Habari za Punde

Rais Dk Shein: Serikali itahakikisha hali ya amani na utulivu itaendelea kudumu baada ya uchaguzi mkuu

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dk.Ali Mohamed Shein alipokuwa kitoa hutuba yake ya kulivunja Baraza la 9 la wawakilishi la Zanzibar katika sherehe zilizofanyika leo Chukwani Nje ya Mji wa Zanzibar.[Picha na Ikulu.] 20/06/2020. 

                               STATE HOUSE ZANZIBAR
                        OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE

Zanzibar                                                     Juni 20, 2020


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema Serikali itaendelea kuhakikisha hali ya amani na utulivu iliopo nchini inaendelea kudumu kabla na baada ya uchaguzi mkuu ujao.


Dk. Shein amesema hayo leo katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Mbweni , nje kidogo ya Jiji la Zanzibar  wakati akilivunja Baraza la Tisa la Wawakilishi.


Alisema Serikali imetunga sheria ya Uchaguzi namba 4 ya mwaka 2018, kwa lengo la kuweka utaratibu bora wa Uchaguzi na kuondoa kasoro zote zilizojitokeza katika chaguzi zilizopita, hivyo ni wajibu wa Viongozi wa vyama vya siasa na wanachama kuheshimu, kazi na majukumu ya Tume za Uchaguzi nchini (ZEC na NEC), akibainisha vyombo hivyo vimeundwa kikatiba.


Alisema hatua yoyote ya kuchukua maamuzi kinyume na utaratibu uliowekwa na sheria, utasababisha zogo na kuanzisha fujo.


“Zogo na fujo ndio chanzo cha watu kugombana na hatimae kuingiana maungoni, hayo sio madhumuni ya uchaguzi, kwa hivyo uchaguzi wa Oktoba mwaka huu utakuwa huru na haki”, alisema.


Alitoa indhari kwa wale wenye nia ya mawazo ya kutaka kuharibu uchaguzi kwa njia yoyote ile au kufanya fujo,  waondokane na fikra hizo, kwani jambo hilo halitowezekana kwenye uchaguzi wa mwaka huu.


Aidha, aliwahakikishia wananchi kuwa sheria za uchaguzi, katiba pamoja na fedha za kuendesha uchaguzi huo zipo kutoka Serikalini  na kubainisha kuwa vikosi vya Ulinzi na Usalama viko makini kusimamia uchaguzi huo.


“Nawatangazia mimi na Dkt. John Pombe Joseiph Magufuli tupo macho, hatutasinzia seuze kulala, tutatekeleza wajibu wetu na watakaofanya vituko dhidi ya sheria  tutawashughulikia”, alisema.


Aidha, Rais Dkt. Shein alisema Serikali imeamua kuzifungua skuli zote za maandalizi, msingi na Sekondari Unguja na Pemba kuanzia Jumatatu ya Juni 29, mwaka huu.


Alisema hatua hiyo inatokana na hali ya ugonjwa wa Corona hivi sasa kuwa shwari kuliko ilivyokuwa mwezi wa April, Mei na wiki ya mwanzo ya mwezi wa Juni, akibainisha kutowepo kwa mgonjwa hata mmoja katika vituo vyote vilivyokuwa vikiwatibu wagonjwa Unguja na Pemba.


Alisema ni muda wa siku kumi umepita tangu mgonjwa wa mwisho kutoka katika vituo hivyo, hali inayobainisha kuwa ni shwari.


Hata hivyo, aliitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya amali kuandaa mipango madhubuti na kabambe ya namna bora zaidi kwa wanafunzi wanapokuwa masomoni, ikizingatiwa mazingira ya madarasa mengi kuwa na idadi kubwa ya  wanafunzi.


Vile vile,  aliutaka uongozi wa Kampuni za Boti na meli zinazosafiri kati ya Zanzibar na Dar es Salaama pamoja na Unguja , Pemba na Tanga kuhakikisha zinachukua abiria kwa mujibu ya viti ya vyombo vyao kama ilivyosajiliwa , kuanzia  Juni 29, mwaka huu.


“Abiria hawataruhusiwa kusimama au kukaa popote wakiwa safarini, Serikali itachukua hatua dhidi ya Kapteni na kukifungia chombo chochote  kitakachokiuka mashart haya”, alisema.


Aliitaka Wizara ya ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Mamlaka ya Usafiri Baharini (ZMA) pamoja na Shirika la Bandari kusimamia utekelezaji wa maagizo hayo sambamba na kuhakiki ‘manifesto’ za wasafiri wote wanaopanda na kushuka ili kujiridhisha.


Aidha, Dk. Shein aliwataka wafanya biashara kufanya shughuli zao kwa nidhamu pamoja na kuruhusu shughuli za kijamii kuendelea kama kawaida; ikiwemo arusi, maulidi, hitma na kadhalika, huku akiwataka wananchi kuzingatia taratibu na kanuni za Afya kama inavyoshauriwa na wataalamu ili kuepuka maambukizi, akibainisha virusi vya Covid 19 kuwa bado havijamalizika kabisa.


Kuhusiana na michezo, Dk. Shein alisema Serikali imeruhusu kuendelea kwa mchezo ya mpira wa miguu pekee katika ngazi za Ligi kuu na Premier, na kuwataka wanamichezo mingine wakiwemo wa riadha pamoja na mazoezi ya viungo kuvuta subira..


Katika hatua nyengine, Dk. Shein aligusia maendeleo ya kiuchumi nchini katika kipindi cha miaka 10 ya uongozi wake, na kusema Serikali imeendelea na juhudi za kutekeleza mipango ya kiuchumi ili kuhakikisha ustawi wa wananchi wa Zanzibar unaimarika.


Akinukuu  vifungu mbali mbali  kutoka Ilani ya Uchaguzi mkuu ya CCM ya mwaka 2010 na mwaka 2015, Dk. Shein alisema Ilani iliielekeza Serikali kujenga mazingira yatakayowezesha uchumi wa Zanzibar  kufikia kiwango cha uchumi wa nchi zenye kipato cha kati.


“Ilani ilielekeza kuhakikisha mfumko wa bei unabaki katika tarakimu moja na wastani wa pato la kila mwananchi linaongezeka”, alisema.


Aidha, alisema Ilani ilielekeza mapato yaendelee kudhibitiwa pamoja na kuwepo nidhamu katika matumizi ya Serikali, kupunguza utegemezi wa wahisani wa maendeleo, misamaha ya kodi isiyokuwa na tija, sambamba na kuongezeka kwa kiwango cha ukusanyaji wa mapato ya ndani.


Alisema katika kipindi hicho cha miaka 10, Pato la taifa limeweza kukua  kutoka thaamni ya shilingi Bilioni 1.7 (mwaka 2010) hafi kufikia thamani ya shilingi Bilioni 3, ikiwa sawa na mara 1.74, zaidi ya wakati Awamu ya saba ikiingia madarakani.


Alielelza kuwa kasi ya ukuaji uchumi nayo imeongezeka kutoka asilimia 4.3 (2010) hadi kufikia asilimia 7.0 mwaka 2019.


Vile vile, alisema Pato la mwananchi nalo limeongezeka kutoka shilingi 942,000 (USD675) mwaka 2010 hadi kufikia shilingi 2,549 (USD1,114) mak 2019, ikiwa sawa na asilimia 170.59.


Aidha, alisema mfumko wa bei ulishuka kutoka asilimia 14.7 (2011) hadi asilimia 2,9 mwaka 2019, na kubainisha hali hiyo imeleta faraja kubwa kwa wananchi kwani wameweza  kupata bidhaa muhimu kwa bei ya kuridhisha.


Nae, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, akitoa shukuran kwa Rais Dk. Shein alimtakia afya njema, umri mrefu na mapumziko mema baada ya kulitumikia Taifa kwa mafanikio makubwa.


Aidha, alimkabidhi Dk. Shein zawadi za sheria zote 128 zilizopitishwa na Baraza hilo katika kipindi cha Uongozi wake, pamoja na zawadi ya umbo linalofanana na  jengo la Baraza la wawakilishi, kwa ajili ha kumbukumbu yake.


Hafla hiyo, iliyohudhuriwa na Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein, Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Majaliwa Kasssim Majaliwa, Makamu w aPili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai pamoja viongozi mbali mbali wa serikali, wastaafu na  baadhi ya mabalozi a nchi za nje. 


 Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822  

 E-mail: abdya062@gmail.com

1 comment:

  1. Unaondoka Zanzibar haijawa hata robo ya Dubai ulio tuahidi. Hatuna hata maji majumbani mwetu, umeme bado tunategemea Tanganyika, wakizima tunalala kiza

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.