Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Rais wa Umoja wa Kamati za Olimpiki za Afrika,(ANOCA) Bw.Mustapha Berraf kulia akiwa na Ujumbe wake walipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo leo,17-11-2019,
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein amepongeza uwamuzi wa Umoja wa Kamati za Olympiki kwa
kuichagua Zanzibar kuwa mwenyeji wa mkutano wa Makatibu Wakuu wa Kamati za
Olympiki za Afrika (ANOCA).
Rais Dk. Shein
aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya
mazungumzo na Rais wa Umoja wa Kamati za Olympiki za Afrika Mustapha Berraf
akiwa amefuatana na Ujumbe wake.
Katika maelezo yake
Rais Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo kuwa uwamuzi wa Kamati hiyo ya Olympiki
(ANOCA) kwa kushirikiana na Kamati ya Olympiki ya Tanzania (TOC) ni uwamuzi wa
busara kwani unaendeleza mahusiano na mashirikiano mazuri yaliopo katika sekta
ya michezo kwenye nchi za Bara la Afrika.
Pamoja na hayo, Rais
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais huyo wa Umoja wa Kamati za
Olympiki za Afrika Mustapha Berraf kwa kuchaguliwa kushika wadhifa huo na
kueleza imani yake kwamba mafanikio zaidi yatapatikana katika Bara la Afrika
kwenye sekta ya michezo.
Aidha, Rais Dk. Shein
alieleza haja kwa Umoja huo kwa mashirikiano na Kamati ya Olympiki ya Tanzania ushirikiane
na Wizara ya Vijana, Utamaduni Sanaa na Michezo
pamoja na Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale kutayarisha michezo
ya Kimataifa na mashindano mengine hapa Zanzibar kwa lengo la kuimarisha sekta
ya utalii, ajira kwa vijana, mashirikiano, amani pamoja na kujenga afya.
Rais Dk. Shein pia
alieleza haja kwa Umoja wa Kamati za Olympiki za bara la Afrika (ANOCA) kwa
mashirikiano ya Kamati za Olympiki Tanzania (TOC) na Kamati ya Olympiki ya
Kitaifa (IOC) kutoa ufadhili wa mafunzo kwa makocha wa michezo mbali mbali ikiwemo
riadha, mpira wa miguu na mengineyo.
Rais Dk. Shein pia,
alimueleza kiongozi huyo mwenye asili ya nchi ya Algeria, kuwa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ina uhusiano mzuri na wa kihistoria kati yake na Algeria
hivyo hatua hiyo itajenga zaidi mashirikiano na uhusiano uliopo.
Sambamba na hayo, Rais
Dk. Shein alimtaka kiongozi huyo pamoja na ujumbe wake kuitumia vizuri nafasi
hiyo ya kuja kufanya mkutano wao hapa Zanzibar kwa kuvitembelea vivutio mbali
mbali vya kitalii vilivyopo Zanzibar.
Rais Dk. Shein pia,
alimueleza kiongozi huyo juhudi za makusudi zinazochukuliwa na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya michezo ambayo inahistoria
kubwa hapa nchini.
Pia, Rais Dk. Shein
alitumia fursa hiyo kumueleza Rais huyo wa Umoja wa Kamati za Olympiki za
Afrika Mustapha Berraf historia ya Zanzibar katika anga za michezo na jinsi
ilivyotambuliwa ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hata hivyo Rais Dk.
Shein alimueleza kiongozi huyo na ujumbe wake kuwa majadiliano na maazimio yatakayofikiwa
katika mkutano huo yatakuwa chachu katika kuimarisha sekta ya michezo katika
Bara la Afrika.
Nae Rais wa Umoja wa
Kamati za Olympiki za Afrika Mustapha Berraf alimueleza Rais Dk. Shein azma ya
mkutano wao unaofanyika hapa Zanzibar katika Hoteli ya Verde na kueleza jinsi
walivyopata mapokezi mazuri yeye na wajumbe wengine wa mkutano huo.
Kiongozi huyo alitumia
fursa hiyo kuipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa
Rais Dk. Shein kwa kuendeleza na kuimarisha sekta ya utalii hapa nchini na
kueleza jinsi Zanzibar inavyovutia.
Hata hivyo, kiongozi
huyo wa Kamati ya Olympiki ya Bara la Afrika alimueleza Rais Dk. Shein
mashirikiano mazuri yaliopo kati ya Kamati anayoiongoza na ile ya Tanzania
hatua ambayo imepekea kufanikisha vyema mkutano huo.
Alisema kwamba mkutano
wao huo Mkuu wa 36 utakuwa wa siku mbili ulioanza leo na kuishia kesho ambao ulitanguliwa na mikutano iliyoanzia
Novemba 14 na 15 ambayo ilijumuisha nchi zinazozungumza Kiengereza na tarehe 19
na 20 mwezi huu kutakuwa na mkutano kwa nchi zinazozungumza lugha ya Kifaransa.
Alisema kuwa jumla ya
mikutano minne yote itawajumuisha wajumbe hao wakiwemo wajumbe wa (ANOCA),
(OS), (IOC) sambamba na matayarisho ya mashinadano ya Olympiki ya Tokyo 2020.
Kiongozi huyo ambaye pia,
ni Rais wa Kamati ya Kitaifa ya Olympiki ya Algeria alieleza kuwa mkutano huo
wenye wajumbe zaidi ya 150 wote wanatoka katika nchi 54 za Bara la Afrika
pamoja na baadhi ya nchi za Ulaya zikiwemo Japan, Switzerland, Hungary na
nyenginezo.
Kwa maelezo ya Rais wa
Kamati ya Olympiki Tanzania Gulam
Abdallah alisema kuwa mkutano huo pia, umehudhuriwa na Kamati ya Maandalizi ya
Olympiki 2020 Tokyo ambayo pia inashiriki katika mkutano huo ambapo pia mkutano
huo mbali ya mambo yake mengine pia utajadili shughuli za michezo ya Olympiki
kwa Bara la Afrika sambamba na matayarisho ya Olymki 2020 Tokyo.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment