Habari za Punde

Jeshi la Magereza Latakiwa Kuitunza Miradi Pamoja na Usimamizi wa Matumizi ya Fedha -Dk. Hussein Mwinyi.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwa na Mkewe Mama Mariam Mwinyi  wakitembelea Mradi za Nyumba za Makaazi za Watumishi wa Gereza la Mtego wa Simba Kingolwira, baada ya kuzizindua leo 15 /10/2021, ikiwa ni mmoja wa Miradi Minne aliyoizindulia leo katika Gereza hilo.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amelitaka Jeshi la Magereza Tanzania kuitunza miradi mbalimbali pamoja na kusimamia matumizi ya fedha zinazotolewa kuwezesha miradi hiyo inayoendelea kutekelezwa kwani kufanya hivyo kutakuwa ni kuenzi vizuri juhudi zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 

Mhe. Samia Suluhu Hassan.Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo hii leo Oktoba 15, 2021 mkoani Morogoro alipokuwa akizindua miradi minne ya maendeleo iliyo chini ya Jeshi la Magereza ikiwemo Kiwanda cha Maziwa, ujenzi wa Kituo cha huduma ya Mama na Mtoto, ujenzi wa ngome ya Gereza la Mkono wa Mara na mradi wa ujenzi wa Nyumba za Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi ametoa wito kwa kuwataka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuhakikisha miradi hiyo inatangazwa na kuwezeshwa hususani kiwanda cha Maziwa ili kiweze kupata malighafi nzuri zitakazowezesha kuzalisha bidhaa bora.

Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Tanzania, Meja Jenerali Suleiman Mungia amesema uzinduzi wa miradi hiyo ni hatua muhimu katika kutekeleza m aagizo na maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kulitaka jeshi hilo linajiendesha kwa kujitegemea.

Hafla hiyo ya Uzinduzi wa Miradi hiyo imefanyika Kingolwira, Mkoani Morogoro na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe. George Simbachawene, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Martin Shigela pamoja viongozi mbalimbali wa Serikali na Chama.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.