Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali
Mwinyi ameupongeza utayari wa Serikali ya Italia kuunga mkono juhudi za
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika utekelezaji wa mipango yake ya maendeleo.
Rais Dk. Mwinyi amesema hayo leo Ikulu Zanzibar katika mazunguzo kati yake na Balozi wa Italia nchini Tanzania Marco Lombardi, Ikulu Zanzibar.
Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi alipongeza azma ya Serikali ya Italia ya kushirikiana na Zanzibar katika kuhakikisha inaimarisha sekta zake za maendeleo ikiwemo sekta ya utalii ambapo nchi hiyo ni mdau mkubwa.
Rais Dk. Mwinyi alifahamisha kuwa Zanzibar kwa kipindi kirefu imekwua ikinufaika kutokana na kuwepo wka idadi kubwa ya wawekezaji na wageni kutoka nchi ya Italia.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi alimuahidi Balozi Lombardi kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuweka mazingira mazuri katika kuhakikisha wawekezaji na wageni wanaotoka nchi hiyo pamoja na nchi nyengine duniani wanatekeleza shughuli zao katika mazingira yanayokidhi matarajio yao.
Rais Dk. Mwinyi aliipongeza azma ya Serikali ya Italia kuongeza huduma za usafiri wa anga kwa kuleta ndege kutoka kampuni kubwa kubwa za nchi hiyo ambazo zitafanya safari zake moja kwa moja kati ya Zanzibar na Italia.
Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba hatua hiyo itaimarisha zaidi hali ya uchumi na biashara hapa Zanzibar.
Pamoja na hayo, Dk. Mwinyi alimueleza Balozi Lombardi kuwa bado Zanzibar ina fursa kadhaa ambazo wawekezaji wa nchi hiyo wanakaribishwa kuzitumia zikiwemo kuendeleza sekta za uchumi wa Buluu, ujenzi wa nyumba za kisasa na majengo ya biashara, kuendeleza ujenzi wa viwanda, kuwawezesha wajasiriamali sanjari na kuliimarisha zao la mwani.
Pia,
Rais Dk. Mwinyi aliipongeza rai ya Balozi Lombard ya kuanzisha vyuo vya ufundi
vitavyowasaidia vijana katika sekta ya ajira ikiwa ni pamoja na ufundi. katika
masuala ya mambo ya utalii.
Mapema Balozi Balozi wa Italia nchini Tanzania Marco Lombardi alimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba Serikali ya Italia inaziona juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hivyo, iko tayari kuendelea kuziunga mkono.
Balozi Lombardi alimuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kwamba Italia itaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakikisha sekta ya utalii inaimarika hapa nchini.
Katika kuhakikisha azma hiyo inafikiwa, Balozi Lombardi alimueleza Rais Dk. Mwinyi azma ya ubalozi huo kufanya kongamano kubwa la biashara mnamo mwezi wa Septemba mwaka huu 2022 hapa Zanzibar ili kujadili fursa mbali mbali za uchumi zilizopo.
Aidha, alimueleza Rais Dk. Mwinyi azma ya Kampuni kubwa za nchi hiyo kufanya safari zake za ndege moja kwa moja na sio zile za msimu kama ilivyo kwa hivi sasa hatua ambayo itaimarisha zaidi sekta ya utalii na biashara.
Sambamba na hayo, Balozi huyo wa Italia alimueleza Rais Dk. Mwinyi mikakati iliyoiweka katika kuanzisha vyuo vya ufundi hapa hapa Zanzibar ambavyo, pamoja na mambo mengine, vitasaidia katika kuimarisha sekta ya utalii.
Balozi Lombardi alimuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kwamba Serikali yake itaiunga mkono Sera ya Uchumi wa Buluu ili kuhakikisha Zanzibar inapiga hatua na kufikia malengo iliyojiwekea.
Imetayarishwa na Kitengo cha Habari
Ikulu Zanzibar.
No comments:
Post a Comment