SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR
HOTUBA YA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA YA OFISI YA RAIS, FEDHA NA MIPANGO KWA MWAKA WA FEDHA 2021/2022
MHE. JAMAL KASSIM ALI
WAZIRI NCHI OFISI YA RAIS, FEDHA NA MIPANGO JUNI, 2021
YALIYOMO UKURASA
UTANGULIZI.........................................................................................1 MUUNDO WA OFISI YA RAIS, FEDHA NA MIPANGO ........................3 MAJUKUMU MAKUU YA OFISI YA RAIS, FEDHA NA MIPANGO ........3 UTEKELEZAJI WA MAPATO NA MATUMIZI YA OFISI YA RAIS FEDHA
NA MIPANGO KWA MWAKA WA FEDHA 2020/2021........................4 Mapato ya Ofisi ya Rais Fedha na Mipango..................................4 Matumizi ya Ofisi ya Rais Fedha na Mipango ................................5 UTEKELEZAJI WA BAJETI ZA TAASISI ZA OFISI YA RAIS, FEDHA
NA MIPANGO KWA JULAI 2020-MACHI 2021...................................12
Bodi Ya Mapato Zanzibar (ZRB)........................................................12
Mfuko wa Barabara(ZRF) ..................................................................13 Mamlaka ya Ununuzi na Uondoaji wa Mali za Umma(ZPPDA) ....13
Mfuko Wa Hifadhi Ya Jamii Zanzibar(ZSSF)......................................16
Benki ya Watu w a Zanzibar (PBZ)....................................................17
Shirika La Bima (ZIC)...........................................................................18 MWELEKEO WA BAJETI KWA TAASISI ZINAZOSIMAMIWA NA OFISI
YA RAIS, FEDHA NA MIPANGO ..........................................................19 Bodi ya Mapato Zanzibar..................................................................19 Mfuko wa Barabara...........................................................................20 Mamlaka ya Ununuzi na Uondoaji wa Mali za Umma ..................20 Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar................................................21 Benki ya Watu w a Zanzibar PBZ.......................................................21 Shirika la Bima la Zanzibar.................................................................23 MWELEKEO WA BAJETI YA OFISI YA RAIS, FEDHA NA MIPANGO
KWA MWAKA 2021-2022 ....................................................................24 Vipaumbele vya Ofisi ya Rais Fedha na Mipango ........................24 Makadirio ya Mapato ya Ofisi ya Rais Fedha na Mipango..........25 Makadirio ya Matumizi ya Ofisi ya Rais Fedha na Mipango.........25 Matumizi ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Ofisi ya
Rais, Fedha na Mipango kwa mwaka 2021/2022..........................26 SHUKRANI ............................................................................................26 HITIMISHO ............................................................................................26
OR-Fedha na Mipango i
A. UTANGULIZI
1.0 Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Muumba mbingu na ardhi kwa kutujaalia neema ya uhai na kutuepusha na kutuhifadhi majanga ya kilimwengu ikiwemo maradhi, vita na maafa yanayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa ulimwenguni.
2.0 Mheshimiwa Spika, naomba kuchukua nafasi hii pia kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa imani yake kwangu iliyompelekea kunikabidhi jukumu la kusimamia Ofisi yake muhimu inayoshughulikia Fedha na Mipango ya Nchi yetu. Aidha, napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru wasaidizi wakuu wa Rais wetu ambao ni Makamo wa Kwanza wa Rais Mheshimiwa Othman Masoud Othman na Makamo wa Pili wa Rais Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla ambao wanashirikiana nae kwa karibu katika kuimarisha umoja na mashirikiano ambayo ni chachu kwa maendeleo ya nchi yetu .
3.0 Mheshimiwa Spika, naomba nikushukuru wewe binafsi, ukiwa Spika wa Baraza hili, Naibu Spika Mheshimiwa Mgeni Hassan Juma na Wenyeviti wa Baraza; Mheshimiwa Shaaban Ali Othman na Mheshimiwa Mwanaasha Khamis Juma, kwa jinsi mnavyoshirikiana kuliongoza vyema Baraza hili wakati wote. Pia, natoa shukrani za dhati kwa Kamati ya Uchumi ya Baraza lako tukufu inayoongozwa na Mwenyekiti wake Mheshimiwa Shaaban Ali Othman, Makamo wake na wajumbe wote. Ofisi yetu inafarijika kwa kupokea ushauri na mashirikiano makubwa tunayoyapata kutoka kwao ambayo yanazidisha ufanisi katika kutekeleza majukumu ya kazi zetu za kila siku.
OR-Fedha na Mipango 1
4.0 Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee nachukua nafasi hii kuwashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo la Magomeni kwa kunichagua kwa imani kubwa na kunipa nafasi kuwa muwakilishi wao katika Baraza hili. Waliniamini kuwa Mbunge wao kwa miaka mitano na kwa sasa wameniamini tena na kunichagua kuwa mwakilishi wao katika Baraza hili. Nawaahidi sitawaangusha, nitakuwa nao pamoja wakati wote kwa ajili ya maendeleo ya Jimbo letu na nchi yetu kwa ujumla.
5.0 Mheshimiwa Spika, Naomba kuchukua nafasi hii kuungana na wananchi wenzangu wa Zanzibar kuwaombea dua viongozi wetu ambao tulikuwa nao pamoja wakati tunalianza Baraza hili la kumi (10) na leo hii wameshatutangulia mbele ya haki. Viongozi hawa wametujengea hamasa kubwa kutokana na weledi, umakini, uaminifu na uadilifu wao katika kazi utumishi wao ambao umetuwezesha kupiga hatua kubwa ya maendeleo. Kwa hakika viongozi hawa wametufunza namna bora ya kulitumikia taifa letu. Mwenyezi Mungu awalaze pema peponi Marehemu Mzee wetu Maalim Seif Sharif na Mzee wetu Dkt. John Pombe Magufuli (Ameen).
6.0 Mheshimiwa Spika, naomba kutoa shukrani maalum kwa watendaji wa Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango kwa mashirikiano wanayonipa katika kutekeleza majukumu yangu ya Uwaziri katika Ofisi hii. Sote kwa pamoja tunathamini sana michango maoni na ushauri tunaoupata kutoka wadau wa Sekta tunayoisimamia pamoja na wananchi wote kwa ujumla.
7.0 Mheshimiwa Spika, baada ya shukrani sasa naomba uniruhusu kuwasilisha mbele ya Baraza hili Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango kwa mwaka wa Fedha 2021/2022 kama ambavyo Katiba ya
OR-Fedha na Mipango 2
Zanzibar ya mwaka 1984 imeelekeza ndani ya kifungu cha 88 kifungu kidogo (b) na (d).
B. MUUNDO WA OFISI YA RAIS, FEDHA NA MIPANGO
8.0 Mheshimiwa Spika, Kimuundo Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango imeundwa na mafungu makuu matatu ambayo ni Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango (F01), Mfuko Mkuu wa Serikali (F02) na Tume ya Mipango (F03). Mafungu hayo yanajumuisha Idara kumi na tano (15), taasisi nane (8) zinazojitegemea na ofisi mbili (2) zinazoratibu shughuli za Wizara kwa upande wa Pemba.
C. MAJUKUMU MAKUU YA OFISI YA RAIS, FEDHA NA MIPANGO
9.0 Mheshimiwa Spika, Miongoni mwa majukumu ya Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango ni:
a. Kusimamia mapato ya Serikali kutokana na vyanzo mbali mbali. Mapato hayo yanajumuisha mapato ya ndani ya kodi na yasiokuwa ya kodi, Ruzuku na Mikopo kutoka kwa Mashirika ya Kimataifa na Nchi Wahisani;
b. Kusimamia mali za Serikali kupitia usimamizi wa ununuzi, utunzaji na uondoaji wa mali za Serikali pamoja na Hisa za Serikali katika Mashirika na Kampuni binafsi ambazo Serikali inamiliki;
c. Kusimamia Fedha za Umma na shughuli za Uhasibu Serikalini. Katika jukumu hili Ofisi inasimamia Bajeti ya Serikali, usimamizi wa Hazina, huduma za Uhasibu na ukaguzi wa ndani Serikalini;
d. Kusimamia Deni la Taifa kwa kutoa ushauri, kujadili deni na kufuatilia mwenendo wa Deni la Taifa (Mikopo ya Ndani na Nje) na udhibiti wake;
e. Ofisi inasimamia maendeleo ya Sekta ya Fedha, inayohusisha masuala ya Benki, Bima, Hifadhi ya Jamii,
OR-Fedha na Mipango 3
Soko la Hisa na Mitaji pamoja na usimamizi wa Taasisi za huduma ndogo ndogo za fedha; na
f. Kusimamia Teknologia ya habari na Mawasiliano (TEHAMA) kupitia mifumo inayohusisha mapato, matumizi na malipo ya Serikalini.
10.0 Mheshimiwa Spika, Kwa vile muundo wa Ofisi ya Rais Fedha na Mipango unajumuisha na Tume ya Mipango. Hivyo, Ofisi pia inatekeleza majukumu yafuatayo kupitia Tume ya Mipango:
g. Kuandaa na kusimamia utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa na kuitafsiri kwenye Mipango ya kipindi cha muda wa kati kwa kuzingatia idadi ya watu na mahitaji yake;
h. Kuratibu na kusimamia maendeleo ya uchumi kupitia Sekta za Kiuchumi na Kijamii;
i. Kuratibu Sera za Kisekta na upunguzaji wa umaskini nchini;
j. Kusimamia upatikanaji na utoaji wa takwimu rasmi kwa maendeleo ya nchi; na
k. Kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa mipango ya kitaifa na kimataifa.
D. UTEKELEZAJI WA MAPATO NA MATUMIZI YA OFISI YA RAIS, FEDHA NA MIPANGO KWA MWAKA WA FEDHA 2020/2021
D.1 Mapato ya Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango
11.0 Mheshimiwa Spika, kabla sijawasilisha muelekeo kwa upande wa ukusanyaji wa Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, kwa ruhusa yako naomba kuwasilisha muhtasari wa Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2020/2021 kama ifuatavyo: Ofisi hii ilipangiwa kusimamia na kukusanya Mapato yaliyokadiriwa kufikia jumla ya TZS 1.549 trilioni kutoka vyanzo mbali mbali.
OR-Fedha na Mipango 4
12.0 Mheshimiwa Spika, Kwa kipindi cha Julai hadi Machi mwaka wa fedha 2020/21, mapato halisi yaliyokusanywa na Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango yalifikia Jumla ya TZS 678.79 bilioni sawa na asilimia 44 ya makadirio ya mwaka ya kukusanya TZS 1.549 trilioni na pia ni sawa na asilimia 70 ya kukusanya TZS 965.73 bilioni ndani ya kipindi cha Julai 2020- Machi 2021. Uchambuzi wa mapato hayo ni kama ufuatavyo:
a. Bodi ya mapato ilikusanya TZS 223.3 bilioni sawa na asilimia 43 ya makadirio ya mwaka na pia ni sawa na asilimia 74 ya makadirio ya kipindi cha miezi tisa;
b. Mamlaka ya Mapato (TRA) imekusanya TZS 209.1 bilioni sawa na asilimia 55 ya makadirio ya mwaka na pia ni sawa na asilimia 92 ya makadirio ya kukusanya TZS 228.4 bilioni kwa kipindi cha miezi tisa;
c. Mapato kutoka kwa Washirika wa Maendeleo ya TZS 119.6 bilioni sawa na asilimia 29 ya makadirio ya TZS 419.4 bilioni kwa mwaka na sawa na asilimia 39 ya matayajio ya kupokea TZS 306.0 bilioni kwa kipindi cha miezi tisa. Kati ya Fedha hizo TZS 106.4 bilioni ni Mikopo na TZS 13.23 bilioni ni Ruzuku; na
d. Misaada ya Kibajeti (GBS) ya TZS 9.46 bilioni;
e. Fedha za Mfuko wa pamoja wa Washirika wa Maendeleo ni TZS 2.6 bilioni sawa na asilimia 68 ya makadirio ya mwaka ya kupokea TZS 3.9 bilioni.
f. Mapato yasiyokuwa ya kodi yaliyokusanywa na fungu F01-Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango ni TZS 51.06 bilioni sawa na asilimia 32 ya makadirio ya kukusanya TZS 159.9 bilioni, pia ni sawa na asilimia 96 ya makadirio ya kukusanya TZS 53.44 bilioni kwa kipindi cha miezi tisa.
D.2 Matumizi ya Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango
13.0 Mheshimiwa Spika, kwa upande wa matumizi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango ilipangiwa kutumia TZS 442.93 bilioni
OR-Fedha na Mipango 5
kwa mafungu ya Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango ya F01, F02 na F03 Kwa ujumla Mafungu haya yametumia TZS179.82 bilioni ambazo ni sawa na asilimia 41 ya makadirio ya TZS 442.43 bilioni ya mwaka. Kati ya fedha hizo, TZS 37.94 bilioni zilitumika kwa upande wa Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango (F01), TZS 136.47 bilioni zilitumika kwa matumizi ya Mfuko Mkuu wa Serikali (F02) na TZS 5.40 bilioni ni matumizi ya Tume ya Mipango (F03) .
14.0 Mheshimiwa Spika, Mchanganuo wa matumizi ya F01 na F03 kimafungu ni kama ifuatavyo:
i. Mshahara ni TZS 7.4 bilioni;
ii. Ruzuku kwa Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Rais Fedha na Mipango ni TZS 22.78 bilioni;
iii. Matumizi Mengineyo (OC) ni TZS 5.26 bilioni; na iv. Matumizi ya kazi za Maendeleo ni TZS 7.29 bilioni.
15.0 Mheshimiwa Spika, kwa upande wa matumizi program zinazosimamiwa kwa Fungu F01, fedha zilizotumika ni kama ifuatavyo:
a. Programu ya bajeti na Usimamizi wa Fedha za umma ilikadiriwa kutumia jumla ya TZS 47.48 bilioni. Hadi kufikia Machi 2021, program hii imetumia TZS 24.91bilioni sawa na asilimia 52 ya makadirio ya mwaka. Shughuli zilizotekelezwa ni pamoja na:
i. Kusimamia ukusanyaji wa mapato ya Serikali ya TZS 678.79 bilioni ambazo zimekusanywa kwa kipindi cha tathmini;
ii. Kuandaa na Kusimamia vikao 9 vya ukomo wa mapato na matumizi ya Serikali (Ceiling Committee); iii. Uimarishaji wa Mfumo wa Udhibiti wa Matumizi Serikalini – IFMlS na kuunganisha Mfumo huu katika Ofisi za Baraza la Mji Mkoani, Kaskazini A, Wilaya ya Kati, Manispaa za Mjini, Magharibi A na B;
OR-Fedha na Mipango 6
iv. Kuhudhuria vikao 12 vya Usuluhishi wa madeni ya nje baina ya Zanzibar na Tanzania Bara; na
v. Kuwapeleka mafunzo wafanyakazi 25 ili waweze kufanya mitihani ya IPSAS na CPA;
vi. Kufuatilia utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa kipindi cha miezi tisa (9);
vii. Kufanya Uhakiki na Ufatiliaji wa Malipo ya Mishahara kwa Idara Maalumu za SMZ;
viii. Kurekebisha mfumo wa malipo ya mishahara; ix. Kuandaa majukwaa la Bajeti na Uchumi kwa Serikali kuu na Serikali za Mitaa;
x. Kushiriki mikutano 4 ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani, kuendelea na maandalizi ya Mradi wa Kuimarisha Ukuaji wa Uchumi (BIG-Z);
xi. Kukamilisha kwa Ukaguzi wa Mfumo wa usimamizi wa matumizi (IFMS); na
xii. Kukamilisha kwa ripoti ya Ukaguzi wa ndani ya mwaka wa Fedha 2019/2020.
b. Pogramu ya Usimamizi na Uwekezaji wa Mali za Umma.
16.0 Mheshimiwa Spika, Lengo la programu hii ni Kusimamia mali za Serikali kupitia usimamizi wa ununuzi, utunzaji na uondoaji wa mali za Serikali pamoja na Hisa za Serikali katika Mashirika na Kampuni binafsi ambazo Serikali inamiliki. Programu hii imetumia TZS 6.93 bilioni sawa na asilimia 27 ya makadirio ya mwaka TZS 25.28 bilioni. Shughuli zilizotekelezwa ni pamoja na:
i. Ukaguzi, uhakiki na uthamini wa Mali za Serikali katika Wizara kumi na tatu (13) na taasisi zake;
ii. Kusimamia uondoshwaji wa mali chakavu katika Wizara kumi na tatu (13) na taasisi zake;
iii. Kukagua na kutathmini hesabu za mashirika ya Serikali na kufuatilia ukusanyaji wa Gawio la TZS 8.44 bilioni; na
OR-Fedha na Mipango 7
iv. Kulipia fedha za ujenzi wa jengo la Ofisi za Mahkama zinazojengwa Tunguu TZS 4.92 bilioni;
v. Kukamilisha mapitio ya Sheria ya Usimamizi wa Mitaji ya Umma ya mwaka 2002 na kukamilisha Mswaada wa Sheria mpya itakayoshika nafasi ya Sheria hii iliyopo sasa.
c. Programu ya Mipango na Uendeshaji wa Sekta ya Fedha.
17.0 Mheshimiwa Spika, Lengo la Programu hii ni kuimarisha uendeshaji wa shughuli za Sekta ya Fedha. Programu hii ilipangiwa kutumia jumla ya TZS 56.22 bilioni. Hadi kufikia Machi 2021, TZS 6.12 bilioni zimetumika sawa na asilimia 11 ya makadirio ya mwaka. Shughuli zilizotekelezwa ni pamoja na:
i. Kuratibu uendeshaji wa vikao 16 vya Kamati ya Uongozi, Kamati Tendaji na Kamati ya Ukaguzi;
ii. Kuratibu vikao 18 vya Bodi ya Zabuni;
iii. Kukarabati maeneo ya Ofisi za Unguja;
iv. Kuratibu vikao vya Uchambuzi wa takwimu za fedha za Serikali kuu hadi kufikia mwaka wa fedha 2019/2020 ; v. Kuratibu vikao 16 vya Bodi ya Rufaa na Baraza la Rufaa za Kodi la Zanzibar;
vi. Kukamilisha Mswaada wa Sheria ya Usimamizi wa Taasisi zinazotoa huduma ndogo za fedha; na
vii. Kuratibu Shughuli za Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango kwa upande wa Pemba.
d. Matumizi ya Mfuko Mkuu wa Serikali
18.0 Mheshimiwa Spika, program ya Usimamizi wa Mfuko Mkuu lengo lake ni kusimamia huduma za Mfuko Mkuu wa Serikali. Kwa kipindi cha Miezi tisa (Julai 2020 – Machi 2021), Programu
OR-Fedha na Mipango 8
ya Usimamizi wa Mfuko Mkuu wa Serikali imetumia jumla ya TZS 136.47 bilioni sawa na asilimia 57 ya makadirio ya kutumia TZS 239.23 bilioni kwa mwaka. Matumizi hayo yalitumika kwa kutekeleza shughuli zifuatazo:
i. Malipo ya Riba na Mikopo TZS ni 13.495 bilioni; ii. Malipo ya mafao ya Kiinua mgongo kwa wastaafu 885 wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni TZS 15.864 bilioni; iii. Malipo ya Pencheni kwa wastaafu 14,084 wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni TZS 22.783 bilioni; na
iv. Kulipa matumizi Mengineyo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni TZS 84.331 bilioni.
e. Programu ya Kuratibu Mipango ya Kitaifa na Maendeleo ya Watendakazi
19.0 Mheshimiwa Spika, Lengo la program hii ni kuimarisha uratibu wa mipango ya maendeleo ya Kitaifa na kufanya ufuatiliaji na tathmini wa mipango hiyo. Katika kipindi cha Julai 2020 – Machi 2021 programu hii imetumia jumla ya TZS 2.5 billioni sawa na asilimia 66.8 ya makadirio ya mwaka ya TZS 3.78 bilioni. Shughuli zilizotekelezwa ni pamoja na:
i. Dira ya Maendeleo 2050 imekamilika na imezinduliwa na Jumla ya nakala 600 zimechapishwa na kusambazwa kwa wadau;
ii. Rasimu ya Mpango wa Maendeleo wa muda wa kati 2021/25 rasimu imekamilika;
iii. Wafanyabiashara 50 wamepatiwa mafunzo juu ya uendeshaji biashara na utunzaji wa fedha ili kurasimisha biashara zao katika Wilaya ya ChakeChake Pemba.
iv. Ziara ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Programu/Miradi ya Maendeleo imefanyika kwa Unguja na Pemba na kutembelea miradi jumla ya miradi sitini na tano (65)
OR-Fedha na Mipango 9
pamoja na kuandaa ripoti;
v. Kufanya Tathmini ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya 2020 na kuiwasilisha kwa wadau mbalimbali;
vi. Kufanya Tathmini ya utekelezaji wa Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUZA III); na
vii. Kukamilisha Mfumo wa kielektroniki wa Ufuatiliaji na Tathmini.
f. Programu ya Usimamizi wa Uchumi Mkuu na Takwimu
20.0 Mheshimiwa Spika, Lengo la program hii ni kuandaa sera za kiuchumi na kufanya tafiti za kiuchumi na kijamii kutokana na vipaumbele vya Taifa. Hadi kufikia Machi 2021 programu hii imetumia jumla ya TZS 1.9 bilioni ambayo ni sawa na asilimia 11.3 ya makadirio ya mwaka ya TZS 17.35 bilioni. Shughuli zilizotekelezwa ni pamoja:
i. Kutoa ripoti kumi na tatu za hali ya uchumi Zanzibar; ii. Kuwapatia mafunzo Wafanyakazi 30 juu ya namna ya ukusanyaji wa taarifa za kiuchumi katika Sekta ndogo ya mazao;
iii. Kuwapatia mafunzo Wanahabari 20 wa vyombo mbalimbali kisiwani Pemba juu ya namna bora ya kuhabarisha umma kuhusu matokeo ya tafiti mbali mbali;
iv. Kukusanya taarifa za tafiti 320 za sekta ya uvuvi nchini kwa lengo la kuzitambua na hapo baadae kuzichakata na kushajiiisha matumizi ya matokeo yake katika kutatua chamgamoto mbalimbali za sekta ya uvuvi nchini;
v. Utayarishaji wa vipaumbele vya tafiti vya kisekta na kupata rasimu ya awali ya ajenda ya utafiti ya Zanzibar ya mwaka 2021-2026;
OR-Fedha na Mipango 10
vi. Kutayarisha maandiko kwa ajili ya kutafuta ufadhili wa shughuli za kujenga uwezo watafiti wa kutoka taasisi za utafiti , Taasisi za elimu ya juu pamoja na vitengo vya utafiti vya wizara;
vii. Ripoti mbalimbali za kitakwimu za kila mwezi, robo mwaka na mwaka zimetolewa kama vile ripoti za kila mwezi za Faharisi ya Bei ya Mlaji (Consumer Price Index - CPI) na ripoti ya takwimu za robo mwaka za takwimu za Pato la Taifa (Growth Domestic Product – GDP) ikiwa ni pamoja na kuwasilisha na kusambaza ripoti ya matokeo ya Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya wa mwaka 2019/2020(HBS 2019/2020).
g. Programu ya Utawala na Uendeshaji wa Tume ya Mipango
21.0 Mheshimiwa Spika, lengo la programu hii ni kusimamia shughuli za utendaji na utumishi ndani ya Tume ya Mipango na kuhakikisha kazi zote zinatekelezwa kwa umakini na ufanisi. Kwa mwaka 2020/2021 programu hii ilitengewa jumla ya TZS 2.55 bilioni, ambapo hadi kufikia Machi 2021, imetumia jumla ya TZS 913.20 milioni ambayo ni sawa na asilimia 35.76 ya makadirio. Utekelezaji kwa program ni kama ifuatavyo:
i. Wafanyakazi kumi na saba wamepatiwa mafunzo, kati ya hao wafanyakazi wawili mafunzo ya muda mfupi na wafanyakazi kumi na tano mafunzo ya muda mrefu katika fani zinazohusiana na kada zao;
ii. Jumla ya vikao vitatu vimefanyika kwa wadau Unguja na Pemba kwa ajili ya kukusanya maoni na kuboresha Mkataba wa Huduma kwa Umma wa Tume ya Mipango Zanzibar;
iii. Wafanyakazi thamanini na tisa wa Unguja na Pemba wamepatiwa mafunzo ya ndani (Inhouse training) kuhusiana na miongozo mbali mbali ya kisheria pamoja na Mfumo wa Upandishwaji Vyeo kwa Watumishi wa
OR-Fedha na Mipango 11
Umma;
iv. Vikao kumi na sita vimeratibiwa; vikiwemo Kikao kimoja cha Tume ya Mipango , kumi na nne bodi ya Zabuni na Tathmini na viwili Ukaguzi wa Hesabu za ndani; na
v. Kutoa huduma za kiutawala na kiuendeshaji zikiwemo usafiri, ununuzi wa mafuta, vifaa vya kuandikia, pamoja na ununuzi wa vitendea kazi.
E. UTEKELEZAJI WA BAJETI ZA TAASISI ZA OFISI YA RAIS, FEDHA NA MIPANGO KWA JULAI 2020-MACHI 2021
E.1 Bodi Ya Mapato Zanzibar (ZRB)
22.0 Mheshimiwa Spika, Bodi ya Mapato Zanzibar ni Wakala Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa kukusanya mapato yatokanayo na kodi. Kwa mwaka wa Fedha 2020/2021, ZRB ilikadiriwa kukusanya jumla ya TZS 516.73 bilioni. Hadi kufikia Machi 2021, Bodi ya mapato imekusanya jumla ya TZS. 223.34 bilioni sawa na asilimia 43 ya makadirio ya mwaka.
23.0 Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa matumizi, Bodi ya Mapato Zanzibar ilikadiriwa kutumia TZS 33.12 bilioni kwa ajili ya kutekeleza kazi zake. Hadi kufikia Machi 2021 Bodi ya Mapato Zanzibar imetumia jumla ya TZS 16.71 bilioni sawa na asilimia 50 ya makadirio ya mwaka. Kati ya Fedha hizo TZS 5.60 bilioni zimetumika kwa kazi za maendeleo na TZS 11.10 bilioni zimetumika kwa kazi za kawaida. Shughuli zilizotekelezwa nia pamoja na :
i. Kufuatilia ugomboaji wa madeni ya TZS 12.41 bilioni yaliyokuwa hayajalipwa kutoka kwa walipa kodi mbalimbali. Kwa kipindi cha miezi tisa jumla ya TZS 9.70 bilioni sawa na asilimia 78 ya madeni yote yalilipwa;
ii. Kukamilisha kutengeneza Mfumo wa ZRB wa Kukadiria
OR-Fedha na Mipango 12
Mapato yatakayokusanywa (A Robust Zanzibar Revenue Forecasting Model for Zanzibar Revenue Board);
iii. Kukamilisha kazi ya kutengeneza Kituo cha Huduma kwa Walipakodi (ZRB Contact Centre);
iv. Kusajili walipakodi wapya 896 sawa na asilimia 108 ya makadirio ya walipakodi 830 waliotarajiwa kusajiliwa; na
v. Kukamilisha na ujenzi wa jengo la Ofisi Pemba katika maeneo ya Gombani.
E.2 Mfuko wa Barabara (ZRF)
24.0 Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2020/2021 Mfuko wa Barabara umeendeleza jukumu la kuimarisha utunzaji wa fedha zinazokusanywa kwa ajili ya matengenezo ya barabara. Hadi kufikia Machi 2021, matumizi ya Mfuko yamefikia TZS 5.5 bilioni sawa na asilimia 36 ya makadirio ya mwaka ya TZS 15.14 bilioni. Kati ya matumizi hayo jumla ya TZS 3.5 bilioni zimetumika kwa matengenezo ya barabara kuu sawa na asilimia 44 ya makadirio ya mwaka ya TZS 8.04 bilioni, na TZS 1.1 bilioni zililipwa kwa kazi za matengenezo ya barabara za ndani sawa na asilimia 21 ya makadirio ya mwaka ya TZS 5.36 bilioni.
E.3 Mamlaka ya Ununuzi na Uondoaji wa Mali za Umma (ZPPDA)
25.0 Mheshimiwa Spika, Lengo la Mamlaka ni kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Ununuzi na Uondoaji wa Mali za Umma, namba 11 ya mwaka 2016. Kwa mwaka wa fedha 2020/2021, Mamlaka ya Ununuzi na Uondoaji wa Mali za Umma imepangiwa kukusanya jumla ya TZS 325.00 milioni kutoka katika vianzio vyake mbali mbali vya mapato. Hadi kufikia Machi 2021 Mamlaka imekusanya jumla ya TZS 94 milioni ambayo ni sawa na asilimia 29 ya makadirio ya mwaka.
OR-Fedha na Mipango 13
26.0 Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa matumizi, hadi kufikia mwezi Machi 2021, Mamlaka imetumia jumla ya TZS 833.00 milioni sawa na asilimia 43 ya kupokea ruzuku ya TZS 1.94 bilioni kwa ajili ya kutekeleza shughuli zake zikiwemo zifuatazo:
i. Kukagua taasisi 29 za ununuzi kama zifuatazo;- Wizara ya Ardhi, Nyumba na Nishati, (OR) Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa na Idara maalum za SMZ, Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Usafirishaji, Wizara ya Vijana Utamaduni Sanaa na Michezo, Tume ya Utumishi Serikalini, Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Wizara ya Kilimo Maliasili Mifugo na Uvuvi, Tume ya Kurekebisha Sheria, Tume ya Uchaguzi na Baraza la manispaa magharibi. Aidha, Mamlaka kwa upande wa Mashirika imekagua Shirika la Magazeti, Shirika la huduma za Maktaba, Baraza la Manispaa Magharib “B”, Shirika la nyumba Zanzibar, Shirika la Biashara (ZSTC), Shirika la Bandari Zanzibar, Bodi ya Uhaulishaji, Wizara ya fedha na Mipango (ujenzi wa nyumba za Kwahani), Halmashauri ya wilaya ya Micheweni pamoja na mapitio ya ripoti za tathmini, Baraza la manispaa mjini, Wakala wa Serikali wa uchapaji Unguja, Kamisheni ya Utalii Unguja, Ripoti za tathmini za taasisi nunuzi, Wakala wa Chakula Dawa na Vipodozi, Mamlaka ya mafunzo ya amali Unguja, Halmashauri ya wilaya ya Micheweni, Wakala wa Uchapishaji Pemba, Baraza la Mji Chake Chake na Kamisheni ya Utalii;
ii. Kufanya uchunguzi kwa Taasisi 5 za ununuzi na Uondoaji wa Mali za Umma. Kati ya Hizo ni Mamlaka ya Mafunzo ya Amali juu ya ujenzi wa uzio Vitongoji Pemba, maabara ya usindikaji chakula, ujenzi wa mji mpya wa Kwahani Zanzibar, Halmashauri ya wilaya ya micheweni juu ya ujenzi wa ukumbi (hall) na utekelezaji wa mikataba katika Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC);
OR-Fedha na Mipango 14
iii. Kuandaa na kutoa miongozo ya ununuzi na uondoaji wa mali za umma, Kutengeneza nyaraka za zabuni (standard bid documents) nane (8) Nyaraka zilizo andaliwa kama zifuatazo:
a. Nukuu za bei kwa bidhaa (Quotation national shopping of goods);
b. Nukuu za bei kwa kazi (Quotation national shopping of works);
c. Nyaraka ya ununuzi wa bidhaa (Standard tender document for procurement of general goods); d. Nyaraka za ununuzi wa huduma ya ushauri
elekezi wa kitaalamu kwa kampuni na mtu binafsi (Standard request for proposal (RFP) for selection of consultants under competitive and individual selection);
e. Nyaraka za ununuzi wa kazi (Standard tender documents for procurement of works);
f. Nyaraka za ununuzi wa kazi zenye thamani ndogo (Standard tender document for procurement of smaller works);
g. Nyaraka za ununuzi wa huduma ya ushauri elekezi usiokuwa wa kitaalamu kwa kampuni na mtu binafsi (Standard tender documents for procurement of non-consultancy services);
h. Nyaraka zinazotumika katika uondoaji wa mali za umma (Standard bidding document for disposal of fixed assets”).
iv. Kutoa mafunzo kwa taasisi 118 za Serikali juu ya miongozo ya Ununuzi na Uondoaji wa mali za Umma kwa Wakuu wa vitengo vya manunuzi, Kati ya hizo Unguja 86 na Pemba 32; na
v. Kuwajengea uwezo wafanyakazi wanne (4) mafunzo ya muda mrefu na watatu (3) muda mfupi.
OR-Fedha na Mipango 15
E.4 Mfuko Wa Hifadhi Ya Jamii Zanzibar - ZSSF
27.0 Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021 Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar umeendelea kutoa huduma kwa wanachama wake kwa kukusanya michango yao na kuwekeza fedha hizo katika miradi salama na yenye faida kwa lengo la kulipa mafao kwa wanachama muda unapofika kwa mujibu wa Sheria ya Mfuko Namba 10 ya mwaka 2016. Kwa mwaka wa fedha 2020/2021 Mfuko ulikadiria kukusanya mapato ya jumla ya TZS 145.20 bilioni kutoka katika vyanzo vikuu viwili. Hadi kufikia Machi 2021 Mfuko umekusanya jumla ya TZS 89.92 bilioni sawa na asilimia 61 ya makadirio ya mwaka. Kati ya mapato hayo michango ya wanachama ni TZS 57.23 bilioni sawa na asilimia 61 ya makadirio ya TZS 93.61bilioni na mapato kutoka katika uwekezaji wa Mfuko ni TZS 32.69 bilioni sawa na asilimia 63 ya TZS 51.59 bilioni makadirio ya mwaka.
28.0 Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa matumizi Mfuko ulipanga kutumia Jumla ya TZS 145.20 bilioni. Kati ya fedha hizo TZS 9.36 bilioni ni gharama za uendeshaji, TZS 38. 26 bilioni kulipia Mafao ya wanachama wa Mfuko na TZS 97.58 bilioni kwa ajili uwekezaji. Hadi kufikia Machi 2021, Mfuko umetumia jumla ya TZS 89.92 bilioni sawa na asilimia 62 ya makadirio ya mwaka. Kati ya fedha hizo gharama za uendeshaji zilikuwa ni TZS 6.16 bilioni, TZS 33.32 bilioni ni malipo ya Mafao kwa wanachama na TZS 50.45 bilioni kwa ajili ya uwekezaji wa Mfuko.
E.5 Benki ya Watu wa Zanzibar - PBZ
29.0 Mheshimiwa Spika, Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) ni Taasisi inayomilikiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Benki hii inatoa huduma za benki ya Kawaida (Conventional) na
OR-Fedha na Mipango 16
huduma za Benki ya Kiislam (Islamic Banking). Kwa kipindi cha Julai 2020 hadi Machi 2021 benki ilitarajia kupokea kutoka kwenye vyanzo vyake vya riba na visivyo na riba TZS. 73.09 bilioni na kufanikiwa kupokea TZS 59.59 bilioni sawa na asilimia 82 ya makusanyo ya kipindi hicho. Makusanyo hayo ni upungufu wa asilimia 18 ya lengo, upungufu huu ulisababishwa na kuzorota kwa biashara hasa ya fedha za kigeni iliosababishwa na mripuko wa maradhi ya COVID 19.
30.0 Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa matumizi Benki ilitumia TZS 38.00 bilioni sawa na asilimia 76 ya makadirio ya TZS 49.70 bilioni iliyojipangia kwa kipindi cha tathmini. Matumizi ya Benki kwa kipindi hicho yalipungua kwa asilimia 24 ukilinganisha na makadirio, hali hii imesababishwa na kupungua kwa baadhi ya shughuli za kawaida za benki kutokana na kuzorota kwa biashara katika kipindi hicho. Mbali na changamoto za kibiashara zilizojitokeza, hadi kufikia Machi 2021 Benki ilifanikiwa kupata faida ya TZS. 21.6 bilioni amabayo ni upungufu kwa asilimia 8 ya lengo la TZS 23.42 bilioni.
31.0 Mheshimiwa Spika, Hadi kufikia Machi 2021, Benki ilifanikiwa kuongeza mikopo kutoka TZS 420.36 bilioni mpaka TZS 489.22 bilioni amabayo ni pungufu kwa asilimia 0.2 ya malengo ya kufikia TZS 490.36 bilioni. Rasilimali (Assets) zimeendelea kukua kutoka TZS 800.36 bilioni mpaka kufikia TZS 809.53 bilioni kwa mwezi wa Machi 2021. Aidha, amana za wateja (deposits) zimekua kwa asilimia 2 kwa mwezi wa Machi 2021 kutoka TZS 598.81 bilioni hadi kufikia TZS 610.27 bilioni na Mtaji wa benki umekua kutoka TZS 95.966 bilioni Julai 2020 hadi TZS 119.53 bilioni kwa mwezi wa Machi 2021, ongezeko hilo ni sawa na asilimia 5 ya kiwango kilichotarajiwa cha TZS. 114.14 bilioni.
OR-Fedha na Mipango 17
E.6 Shirika La Bima - ZIC
32.0 Mheshimiwa Spika, Shirika limeendelea na kazi ya kutoa huduma ya bima kwa wateja pamoja na kuongeza mapato kutoka vyanzo vyake mbalimbali. Katika kipindi cha miezi tisa Julai 2020 - Machi 2021 pamoja na kuwepo na changamoto mbalimbali katika soko la Bima Tanzania bado Shirika limeweza kukusanya jumla ya TZS 17.2 bilioni sawa na asilimia 59 ya makadirio ya kukusanya TZS 29.10 bilioni.
33.0 Mheshimiwa Spika, kwa Upande wa matumizi Shirika limetumia jumla ya TZS 12.7 bilioni ambayo ni sawa na asilimia 95 ya matumizi ya mwaka ya TZS 13.3 bilioni. Kati ya Fedha hizo matumizi ya kawaida ni TZS 5.9 bilioni na matumizi ya maendeleo ni TZS 6.8 bilioni. Shirika katika kipindi hicho Julai 2020 - Machi 2021 limetekeleza shughuli zake zikiwemo zifuatazo:-
i. Kulipa madai halali yaliyowasilishwa na yaliyohakikiwa ya TZS 5.3 bilioni kutoka kwa wateja wake walioathirika wa majanga mbalimbali ya ajali;
ii. Kulipa ujira wa TZS 1.5 bilioni kwa mawakala 87 na madalali 16 wanaofanya biashara ya kuuza Bima kwa niaba ya Shirika;
iii. Kununua vitendea kazi vyenye thamani ya TZS 35 milioni kwa matumizi ya watendaji wa Shirika;
iv. Kuchangia mtaji wa TZS 450 milioni Wizara ya Biashara na Viwanda ikiwa ni mtaji wa uanzishwaji wa kiwanda cha mwani Zanzibar; na
v. Utoaji wa gawio kwa Serikali lenye jumla ya TZS 400 milioni sawa na asilimia 80 ya makadirio ya TZS 500 milioni kutokana na faida iliyopatikana mwaka wa fedha 2019.
OR-Fedha na Mipango 18
F. MWELEKEO WA BAJETI KWA TAASISI ZINAZOSIMAMIWA NA OFISI YA RAIS, FEDHA NA MIPANGO
F.1 Bodi ya Mapato Zanzibar - ZRB
34.0 Mheshimiwa Spika, Bodi ya Mapato Zanzibar inaendelea na kazi ya uwakala wa Serikali wa kusanya mapato yatokanayo na vianzio mbalimbali vya kodi. kwa mwaka wa fedha 2021/2022, inakadiriwa kukusanya jumla ya TZS 525.10 bilioni kutoka katika vyanzo vilivyoainishwa katika kitabu cha Mswada wa Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2021/2022.
35.0 Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa Matumizi ZRB inaombewa kuidhinishiwa matumizi ya TZS 17.02 bilioni kwa ajili ya kutekeleza Shughuli zake za kawaida na Maendeleo. Kati ya fedha hizo TZS 15.75 bilioni ni ruzuku kutoka Serikali kuu na TZS 1.27 bilioni kutoka katika vyanzo vyengine ikiwemo kutoka TRA. Miongoni mwa kazi zitakazotekelezwa ni :
i. Kukusanya mapato ya Serikali ya TZS 525.1 bilioni; ii. Kuendelea kufanya Ukaguzi wa kodi katika Hoteli kubwa za Kitalii;
iii. Kufanya Ukaguzi wa Kodi katika kampuni za Sekta za Mawasiliano ya simu na Taasisi za Fedha;
iv. Kuanzisha Matumizi ya Mashine za Kielektroniki za Utoaji wa Risiti (EFD’s) baada ya kukamilika kwa hatua za majaribio;
v. Kuendelea kuwatambua na kuwasajili walipakodi wapya wapatao 1,000;
vi. Kuongeza ukusanyaji wa mapato kwa kuimarisha mifumo ya kielektroniki na taratibu za utendaji kazi; vii. Kuimarisha taratibu za utendaji kazi kwa kutumia mifumo ya kielektroniki;
viii. Kuongeza ubunifu katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA); na
OR-Fedha na Mipango 19
ix. Kuhamasisha Ulipaji Kodi kwa Hiari kwa kujenga utamaduni wa kulipa kodi na kupunguza gharama za uwajibikaji.
F.2 Mfuko wa Barabara - ZRF
36.0 Mhesimiwa Spika, Kwa mwaka wa fedha 2021/2022 Mfuko unaombewa kuidhinishiwa jumla ya TZS 14.64 bilioni. Kati ya fedha hizo, matengenezo ya barabara ni TZS 12.86 bilioni na TZS 1.78 bilioni kwa ajili ya uendeshaji wa Mfuko kwa kutekeleza shughuli zikiwemo zifuatazo:
i. Matengenezo makubwa ya kilomita tano (5 km) za barabara za Mjini Unguja yanayojumuisha upandishaji wa tabaka la lami (overlaying) na mitaro.
ii. Kukamilisha matengenezo makubwa ya barabara zenye jumla ya kilomita (22 km) za Kipapo-Mgelema Wambaa, Micheweni-Kiuyu na ile inayoelekea eneo la uwekezaji Micheweni.
iii. Kuweka taa za kuongozea magari (traffic lights) kwenye maeneo matano ya Unguja na Pemba.
F.3 Mamlaka ya Ununuzi na Uondoaji wa Mali za Umma - ZPPDA
37.0 Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Ununuzi na Uondoaji wa Mali za Umma itaendelea kutekeleza majukumu yake ya kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Ununuzi na Uondoaji wa Mali za Umma namba 11 ya mwaka 2016. Kwa mwaka wa fedha 2020/2021 Mamlaka hii inakadiriwa kukusanya TZS 444.42 milioni kutoka katika vianzio vyake vya mapato na inaombewa kuidhinishiwa matumizi ya TZS 2.15 bilioni ambayo ni ruzuku kutoka Serikalini kwa ajili ya kutekeleza shughuli zake zikiwemo zifuatazo:
i. Kufanya ukaguzi na uchunguzi wa ununuzi wa mali za umma kwa Serikali;
OR-Fedha na Mipango 20
ii. Kuandaa na kutoa miongozo ya ununuzi wa mali za umma;
iii. Kupokea, kuchunguza na kuamua juu ya malalamiko ya wazabuni katika zabuni za Umma;
iv. Kuendelea kuimarisha mashirikiano na Taasisi zinazojishughulisha na ununuzi na uondoaji wa mali za umma za Tanzana Bara.
F.4 Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar - ZSSF
38.0 Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka wa Fedha 2021 /2022 Mfuko wa Hifadhi ya Jamii unatarajia kukusanya jumla ya TZS 150.24 bilioni kutokana na vyanzo vikuu wiwili, kati ya fedha hizo TZS 93.61 bilioni ni makusanyo ya michango ya wanachama wa Serikali, Taasisi Binafsi na waliojiajiri wenyewe na TZS 56.63 bilioni kutokana na mapato ya uwekezaji wa muda mrefu na muda mfupi wa masoko ya fedha na mitaji.
39.0 Mheshimiwa Spika, Mfuko unategemea kutumia Jumla ya TZS 150.24 bilioni kwa matumizi yake ya mwaka 2021/2022. Kati ya fedha hizo TZS 9.36 bilioni zinategemewa kutumika kwa matumizi ya uendeshaji, TZS 40.13 bilioni kwa kulipia mafao ya wanachama na TZS 100.75 bilioni kwa ajili ya uwekezaji.
F.5 Benki ya Watu w a Zanzibar - PBZ
40.0 Mheshimiwa Spika, Kwa kipindi cha mwaka 2021 Benki imejipanga kufanikisha mambo yafuatayo katika kukamilisha malengo yake.
i. Rasilimali za benki zinatarajiwa kukua kutoka TZS 753.00 billioni hadi TZS 862.00 bilioni. Ukuwaji huu unatarajiwa kuchangiwa na ongezeko la mikopo kwa wateja kutoka TZS 419.00 bilioni hadi kufikia TZS 461.00 bilioni;
ii. Kwa uapande wa amana za wateja Benki inatarajia
OR-Fedha na Mipango 21
kuongeza amana zake kutoka kwa wateja wake hadi kufikia TZS 623.00 bilioni kutoka TZS 576.00 bilioni. Aidha, Mtaji unatarajiwa kukua kwa asilimia 16, kutoka TZS 107.00 bilioni hadi TZS 131.00 bilioni;
iii. Benki inatarajia kupata jumla ya mapato ya TZS 99.75 bilioni, na matumizi ya TZS 69.07 bilioni yanatarajiwa kutumika kwa mwaka 2021 kwa ajili ya riba na matumizi yasio ya riba;
iv. Benki inatarajia kupata faida ya TZS 31.00 bilioni kwa mwaka 2021 kulinganisha na faida ya mwaka 2020 iliopatikana TZS 18.00 bilioni ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 72.
41.0 Mheshimiwa Spika, Benki ya watu wa Zanzibar inatarajia kutekeleza shughuli zifuatazo kwa mwaka 2021:
i. kukamilisha tawi la Dodoma, Kigamboni, Tandika na kituo cha kutolea huduma Tandahimba, Mtwara, Kinyasini, Chwaka, Dunga, ZIPA na Gombani ili kupanua wigo wa huduma za kibenki ;
ii. Kufanya upembuzi yakinifu katika mikoa ya Mwanza, Arusha, Mbeya, Shinyanga na Tanga ili kuweza kufungua huduma za kibenki katika meneo hayo;
iii. Kuimarisha huduma za mawakala kwa ajili ya kurahisisha upatikanaji wa huduma za Benki nchi nzima na ili kuondoa tatizo la foleni kwenye Matawi ya Zanzibar;
iv. Kuanzisha kituo maalum cha huduma kwa wateja kitakachofanya kazi masaa 24 kwa lengo la kupokea na kufanyia kazi changamoto za wateja kwa wakati na haraka;
v. Kufungua vituo (maduka) ya kubadilisha fedha, bureau de change katika maeneo ya Paje, Nungwi, Airport Dar es Salaam na Unguja (Terminal III);
vi. Kuweka mashine sita za kutolea fedha katika maeneo ya Gombani, Konde, Mtambile, Amani, Maungani na
OR-Fedha na Mipango 22
Kinyasini; na
vii. Kutoa huduma kwa kadi za malipo (Master card). F.6 Shirika la Bima la Zanzibar - ZIC
42.0 Mheshimiwa Spika, Shirika la Bima kwa mwaka fedha 2021/22 linatarajia kukusanya jumla ya TZS 31.00 bilioni kutoka katika vianzio vyake vya mapato kwa kutekeleza mikakati ifuatayo:
i. Kutoa taaluma kwa Wananchi na taasisi mbalimbali juu ya suala la kujiwekea kinga mali zao kwa lengo la kuongeza idadi ya wateja wapya wa biashara zisizokuwa za magari katika mtandao wake.
ii. Kuzidisha mashirikiano na mawakala na madalali wanaofanya biashara ya bima kwa niaba ya Shirika. iii. Shirika kwa kushirikiana na mawakala na madalali
kutumia kikamilifu mfumo mpya wa Teknolojia “Smart Policy System” kwa kutoa huduma bora zaidi kwa Wananchi.
iv. Kuendelea kuwapatia Wafanyakazi mafunzo mbalimbali ya kuwajengea uwezo na kuboresha utendaji wa kazi zao.
43.0 Mheshimiwa Spika, kwa upande wa matumizi, Shirika kwa mwaka wa fedha 2021/22 limepanga kutumia jumla ya TZS 15.50 bilioni ikijumuisha matumizi yafuatayo:
i. Matumizi kwa kazi za kawaida za Shirika ni TZS 9.80 bilioni; ii. Matumizi kwa kazi za maendeleo ni TZS 5.70 bilioni ikijumuisha gharama za ujenzi wa jengo la Shirika Pemba
OR-Fedha na Mipango 23
G. MWELEKEO WA BAJETI YA OFISI YA RAIS, FEDHA NA MIPANGO KWA MWAKA 2021-2022
G.1 Vipaumbele vya Ofisi ya Rais Fedha na Mipango
44.0 Mheshimiwa Spika, Baada ya kutathmini miongozo inayotolewa na viongozi wa nchi yetu ikiwemo Dira 2050, Ilani ya Uchaguzi wa CCM ya mwaka 2025 na Hotuba ya Mheshimiwa Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliyoitoa katika uzinduzi wa Baraza la kumi la Wawakilishi aliyoitowa Barazani siku ya tarehe 11/11/2020 na kuzingatia mwenendo wa hali ya Uchumi wa nchi yetu pamoja na mwenendo wa hali ya Uchumi wa Dunia. Baada ya kuyazingatia yote hayo Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango imejipanga kutekeleza vipaumbele vifuatavyo:
i. Kusimamia ukusanyaji wa Mapato ya Serikali ya TZS 1.78 trilioni;
ii. Kuunda na Kusimamia Mifumo ya kielektroniki itakayorahisisha ukusanyaji wa Mapato, Bajeti na Matumizi ya Serikali;
iii. Kuanzisha kitengo maalum cha kuchambua taarifa za kibiashara (Business Inteligence Unit) ili kuweza kuzitambua taarifa hizo na kupata taarifa sahihi katika utozaji kodi ya Serikali;
iv. Kuimarisha kitengo cha Ufuatiliaji na tathmini ili kuweza kufuatilia utekelezaji wa miradi na shughuli za Serikali na kuweza kutoa tathmini halisi za utekelezaji;
v. Kutayarisha Mkakati wa Mawasiliano wa Mpango wa Maendeleo wa Muda wa Kati wa Zanzibar 2021-2025; vi. Kutafsiri Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050 na Mpango wa Maendeleo wa Muda wa kati kwa Lugha nyepesi za Kiswahili na Kiingereza;
vii. Kusimamia Utekelezaji wa Mfumo wa Kielektroniki wa Taarifa za Ufuatiliaji na Tathmini kwa ngazi zote; na
OR-Fedha na Mipango 24
viii. Kuandaa Sensa ya Watu na Makaazi 2022.
G.2 Makadirio ya Mapato ya Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango
45.0 Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2021/2022, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango inakadiriwa kukusanya jumla ya TZS 1.78 trilioni. Makusanyo hayo ni ongezeko la asilimia 15 ikilinganishwa na makadirio ya kukusanya TZS 1.549 trilioni yaliyopangwa kukusanywa kwa mwaka 2020/202.
G.3 Makadirio ya Matumizi ya Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango
46.0 Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka wa Fedha 2021/2022 Ofisi ya Rais Fedha na Mipango inakadiriwa kutumia TZS 402.13 bilioni kwa mafungu yanayosimamiwa na Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango na uchambuzi wake ni kama ifuatavyo:
i. Fungu F01 limekadiriwa kutumia TZS 170.00 bilioni; ii. Fungu F02 limekadiriwa kutumia TZS 208.99 bilioni na iii. Fungu F03 limekadiriwa kutumia TZS 23.15 bilioni.
47.0 Mheshimiwa Spika, naomba sasa uniruhusu kuwasilisha uchambuzi wa matumizi ya Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango kwa kuzingatia programu kama ifuatavyo:
a. Matumizi kwa fungu F01 yanakadiriwa kufikia TZS 170.00 bilioni ambazo zinatarajiwa kutumika katika utekelezaji wa programu kuu tatu (3) zifuatazo:
i. Programu ya Usimamizi wa Fedha za Umma na Bajeti inakadiriwa kutumia TZS 65.06 bilioni;
ii. Programu ya Usimamizi wa Mali za Umma inakadiriwa kutumia TZS 83.81bilioni; na
iii. Programu ya Utumishi na Uendeshaji wa Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango inakadiriwa kutumia TZS 21.14 bilioni.
b. Matumizi kwa fungu F02 yanakadiriwa kufikia TZS 208.98 bilioni ambayo yanategemewa kulipia viinua
OR-Fedha na Mipango 25
mgongo vya wastaafu, Pencheni, kulipia madeni ya Serikali pamoja na kulipia huduma nyengine za Serikali zinazolipwa kwa kupitia Mfuko Mkuu.
c. Matumizi ya fungu F03-Tume ya Mipango yanakadiriwa kufikia TZS 23.15 bilioni ambazo zinatarajiwa kutumika ili kutekeleza shughuli za Programu kuu zifuatazo:
i. Programu ya Uratibu Mipango ya Kitaifa na Maendeleo ya Watendakazi inakadiriwa kutumia TZS 4.85 bilioni;
ii. Programu ya Usimamizi wa Uchumi Mkuu, Tafiti na Takwimu inakadiriwa kutumia TZS 14.58 bilioni; na
iii. Programu ya Uendeshaji wa shughuli za Tume ya Mipango inakadiriwa kutumia TZS 3.72 bilioni.
48.0 Mheshimiwa Spika, pamoja na programu kuu nilizoziwasilisha Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango itatekeleza programu ndogo kumi na tisa (19) ambazo uchambuzi wake umewasilishwa katika rasimu ya Mswada wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya kazi za kawaida na kazi za maendeleo kwa mwaka 2021/2022 ukurasa F01-i hadi F03-11 “volume 2”.
G.4 Matumizi ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango kwa mwaka 2021/2022
49.0 Mheshimiwa Spika, pamoja na utekelezaji wa shughuli za kazi za kawaida, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango kwa mwaka 2021/2022 itatekeleza miradi saba (7) ya maendeleo ambayo inakadiriwa kutumia TZS 99.09 bilioni.
H. SHUKRANI
50.0 Mheshimiwa Spika, Matayarisho ya bajeti yamehusisha wadau wengi, wakiwemo watendaji wa Ofisi yangu na taasisi mbali mbali ambao tumeshirikiana kukamilisha suala hili.
OR-Fedha na Mipango 26
51.0 Mheshimiwa Spika, kwa misingi hiyo naomba kutoa shukrani zangu kama ifuatavyo: kwanza nianze kuwashukuru sana Watendaji wakuu wa Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango wakiongozwa na Katibu Mkuu Dkt. Juma Malik Akil, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Nd. Mwita Mgeni Mwita, Naibu Katibu Mkuu Fedha na Mipango, Ndugu Khamis Suleiman Mwalim na Naibu Katibu Mkuu Mifumo, Ndugu Rashid Said Rashid pamoja na Wakuu wa Taasisi, Idara na wafanyakazi wote wa Ofisi hii kwa mashirikiano wanayonipatia ambayo yanakuza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Ofisi hii. Aidha, nawashukuru sana Washirika wa Maendeleo wakiwemo: Benki ya maendeleo ya Afrika (ADB), Benki ya Dunia, IMF-Kanda ya Afrika Mashariki, Serikali ya Jamhuri ya China, Serikali ya Norway, IFAD na wengine wengi.
52.0 Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee nawashukuru sana wananchi wote wa Zanzibar kwa umoja na mashirikiano yao ambayo yamekuza utulivu na kupelekea nchi yetu kuwa ni nchi ya amani. Mheshimiwa Spika, mwisho lakini sio kwa umuhimu naomba tena nichukue nafasi hii kwa wananchi wa jimbo la Magomeni ambao walinichagua kuwa muwakilishi wao, nawashukuru pia kwa ustahamilivu wao ambao hunipa fursa ya kuendelea na majukumu mengine ya Serikali yetu.
I. HITIMISHO
53.0 Mheshimiwa Spika, Baada ya maelezo niliyoyatowa sasa naomba Baraza lako tukufu kuridhia maombi ya Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango kukusanya mapato ya TZS 1.78 trilioni kwa mwaka 2021/2022. Aidha, naliomba Barara lako kuidhinisha matumizi ya TZS 402.13 bilioni ili Ofisi iweze kutekeleza shughuli zilizopangwa kwa mwaka 2021/2022.
54.0 Mheshimiwa Spika, Maelezo na shughuli zitakazotekelezwa kwa mwaka 2021/2022 yanapatika katika kitabu cha pili
OR-Fedha na Mipango 27
(volume 2) cha Mswada wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Bajeti inayotumia programu (PBB) kwa mwaka wa Fedha 2021/2022-2023/2024 katika ukurasa wa F01-i hadi F03-11.
55.0 Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
JAMAL KASSIM ALI
WAZIRI WA NCHI,
OFISI YA RAIS, FEDHA NA MIPANGO,
ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment