Habari za Punde

Balozi Seif azitaka taasisi za ujenzi wa miundombinu kunusuru mmong'onyoko wa ardhi katika fukwe za Zanzibar

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiambatana na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Hassan Khatibu na Mkurugenzi wa Baraza la manispaa Mgharibi “B” Nd. Natepe wakiangalia mmong’onyoko wa ardhi katika eneo la pembezoni mwa Fukwe ya Mazizini.
 Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Nd. Mustafa Aboud Jumbe akielezea hatua iliyochukuliwa na Serikali katika uimarishaji wa Miundombinu mbali mbali ikiwemo uhifadhi wa Fukwe za Bahari.
 Balozi Seif Ali Iddi akiziagiza Taasisi zinazosimamia Ujenzi, Mazingira na Manispaa kuwa na muelekeo wa pamoja katika kukabiliana na mmong’onyoko wa Ardhi unaoyakumba maeneo tofauti Nchini.
 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mazingira Zanzibar Ndugu Sheha Mjaja akielezea umuhimu wa Timu za Mazingira kuendelea kuyalinda maeneo ya hifadhi.
 Balozi Seif Ali Iddi pamoja na Uongozi wa Taasisi za Ujenzi Mazingira na Serikali ya Mkoa wakilikagua eneo la Mazizini lililoathirika kutokana na kasi ya mawimbi la Bahari yaliyosababisha Bara bara ya eneo hilo kumong’onyoka.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameziagiza Taasisi zinazosimamia masuala ya Ujenzi wa Miundombinu, Manispaa, Mazingira na Serikali ya Mkoa Mjini Magharibi kuwa na muelekeo wa pamoja utakaozaa njia sahihi ya muda mrefu itakayonusuru Mmong’onyoko wa Ardhi katika fukwe za Zanzibar.
Alisema zipo athari nyingi zilizojitokeza za uchafuzi wa mazingira katika sehemu mbali mbali ya fukwe za Bahari pembezoni mwa Visiwa vya Unguja na Pemba akitolea mfano maeneo ya Msuka na Mazizini ambayo kwa sasa hayako katika hali ya kuridhisha Kimazingira.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa agizo hilo alipofanya ziara fupi ya kuangalia eneo la fukwe ya Mazizini ambalo limeathirika vibaya kutokana na kupanda kwa kina cha maji ya Bahari na kusababisha Bara bara iliyopita pembezoni mwa eneo hilo kumong’onyoka.
Alisema jamii imekuwa ikishuhudia uchafuzi wa mazingira unaoongezeka sehemu tofauti Nchini, licha ya baadhi ya maeneo kukumbwa na mabadiliko ya tabia Nchini lakini wakati mwengine husababishwa kwa makusudi na tabia za baadhi ya Watu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaeleza Viongozi pamoja na Wataalamu wa Taasisi hizo kuelewa kwamba wao kwa mamlaka na majukumu waliyopewa ndio wenye dhima ya kuhakikisha uchafuzi wa mazingira sambamba na Mmong’onyoko wa Ardhi unaondoka au kupungua hapa Nchini.
Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Nd. Mustafa Aboud Jumbe alisema Serikali kupitia Wizara hiyo tayari zimeshatiliana saini Mkataba na Kampuni ya China inayojenga Bara bara ya Bububu hadi Mkokotoni kwa ajili ya ujenzi wa Miradi Mitatu hapa Nchini.
Nd. Mustafa alimueleza Balozi Seif miradi hiyo ni pamoja na Mtaro wa Maji machafu wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume, Daraja ya Upenja kuelekea Kiwengwa pamoja na ujenzi wa Ukuta wa kuzuia maji ya Bahari utakalindwa na mawe makubwa pembezoni mwa Fukwe ya Mazizini.
Alisema Mradi huo wa ukuta utakwenda sambamba na bomba ya kupitishia maji machafu na ya mvua yanayotiririka kuingia pwani ya Mazizini  ili kuzuia mmong’onyo wa ardhi kwa mujibu wa ushauri wa Wataalamu wa Taasisi za Mazingira.
Naye kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mazingira Zanzibar Ndugu Sheha Mjaja katika kufanikisha suala hilo ipo haja ya kuwepo kwa Timu Maalum itakayopewa jukumu la kulinda eneo hilo  kwa hatua ya kwanza  ili kuzuia uvamizi wa kimazingira unaowez kuharibu azma ya uiimarishaji wa eneo hilo.
Nd. Mjaja alisema kutokana na athari za mabadiliko ya tabia Nchi zinazoendelea kuathiri sehemu mbali mbali za Dunia ni vyema miradi yinayoanzishwa ya kunusuru mmong’onyoko wa Ardhi ikalenga kudumu kwa kipindi kirefu ili kupunguza gharama kubwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.