Habari za Punde

Waziri Mhe Masauni na Mhe.Gwajima Waungana Sakata la Panya Road

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akizungumza na wakazi wa Chanika wakati wa mkutano wa hadhara ukihusiana na mapambano  ya  uhalifu wa panya road uliotokea siku kadhaa zilizopita ambapo katika mkutano huo aliwaasa wazazi kuwa makini na malezi ya Watoto.

Na Mwandishi Wetu

Mawaziri kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dkt. Dorothy Gwajima wameungana ikiwa ni juhudi za serikali kutatua tatizo la makundi ya Watoto wadogo wanaojihusisha na uhalifu maarufu kama panya road ambao siku kadhaa zilizopita walivamia maeneo ya zingiziwa yaliyopo Chanika na kujeruhi wananchi wa maeneo hayo pamoja na kupora vitu vya thamani ikiwemo simu na televisheni.

Wakizungumza mbele ya wananchi wa Chanika katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Zingiziwa viongozi hao walisisitiza azma ya serikali kupambana na changamoto ya panya road huku wakiwataka wazazi kuwa makini katika usimamizi wa malezi ya Watoto.

“Katika kuhakikisha hawa Watoto wetu wanafanya vinavyowahusu ikiwemo kusoma, Rais Samia Suluhu Hassan amehakikisha kuwa kila mtoto wa nchi hii anapata elimu na kusoma bure ametoa fedha shilingi bilioni 24.4 kwa mwezi katika kuboresha elimu ya  mtoto wa nchi hii, serikali tunawaomba wazazi washughulike na Watoto hao, hatutokubali kuona amani ya nchi hii inavurugwa na kundi la watu ambalo tayari washatengewa mipango maalumu ya kupata elimu kulingana na mahitaji yao” alisema Waziri Masauni

Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dkt. Dorothy Gwajima amewaasa wazazi kuwa na taarifa za maendeleo ya Watoto wao huku akisisitiza kuwepo na kamati maalumu katika mitaa zikihusisha wazazi ili kuweza kuona mzazi yupi ashughuliki watoto wake hadi kufikia hatua ya kusababisha matatizo katika jamii.

“Leo mzazi nikuulize mtoto mara ya mwisho alilala kwako lini, tukuonyeshe na sheria inayokupa mamlaka ya kumuangalia mtoto wako, tuna maafisa ustawi wa jamii wanaoshughulikia na matatizo ya Watoto kama hayo, Mheshimiwa Samia ametengeneza wizara hii ili serikali iweze kushughulikia matatizo ya jamii, hili la panya road ni tatizo, ina maana wazazi mmeshindwa kuwalea Watoto wetu mpaka wafikie kuleta matatizo katika jamii, nawaasa wazazi kuwa makini na Watoto wenu kwani sheria ipo inayowapa wajibu wa kuwalea watoto katika maadili mema” alisema Waziri Gwajima

Akizungumza katika mkutano huo Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Jumanne Muliro amesema mpaka sasa wamekamata jumla ya watuhumiwa wa matukio ya panya road 61 huku akisisitiza kuimarishwa ulinzi katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam kwa ushirikiano uliopo kati ya askari polisi na polisi jamii huku akiwaasa wananchi kutoa taarifa kwa mamlaka pindi waonapo hali ya hatari.

“Jeshi lenu la polisi  liko imara mpaka sasa watuhumiwa 61 tunawashikilia huku tukiendelea na doria katika maeneo mbalimbali, nawaomba wananchi tuwe wepesi wa kutoa taarifa kwa jeshi pindi mkiona changamoto za uhalifu katika maeneo mnayoishi, tuna polisi jamii huko tunaomba mshirikiane nao kuimarisha ulinzi” alisema RPC Muliro.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza na wakazi wa Chanika wakati wa mkutano wa hadhara ukihusiana na mapambano ya  uhalifu wa panya road uliotokea siku kadhaa zilizopita ambapo katika mkutano huo aliwaasa wazazi kusimamia malezi ya Watoto ambayo ni takwa la kisheria mzazi kumsimamia mtoto katika malezi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akizungumza na Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, ACP Muliro Jumanne(kulia) wakati wa mkutano wa hadhara na wananchi wa Chanika ikiwa ni muendelzo wa wa kupambana na uhalifu wa panya road. Katikati ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dkt. Dorothy Gwajima
Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, ACP Muliro Jumanne akizungumza na wakazi wa Chanika wakati wa mkutano wa hadhara ukihusiana na mapambano ya  uhalifu wa panya road uliotokea siku kadhaa zilizopita ambapo katika mkutano huo alisisitiza kuwepo kwa doria maalumu katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam lengo ikiwa kuimarisha ulinzi.

Wananchi mbalimbali wa Chanika wakifuatilia mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo hilo ukihusisha mawaziri kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dkt. Dorothy Gwajima ikiwa ni juhudi za serikali kutatua tatizo la makundi ya Watoto wadogo wanaojihusisha na uhalifu maarufu kama panya road ambao siku kadhaa zilizopita walivamia maeneo ya zingiziwa yaliyopo Chanika na kujeruhi wananchi wa maeneo hayo pamoja na kupora vitu vya thamani ikiwemo simu na televisheni.

Akida Akida 
Afisa Habari
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi


 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.