara kubwa
katika skuli ya Unguja Ukuu kaepwani.
Wazee hao wa Wilaya ya Kati walitoa shukurani zao kwa
wakulima kuendelea kusaidiwa ambapo Serikali imebeba asilimia 70 ya gharama za
pembejeo na wakulima kulipia asilimia 30 tu.
Pamoja na hayo, wazee hao walitumia fursa hiyo kumpongeza
Rais Dk. Shein kwa kuitekeleza kwa vitendo Ilani ya Uchaguzii ya CCM kwa
kuyabadilisha Mabonde yao ya mpunga kwenda na teknolojia ya Kisasa kwa kuyafanya
ya umwagiliaji maji na kupata eka 2095 katika mabonde ya Wilaya hiyo.
Kwa upande wa mifugo wazee hao walieleza jinsi
walivyofaidika na mradi wa “Kopa ngombe lipa ngombe” kwa kuwaongezea kipato
wafugaji na kuifanya Wilaya hiyo kuwa ni moja ya watoaji wa maziwa kwa wingi
ambapo kwa mwezi wanakusanya lita 31068.
Wazee hao walitoa pongeza kwa Rais Dk.Shein kwa
kuwarahisishia harakati zao za maisha kuwa nyepesi kutokana na kuwajengea
barabara kila upande katika Wilaya yao ikiwemo barabara ya Jendele hadi Unguja
Ukuu, Koani hadi Jumbi inaendelea kujengwa, Umbuji hadi Uroa, Ukongoroni,
Charawe hadi Bwejuu inaendelea kujengwa.
Kwa upande wa huduma ya maji, wazee hao walieleza
kufurahishwa na ukarabati wa Matangi ya maji Unguja Ukuu kwani hatua hiyo
itawafanya watu wa kisiwa cha Uzi na Ng’ambwa kuwa na matumaini ya kupata maji
safi na salama.
Nae Mwenyekiti wa
CCM Wilaya ya Kati Aboud Said Mpate alieleza kuwa Wazee wa Wilaya ya Kati wamekuwa
na mchango mkubwa kwa viongozi wa Serikali na Chama kutokana na ushauri,
maelekezo na mashirikiano makubwa wanayotoa.
Wanampongeza sana katika kazi nzuri anayoifanya katika
kuioingoza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na watu wake na kueleza
kwua wamekuwa na mashrikiano mazuri.
Wanampongeza jinsi anavyotoa elimu na maelekezo kwa
viongozi anapokutana nao na jinsi ya kazi nzuri ya kusimamia Ilani ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) hatua ambayo impelekea kupatikana kwa maendeleo na mafaniko
makunbwa chini na uongozi wake.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment