Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Atembelea Nyumba za Maafa Nungwi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman akiwa katika ziara ya kukagua maendeleo ya Ujenzi wa nyumba za Wananchi waliokumbwa na Maafa  zinazojengwa Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Mkurugenzi wa tume ya kuratibu na udhibiti wa dawa za kulevya zanzibar Kheriyangu Mgeni Khamis Kulia  akimpatia maelezo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Muheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla aliyefanya ziara fupi kituo cha matibabu kwa waathirika wa dawa za kulevya kinachoendelea kujengwa Kidimni Wilaya ya Kati.
Mheshimiwa Hemed akiangalia vifaa mbali mbali vilivyohifadhiwa Stoo kwa ajili ya ukamilishaji wa Mradi huo ambapo ujenzi utaendelea mara tu baada ya kuingizwa fedha kwa ajili ya kukamilisha jengo hilo.
Mh. Hemed akimkumbusha Mkandarasi wa Ujenzi wa Nyumba Hizo Mhandisi  Ernest Mbangula kuhakikisha Mradi huo unakamilika katika muda uliopangwa kwa mujibu wa Mkataba.
Muonekano wa Nyumba za Wananchi walioathirika na Maafa zinazojengwa kwa Ufadhili wa Mwezi Mwekundu chini ya Usimamizi wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar huko Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unaguja.

Mh. Hemed akitoa onyo Mtu yeyote atakaekaa katika nyumba hizo kiujanja ujanja kinyume na utaratibu Serikali haitasita kumchukuliwa hatua dhidi yake.

                                    Picha na – OMPR – ZNZ.

Na.Othman Khamis.OMPR.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Muheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla, ameuagiza uongozi wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar, kuhakikisha nyumba zilizojengwa kwa ufadhili wa Shirika la msaada la Mwezi Mwekundu wanapewa walengwa.

Mheshimiwa Hemed Suleiman aliyasema hayo wakati wa ziara ya kukagua nyumba hizo zinazojengwa Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja zinazosimamiwa na Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar, ikiwa ni katika ziara zake za kuikagua miradi iliyo chini ya Ofisi yake.

Alisema wapo viongozi wanaotumia majina ya viongozi wakuu wa serikali katika kujipatia huduma zisizostahiki kwao, na kusisitiza kuwa yeyote atakaekaa katika nyumba hizo kinyume na utaratibu atachukuliwa hatua dhidi yake.

Aidha amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Ungunja kufanya utaratibu wa kuweka eneo maalum la kukoshea maiti katika sehemu hiyo, ili wakaazi wa kijiji hicho waweze kulitumia eneo hilo.

Muheshimiwa hemed amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishajikuandaa mazingira yatakayowezesha kufikia eneo hilo hata kwa kifusi, ili iwe na hadhi ya kutumia wananchi wa eneo hilo. Sambamba na kumtaka afanye utaratibu wa kuweka uzio katika eneo hilo.

Akitoa ufafanuzi kuhusu huduma ya maji kufika katika eneo hilo,  Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Makame Khatib Makame, alisema suala hilo wameshafanya mawasiliano na Mamlaka ya Maji Zanzibar ZAWA na wamehakikisha ndani ya wiki mbili huduma hiyo itakuwa imefika katika makazi hayo

Eneo hilo la nyumba za maafa linalojengwa nungwi mkoa wa kaskazini unguja, lina jumla ya nyumba 58, msikiti,na skuli yenye madarasa saba,maabara na chumba cha walimu

Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Muheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla amekagua kituo cha matibabu kwa waathirika wa dawa za kulevya Kidimni, na kujionea namna maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho ulivyofikia.

Mh. Hemed ameiagiza Mamlaka ya Kuzuwia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA), kuchunguza gharama za mradi huo, ambapo hadi sasa mradi huo umegharimu shilingi billion 2.7, na kuongeza kuwa gharama zilizotumika ni kubwa tofauti na hatua iliyofikiwa.

Aidha aliwataka viongozi mbali mbali wa serikali kuacha tabia ya kutegemea miradi kwa kujipatia maslahi binafsi na badala yake kuendelea kuisimamia ili miradi hiyo iwe ya kiwango na ikamilike ndani ya muda muafaka.

Ameuagiza uongozi wa Wakala wa Majengo ya Serikali kupitia tena mradi huo kwa kuangalia gharama zilizobaki, ili kupunguza kiwango cha  gharama kubwa kilichopo.

Nae Mkurugenzi wa tume ya kuratibu na udhibiti wa dawa za kulevya zanzibar Kheriyangu Mgeni Khamis, alisema vifaa kwa ajili ya ukamilishaji wa Mradi huo vimeshanunuliwa, kilichositisha ni matumizi ya jengo hilo kwa wagonjwa wa covid 19 , ambapo ujenzi utaendelea mara tu baada ya kukabidhiwa fedha kwa ajili ya kukamilisha jengo hilo,ambapo  kukamilika kwa jengo hilo kunahitajika jumla ya shilingi bilioni 1.9

Kituo cha matibabu kwa waathirika wa dawa za kulevya kidimni kinategemea kugharimu shilingi billion 4 za kitanzania hadi kukamilika kwake

Ujenzi wa kituo hicho kina jumla ya majengo matatu,jengo la huduma za tiba, jengo la ofisi na jingo la eneo la kufulia

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.