Habari za Punde

MKATABA WA MAZINGIRA STOCKHOM UMEONESHA MWANGA UDHIBITI WA KEMIKALI HATARISHI

Na Ismail Ngayonga MAELEZO DAR ES SALAAM 12.5.2020                                               
MAENDELEO ya nchi yetu kwa kiasi kikubwa yanategemea matumizi endelevu ya maliasili zilizopo nchini uwepo wake hizi ni muhimu kwa ajili ya mahitaji ya sasa na ya vizazi vijavyo.

Hata hivyo, Taarifa ya Tatu ya Hali ya Mazingira Nchini ya mwaka 2019 imebainisha kuwepo kwa shughuli za kiuchumi na kijamii zisizo endelevu ambazo zimeendelea kuchangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira nchini.

Uharibifu huo ni pamoja na uharibifu wa ardhi, ukataji wa miti hovyo na uharibifu wa misitu, upotevu wa bioanuai, uchafuzi wa mazingira, uharibifu wa mifumo ikolojia ya maji, kupungua kwa ubora na upatikanaji wa maji na mabadiliko ya tabianchi.

Aidha, hivi karibuni kumekuwepo na ongezeko la viumbe vamizi, taka za kielektroniki, taka za kemikali, uchafuzi utokanao na shughuli za utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi, ambavyo kwa kiasi kikubwa vimechangia uharibifu wa mazingira na kuhatarisha afya ya binadamu na ikolojia kwa ujumla.

Katika kulinda, kuhifadhi na kukabiliana na changamoto za uharibifu wa mazingira nchini, Ofisi ya Makamu was Rais (Muungano na Mazingira), imeendelea kusimamia utekelezaji wa Sera, Sheria, Mikakati mbalimbali ya hifadhi ya mazingira na Mikataba ya Kimataifa ya Mazingira.

Katika kipindi cha mwaka 2019/20, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) imeendelea kutekeleza Mkataba wa Stockholm Kuhusu Udhibiti wa Kemikali Zinazodumu Katika Mazingira kwa Muda Mrefu na tayari Serikali imeandaa Mpango wa Kitaifa wa utekelezaji wa mwaka 2018-2023.

Akiwasilisha Hotuba ya Makadiro ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2020/21, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mussa Zungu anasema Mpango huu unafadhiliwa na Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) kwa gharama ya Tsh. bilioni 1.8 chini ya usimamizi wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP).

Waziri Zungu anasema kupitia mpango huo, Serikali iliratibu zoezi la ukusanyaji wa jumla ya sampuli 553 za mafuta ya transfoma zinazokisiwa kuwa na kemikali ya Polychlorinated Biphenyls (PCBs) ambazo zinadumu katika mazingira kwa muda mrefu na hivyo kuhatarisha afya ya binadamu na mazingira.

‘Sampuli hizi zilikusanywa kutoka katika mikoa ya Dodoma, Singida, Mwanza, Kilimanjaro, Arusha, Tanga, Pwani, Dar es Salaam na Morogoro na kwa pande wa Zanzibar, katika Mikoa ya Mjini Magharibi - Unguja na Kaskazini Pemba,  ambapo katika sampuli zilizokusanywa, sampuli 22 zilibainika kuwa na kemikali ya PCBs’’ anasema Waziri Zungu.

Kwa mujibu wa Waziri Zungu anasema kemikali hizo ni mojawapo ya kemikali zinazodhibitiwa chini ya Mkataba wa Stockholm ambazo zinapaswa kuondoshwa kwenye matumizi ifikapo mwaka 2025.

Aidha Waziri Zungu anasema sanjari na zoezi hili, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) imeendelea kuelimisha jamii kuhusu madhara yatokanayo na kemikali ya PCBs ambapo elimu ilitolewa kwa wananchi takriban 810 wakiwemo wafanyakazi 45 wa TANESCO waliopewa mafunzo ya namna bora ya kudhibiti kemikali hiyo.

Zungu anasema Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) pia imekamilisha na kuanza kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Kemikali na Taka Hatarishi wa mwaka 2020 – 2025 na kukamilisha Mfumo wa Kieletroniki wa Upatikanaji wa Taarifa za Kemikali na Taka nchini, ambapo hatua inayoendelea kwa sasa ni kutoa mafunzo kwa wataalam watakaokuwa wanatumia mfumo huo.

Waziri Zungu anasema Ofisi yake pia inatekeleza Mpango wa Kimataifa wa Ufuatiliaji wa Madhara ya Kemikali Zinazodumu Katika Mazingira Kwa Muda Mrefu (2017 – 2020), ambapo tayari Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu imekusanya sampuli 55 za maziwa ya wamama wanaonyonyesha na kutumwa nchini Ujerumani kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara.

‘Sampuli hizi zilichukuliwa katika mikoa ya Mbeya, Pwani, Arusha, Mwanza na Dodoma. Vilevile, sampuli 44 za hewa zilichukuliwa katika Mkoa wa Pwani na kutumwa nchini Uholanzi na Sweden kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara ili kubaini kiwango cha kemikali hizi katika hewa’’ anasema Waziri Zungu.

Udhibiti wa kemikali na kemikali taka ni muhimu katika kila sekta inayotumia kemikali ili kulinda  haki ya kikatiba ya kila mtanzania na azimio la Umoja wa Mataifa la haki za binadamu ya kuhakikishiwa mazingira bora ya kuishi kwa afya na familia yake.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.