Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais Mhe.Hemed Suleiman Azungumza na Ujmbe wa Benki ya Equity.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na uongozi wa Benki ya Equity ulioambatana na viongozi wa wizara ya Habari, vijana, utamaduni na michezo uliofika Afisni kwake Vuga kwa ajili ya kuwasilisha mpango maalum wa kuwasaidia wananchi wa zanzibar hususani wafanyabiashara wa kati pamoja na wajasirimali wadogo wadogo katika kuwawezesha kwa kuwapatia mitaji.
Na.Othman Khamis.OMPR.

Uongozi wa Benki ya Equity umetakiwa kutoa mafunzo maalum kwa walengwa ili kuwajengea uwezo wa kuendesha miradi wanayokusudia kuianzisha kabla ya kuwapatia mikopo inayotolewa na taasisi hiyo ya fedha kwa lengo la kubadilisha hali za kimaisha kwa wananchi wanaoishi ndani ya visiwa vya Unguja na Pemba.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alitoa ushauri huo wakati akizungumza na uongozi wa Benki ya Equity ukiambatana na viongozi wa wizara ya Habari, vijana, utamaduni na michezo uliofika Afisni kwake Vuga kwa ajili ya kuwasilisha mpango maalum wa kuwasaidia wananchi wa zanzibar hususani wafanyabiashara wa kati pamoja na wajasirimali wadogo wadogo katika kuwawezesha kwa kuwapatia mitaji.

Mhe. Hemed alisema kuna umuhimu mkubwa kwa taasisi za kifedha nchini kutambua kuwa jambo la muhimu na msingi katika kuwawezesha wananchi hasa vijana kujikomboa na umaskini, taasisi hizo zina jukumu la kutoa mafunzo yatakayowajenga vijana kujitambua mapema kabla ya kuanza kwa mchakato wa kufanya biashara.

Alisema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuunga mkono jitihada zinazochukuliwa na uongozi wa benki ya Equity kwani kufanya hivyo kutasaidia kwa kisai kizuri katika kuwawezesha na kuwajengea uwezo wananchi kushiriki katika kulipia kodi itakayosaidia kuinua uchumi wa Nchi mara baada ya kuwezeshwa kwa kuwa na mazingira mazuri kimaisha.

“Lazima tuwawezeshe wananchi wetu wawe na mazingira mazuri ya kibiashara ili waweze kulijenga Taifa lao kwa kulipa kodi ili kuinua uchumi wa Taifa”. Alieleza Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifafanua kuwa serikali itaandaa mazingira mahsusi ya kuzikutanisha wizara husika kwa lengo la kuzitatua na kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazowakabili wadau sambamba na wajasiriamali ili lengo la serikali la kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi wake liweze kufikiwa.

Pamoja na mambo mengine Mhe. Hemed ameishauri taasisi hiyo ya kifedha kuweka masharti nafuu juu dhamana wanazotakiwa kuweka wananchi wakati wakiomba mitaji ikiwa pamoja na kupunguza viwango vya faida wakati wa marejesho kwani kufanya hivyo kutatoa fursa zaidi kwa watu wengi kujitokeza kupata mitaji.

Wakiwasilisha mada Mkurugenzi mtendaji wa Benki ya Equity  Bi Esther Kitoka na Mkuu wa Biashara Bi Isabela  Mganga walisema  Benki ya Equity ilioanzishwa mnamo mwaka 2012 imelenga zaidi katika kuwanyanyua kiuchumiu wajasiriamali wadogo wadogo na watu wa kipato cha chini ambao bado hawajafikiwa na Mabenki mengine hapa nchini wakiwemo wakulima na wavuvi.

Walimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa mbali na mafanikio kadhaa walioyapata ikiwemo kuanza kutoa mikopo kwa vikundi mbali mbali zanzibar lakini vinakabiliwa na changamoto lakini vingi walivyovifikia bado havijapatiwa usajili hali inayorudisha nyuma jitihada zao za kuwawezesha vijana waliojikusanya katika vikundi hivyo.

“Katika Utendaji wetu wa kazi tumefanikiwa kuvikusanya jumla ya vikundi Sitini (60) lakini katika hivyo vikundi Kumi tu (10) ndio vyenye usajili na vinaweza kukopesheka” Alifafanua Bi Esther

Nae Mtaalamu wa masuala ya Uchumi na mshauri wa masula ya usimamizi wa biashara, uwekezaji na masoko kwa sekta binafsi na serikali  kutoka taasisi ya Luwigo Trust Tanzania Dk. Godwin Maimu alisema yupo tayari kutoa ushari katika masuala mbali mbali kwa lengo la kukuza uchumi wa wananchi wa kipato cha chini lakini alisisitiza haja ya kuondolewa kwa urasimu na mlolongo mrefu  katika kuvisajili vikundi ili viweze kuwezeshwa na taasisi za kifedha. 

Benki ya Equity yenye makao Makuu yake nchini Kenya inaendelea kutoa huduma  katika nchi za Uganda,  Ruwanda, Congo na Sudani Kusini  ikiwa tayari na  jumla ya matawi Kumi na Nne (14) Tanzania na imejipanga kutoa huduma zake katika Ukanda wa Afrika nzima.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.