Habari za Punde

Makamu wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi Apokea Taarifa ya Kamati.

Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya kusimamiaji Utafutwaji wa Mashamba ya Serikali ambae pia ni Makamu wa Pili wa Raia wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza katika kikao cha kupokea Ripoti ya awali ya uhakiki wa Mashamba hayo kutoka kwa Wakuu wa Wilaya Nne za Pemba.


Na.Othman Khamis.OMPR. 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kazi kubwa iliyofanywa na Viongozi, Watendaji wa Taasisi za Umma, Masheha, Wananchi kwa kushirikiana na Kamati za Ulinzi na usalama za Wilaya Nne za Pemba ndio iliyopelekea kuibuliwa kwa Mashamba mengi ya Serikali yasiyotambulika Kisiwani Pemba.
Alisema azma ya Serikali Kuu kufanya zoezi hilo lililopelekea kuundwa kwa Kamati ndogo  ndogo zilizoongozwa na Wakuu wa Wilaya Miezi Mitatu iliyopita imelenga kuimarisha Uchumi wake kupitia Rasilmali inazomiliki kwa mujibu wa Sheria.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati wa Kikao cha Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya Nne na Mikoa Miwili za Kisiwani Pemba katika Kikao cha kupokea Taarifa ya utambuzi wa Mashamba ya Serikali kilichofanyika katika Ukumbi wa Kiwanda cha Makonyo Wawi Chake Chake Pemba.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  haitegemei Wajomba kutoka Nje ya Nchi katika kusaidia Uchumi wake badi inachofanya ni kujitahidi kufanya juhudi za kuimarisha  vianzio vyake vya mapato kutegemea huduma zinazotolewa na Taasisi pamoja na Mashirika ya Umma.
Balozi Seif alionya kwamba wakati Kamati zilizoundwa kuendelea na kazi ya kutafuta Mashamba yaliyobaki ya Serikali kupitia Vyombo vyake vya Dola haitasita kumuwajibisha Mtu ye yote atakayebainika kuendelea kuyaficha Mashamba ya Serikali.
Alikemea baadhi ya Masheha wanaoendelea kuficha Taarifa za uwepo wa Mashamba ya Serikali katika Shehia zao watambue kwamba iko siku itawagharimu kwa kuwajibishwa katika misingi ya uhujumu Uchumi wa Taifa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uzalendo mkubwa uliotumika katika kuyatafuta Mashamba ya Serikali na akaendelea kuwakumbusha Wakuu wa Wilaya kuongeza jitihada za kuyatafuta na hatimae kuyahakiki Mashamba yaliyobakia ya Serikali yaliyomo ndani ya Wilaya zao.
Balozi Seif akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa iliyopewa jukumu la  kuyatafuta na kuyahakiki Mashamba yote ya Serikali ambayo  bado hayajatambulika aliagiza Kuudwa kwa kamati za kufuatilia Mashamba hayo zikiongozwa na Wakuu wa Wilaya.
Akitoa Taarifa ya Jumla ya mafanikio ya utafutwaji wa Mashamba hayo, Mkuu wa Mkoa Kusini Pemba Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdullah alisema Mkoa wa Kusini Pemba ulipewa jukumu la kuyatambua Mashamba 1,510.
Mh. Hemed alisema katika utafutaji huo Kamati iliyoundwa kufanya kazi hiyo ilifanikiwa kuyatambua Mashamba 1,356 sawa na asilimia 90% na Mashamba 154 bado yanaendelea kutafutwa.
Kwa upande wa Mkoa wa Kaskazini Pemba akiwa Kaimu Mkuu wa Mkoa huo Mh. Hemed alisema Mashamba 1,924 yalipaswa kutambuliwa ndani ya Mkoa wa Kaskazini Pemba kwa mujibu wa Takwimu zilizopatikana ndani ya Vitabu vya Kumbukumbu.
Alisema zoezi hilo lilifanikiwa kubainisha  Mashamba 671 ndani ya Mkoa wa Kaskazini Pemba ikiwa ni sawa na asilimia 35% na Mashamba 1253  ambayo bado hayajaonekana.
Mh. Hemed Suleiman Abdullah alisema Kamati zilizoundwa zilitekeleza majukumu yao kwa ueledi mkubwa licha ya baadhi changamoto zilizojichomoza na kupelekea kazi hiyo kuongezwa muda wa Miezi Mitatu badala ya Miwili.
Mkuu huyo wa Mkoa Kusini Pemba aliiomba Jamii kuendelea kuviamini vyombo vya Ulinzi pamoja na Ushauri vinavyotoa na kuepukwa tabia za dharau na kebehi zilizoonyeshwa na baadhi ya Watendaji wa Taasisi za Umma wakati wa kuendeshwa kwa zoaezi hilo la uhakiki wa Mashamba ya Serikali.
“ Zipo dharau nyingi zilizojitokeza wakati wa zoezi hilo zilizofanywa na baadhi ya Watendaji wa Taasisi za Umma wakiwemo pia Wananchi, lakini ieleweke kwamba Uongozi wa Kamati za Ulinzi kamwe hautaridhia kukebehiwa Mashauri yake”. Alisisitiza Mh. Hemed.
Alibainisha kwamba Kamati ye yote inayoundwa na Serikali kamwe  haielekezi mwenendo wa kudhulumu Mwananchi. Hivyo alishauri endapo yapo maelezo na mapendekezo iwe ya Mwananchi na hata Taasisi za Umma yanapaswa yakawasilishwa kwa utaratibu uliowekwa wa Kiserikali.
Wakitoa Taarifa za ufafanuzi wa kina kutokana na ufuatiliaji wa Mashamba ya Serikali ndani ya Wilaya Nne za Pemba Wakuu wa Wilaya hizo walisema uhakiki wao umebainisha baadhi ya Mashamba hayo kutumiwa kwa shughuli nyengine zisizo za Kilimo.
Walisema yapo Mashamba yaliyofanywa Makaazi ya Watu, kutumika katika Ujenzi wa Majengo ya shughuli za Kijamii kama Skuli, Vituo vya Afya Miradi ya Maji pamoja na kupitishwa Bara bara kwa matumizi ya harakati za huduma za Mawasiliano.
Nao kwa upande wao Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kitaifa iliyopewa jukumu la  kutafuta na kuyahakiki Mashamba yote ya Serikali Balozi Amina Salum Ali, Mh. Mmanga Mjengo Mjawiri, Mh. Ali Juma Khatib, Mh. Said Soud, Mh. Shamata Shaame Khamis walitahadharisha kwamb muhali kwa baadhi ya Watu unaweza kuviza zoezi hilo.
Wajumbe hao walisema kutokuwajibika ipasavyo miongoni mwa Watendaji wa Taasisi za Umma kunachangia migogoro na matatizo yanayoweza kuepukwa mapema ili kufanikisha kazi ya Kamati hiyo na hatimae Serikali kuu ifikie lengo iliyolikusudia.
Hata hivyo walipongeza hatua kubwa iliyofikiwa ya utafutaji wa Mashamba yote ya Serikali yaliyo nje ya umiliki hasa kutokana na ushirikiano mzuri ulifikiwa kati ya Viongozi, Watendaji wa Taasisi za Umma, Wananchi na Vikosi vya Ulinzi na Usalama wa SMT na SMZ.
Walishauri Taarifa zilizotolewa na Wakuu wa Wilaya zote zilingane na kufafanua kwa kina matokeo ya Utafiti wao ili Serikali itakapokaa kwa ajili ya Uchambuzi zaidi ipate muelekeo halisi wa Namna ya kuyaratibu Mashamba yake yote hata yake iliyoaridhia kusimamiwa na Wananchi zikiwemo Eka Tatu Tatu.
Waziri wa Biashara na Viwanda Balozi Amina Salum Ali akitoa ushauri wa Ripoti za Wilaya zote zifanane ili Serikali itapofanya uchambuzi iwe kazi rahisi.
Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Mh. Mmanga Mjengo Mjawiri akizipongeza Kamati za Utafutaji Mashamba ya Serikali za Wilaya kwa kazi kubwa zilizofanya na hatimae kufanikiwa vyema.
Mkuu wa Mkoa Kusini Pemba Mh. Hemed Suleiman Abdullah akitoa Taarifa ya jumla ya upatikanaji wa Mashamba ya Serikali Mkoa wa Kusini na Kaskazini Pemba  hapo ukumbi wa Kiwanda cha Mafuta ya Makonyo Wawi chake chake Pemba.
Pich na – OMPR – ZNZ.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.