Habari za Punde

Jeshi la Polisi kuhakikisha linafanya uchunguzi wa hali ya juu ili kumkamata mtuhumiwa-Waziri Pembe.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar Mhe, Riziki Pembe Juma, akimsalimia Mtoto Andrea Benard aliyelazwa katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Unguja Jijini Zanzibar akiunguza majaraha aliyoyapata kwa kumwagiwa maji ya moto na mtu asiyejulikana wakati akiwa amelala usiku nyumbani kwao na kupata majeraha sehemu ya usoni na mkononi.  


WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe, Riziki Pembe Juma, ameliomba Jeshi la Polisi kuhakikisha linafanya uchunguzi wa hali ya juu ili kumkamata mtuhumiwa aliehusika kumuunguza maji ya moto mtoto wa miaka saba.

Kauli hiyo ameitoa wakati alipomtembelea mtoto huyo  katika wodi ya watoto Hospitali ya Rufaa Mnazimmoja kutokana na kujeruhiwa na maji hayo.

Amesema ni jambo la msingi kwa jeshi hilo kushirikiana na Wizara yao kuona mtuhumiwa aliyefanya kitendo hicho cha unyama na cha  udhalilishaji anakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Aidha amesema kumuunguza mtoto ambae hana hatia haipaswi kuvumiliwa na kwamba inaonekana wazi aliyefanya tukio hilo hatoki maeneo ya mbali wa maeneo wanayoishi.

Amesema ikiwa jeshi hilo litatumia nguvu zao na utalamu walionao hana shaka mtuhumiwa aliyetenda tukio hilo atakamatwa ili kuona haki ya mtoto huyo inapatikana .

“Naliomba jeshi lifanye kazi yake kwa nguvu zote naamini mnafanya kazi ila katika hili nawaombeni sana tuchukue hatua kuona mtuhumiwa anapatikana ili iwe mfano kwa wengine,” alisisitiza.

Waziri Riziki amesema binafsi yeye ni mzazi,  analaani tukio hilo kwa nguvu zote na kuwaomba wanawake, walezi na wazazi kulaani vitendo vya aina hiyo ambavyo vina wadhalilisha watoto.

“Udhalilishaji sio kulawitiwa au kubakwa tu, kumhujumu mtoto wa jambo lolote lile nalo pia ni kumdhalilisha hasa  ukizingatia maadili yetu ya kizanzibari hatuishi katika hatua kama hii,” amesisitiza Mhe, Riziki 

Hata hivyo amewaomba madaktari kuendelea kumpa tiba mtoto huyo huku Wizara ikiendelea kushirikiana na familia na madaktari kuona kinachotakiwa katika usaidizi wanasaidia ili kuona mtoto huyo anarudi katika hali yake ya uzima na kuendelea na masomo yake.   

Naye Muuguzi kutoka Wodi ya upasuaji na watoto walioungua,  bi Rukia Seif Said amesema mtoto huyo wamempokea Mei 18 mwaka huu majira ya saa 7:00 za mchana akiwa na majeraha ya uso, mikono na katika bega.

Amesema hali ya mtoto huyo wakati anafikishwa hospitali hali yake ilikuwa sio nzuri na alipatiwa huduma ya kwanza na amekuwa akisafishwa vidonda vyake na hivi sasa anaendelea vizuri.

Kwa upande wake Mama Mzazi wa mtoto  Andrea Benard ambae ameunguzwa maji ya moto nae hakutaka kutajwa jina lake amesema wakati mtoto wake akiwa amelala katika chumba chake usiku wa manane walisikia akipiga kelele na kusema maji ya moto na walipofika walimkuta ameshaungua katika sehemu ya uso na mkono.

Alisema wakati alipokwenda kugusa godoro alikuta maji ya moto ambayo yamepenya mpaka chini na walitoka kwenda kwa sheha kwa ajili ya kutoa taarifa.

Aidha alisema wakati tukio hilo linatokezea hawakuweza kutoka kutokana na eneo wanalokaa hakuna hospitali na ilipofika asubuhi ndipo walipompeleka hospitali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.