Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais Mhe Hemed amuagiza RC Kaskazini Ungujua kuufanyia mapitio mradi wa maua Kijiji cha Kibumbwi

Mkurugenzi wa Jumuiya ya Kiislamu ya Al – Fatah  Sheikh  Rashid Salim Mohammed akielezea huduma zinazotolewa na Taasisi yake kwa Jamii ikiwemo Madrasa, Misikiti, Huduma za Maji na Skuli wakati Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman alipofanya ziara katika Kijiji cha Kibumbwi na Kipandoni Wadi ya Upenja.
Baadhi ya Wananchi wa Kijiji cha Kibumbwi kiliomo ndani ya Wadi ya Upenja Jimbo la Mahonda wakimsikiliza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman alipowatembelea kujua changamoto zinazowakabili.

Bibi Vatima Amour Zonge wa Kijiji cha Kibumbwi akielezea changamoto zinazowakabili Watoto wao za ukosefu wa Jengo la Skuli kwa Elimu ya Msingi ambapo hulazimika kufuata elimu Upenja na Kiwengwa.

Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Shughuli za Serikali SMT na SMZ anayesimamia Mfuko wa Tasaf Nd. Khalid Bakar Amran akielezea fursa wanazoweza kuzipata Wananchi wa Kijiji cha Kibumbwi wakati wa kuanza kwa Tasaf Awamu wa Tatu Kipindi cha Pili.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman akiwahakishia Wananchi wa Kijiji cha Kibumbwi kasi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane ilivyojipanga kuwasogezea Maendeleo katika maeneo yao.
Wananchi wa Kijiji cha Kipandoni wakishangiria na kufurahia ujio wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman kwenye Kijiji chao.
Bibi Maryam Kombo wa Kijiji cha Kipandoni ndani ya Wadi wa Upenja akimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed changamoto ya ukosefu wa Skuli ya Msingi kwa Watoto wao.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman akisalimiana na Wananchi wa Kijiji cha Kipandoni alipofika kuangalia changamoto zinazowakabili.

Picha na – OMPR – ZNZ.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla ,amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja kufanya mapitio ya Mradi wa maua uliwekezwa ndani ya Kijiji cha Kibumbwi katika kipindi cha mwezi mmoja na ripoti yake kuwasilishwa katika ngazi ya Juu kwa hatua zitakazofuata.

Makamu wa Pili wa Rais, aliyasema hayo alipotembelea kijiji cha Kibumbwi Jimbo la Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja kujionea hali halisi ya mazingira ya kijiji hicho, pamoja na kujua changamoto mbali mbali zinazowakabili wananchi wake.

Alisema malalamiko ya Wananchi waliobahatika kufanya kazi ndani ya Mradi huo bila ya tija wala kipato yamethibitisha kwamba muwekezaji wa Mradi huo wenye muda takriban miaka 15 sasa hauna  mafanikio yoyote kwa Wananchi wa eneo hilo jambo ambalo ni kinyume na malengo ya Serikali kuu ya kukaribisha Wawekezaji kwa faida ya Jamii.

Mh. Hemed Suleiman alionya kwamba ili kuhakikisha Muwekezaji huyo anafanyakazi kwa kuheshimu  maslahi ya wananchi, na endapo akishindwa Serikali inahaki ya kumuondoa na kukaribishwa muwekezaji mwengine.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewataka wananchi wa kijiji hicho kutoa mashirikiano kufuatia ahadi zilizotolewa na Wakuu alioambatana nao  ambao wanasimamia Miradi ya kijamii kama Bara bara, Umeme, Maji Safi, Elimu ambayo imekuwa changamoto kupatikana katika kijiji chao.

Mheshimiwa Hemed amewatahadhisha viongozi taasisi hizo na wale wa mkoa na wilaya, kwamba ahadi walizozitoa kwa wananchi hao, ndani ya muda wa Miezi Mitatu pindipo miradi hiyo haitokamilika atalazimika kuwachukuliwa hatua viongozi hao kwa kushindwa kukamilisha ahadi zao.

Akitoa maelezo Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mheshimiwa Ayoub Muhamed Mahmoud ,alisema mwanzoni wa mwaka ujao wanategemea wanafunzi wa Kijiji hicho wataanza kusoma katika skuli ilojengwa katika eneo hilo.

Hatua hiyo ya dharura ni jambo la msingi ambalo litawasaidia wanafunzi kupunguza changamoto ya kufuata huduma ya elimu masafa ya mbali Kiwengwa na Upenja sambamba na kuwaepusha na wimbi kubwa la vitendo vya udhalilishaji lililoibuka katika Jamii dhidi ya  watoto.

Aidha Mheshimiwa Ayoub, amemuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, watayafanyia kazi maelekezo aliyoyatoa kwa muda ili kuhakikisha wananchi wa kijiji hicho wanaondokana na changamoto zote zinazowakabili.

Mapema wananchi wa kijiji cha kibumbwi walimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, changamoto zinazowakabili, ikiwemo ukosefu wa maji, umeme, kituo cha afya, na skuli.

Wananchi hao walimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, kufurahishwa kwao  ujio wake wa kuwatembelea na kusikiliza changamoto zao zinazowakabili, jambo ambalo linawapa faraja na matumaini kwa awamu ya nane inayoongozwa na Dr. Hussein Ali Mwinyi.

Aidha wananchi hao wameishukuru Jumuiya ya Al - fattah kwa kuwafikishia misaada na huduma mbali mbali za kijamii, ikiwemo msikiti, madrasa na nyumba tatu za Wananchi wenye mazingira magumu , katika kijijini hapo.

Katika ziara hiyo Mheshimiwa Hemed pia ametembelea kijiji cha Kipandoni,wilaya ya kaskazini B, na kusikiliza changamoto zinazowakabili wananchi hao, ikiwemo kusuasua kwa mradi wa umwagiliaji, changamoto ya maji, pamoja na skuli.

Mkurugenzi Msaidizi anaesimamia kilimo wa halmahsauri ya Wilaya ya kaskazini B alisema mradi Umwagiliaji utakamilika mwezi machi mwakani, na kuwataka wananchi kuwa wavumilivu kwani serikali imeweka mkataba na kampuni inayosimamia mradi huo uliofikia hatua ya asilimia 60 ili baadae kuwasaidia wananchi hao.   

Akitoa salamu Makamu wa Pili wa Rais mheshimiwa Hemed Suleiman Abdullah, aliwataka viongozi wanaohusika na changamoto hizo  wanatafuta njia muwafaka wa kuzitatua na pale itakaposhindikana wa wajibu wa kuziwasilisha ngazi ya juu ya Serikali.

Mapema Mkurugenzi wa Jumuiya ya Kiislamu ya Al – Fatah  Sheikh  Rashid Salim Mohammed alisema Taasisi yao imekuwa inayotowa huduma za Kijamii kusaidia Wananchi wenye mazingira magumu Mijini na Vijijini Unguja na Pemba.

Sheikh Rashid ameipongeza na kuishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuthamini juhudi za Taasisi hiyo jambo ambalo limeleta faraja kwa Watendaji wa Taasisi hiyio ya Kijamii.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.