Habari za Punde

Maafisa Ustawi Waomba Ushirikiano Vita ya Ukatili

 

Na WMJJWM, DSM
Maafisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Dar Es Salaam wameiomba Jamii kutoa ushirikiano katika kufuatilia na kushughulikia kesi za vitendo vya ukatili ili lengo la kutokomeza vitendo hivyo lifikiwe.

Hayo yamebainika wakati wa kikao kazi kati ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima na Maafisa hao, kilichofanyika jijini Dar Es  Salaam chenye lengo la kutathmini utendaji kwenye kutokomeza vitendo vya ukatili alipofanya ziara Mkoani hapo tarehe 05 Oktoba, 2022.

Mmoja wa Afisa Ustawi wa Jamii Suzan Boniphace amesema wanakutana na changamoto nyingi zinazokwamisha utendaji wao ikiwemo kukosa ushirikiano wa wanajamii na wadau wengine.

"Mara nyingi tunapoanza kufuatilia kesi tunajikuta zinaishia njiani kwa kukosa ushirikiano, wengine kesi zinaishia nyumbani na wakati mwingine wenzetu wa Mamlaka nyingine kutukwamisha" alisema Suzana

Naye Afisa Ustawi wa Jamii, Magdalena Msaki amesema ili kupunguza ukatili dhidi ya watoto wanaoomba mitaani, kuwe na mwongozo wa watu wanaotaka kutoa misaada kama ibada waelekezwe sehemu Maalum kwani baadhi ya watoto wanakosa fursa za elimu na kukimbilia misaada hiyo hadi wanafika utu uzima wao.

Maafisa hao wamebainisha pia kuongezeka kwa kundi la watoto hasa wenye ulemavu kutumikishwa kuomba mitaani pamoja na kwenye kumbi za starehe.

Akizungumza katika Kikao Kazi hicho  Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amewataka Maafisa hao kuendelea na kazi kubwa wanayoifanya katika kutokomeza ukatili wakati Serikali inaendelea kufanyia kazi changamoto ya uhaba wa Maafisa hao.

"Wakati tunaendelea kuja na uwezesho wa Maafisa wengi sisi tujitahidi kwani ni katika kipindi hiki kazi ya Maafisa Ustawi wa Jamii inaonekana na ndiyo sababu Mhe. Rais akaona kulingana na Maendeleo na mahitaji ya sasa aunde Wizara hii" amesema Mhe. Gwajima.

"Mnafahamu kwamba ukatili ni changamoto inayoathiri sana watoto na Wanawake
imefika mahali watoto wanatumikishwa
Jamii haijui, watu wanatoa misaada wakati kumbe kuna watu wananufaika nyuma yao, kazi ya kuielimisha jamii namna bora ya kuwasaidia watoto hawa, wa kuongoza mijadala hii ya kuelimisha jamii ni nyie Maafisa Ustawi wa Jamii" ameongeza Mhe. Dkt. Gwajima. 

Ametoa wito pia kwa viongozi na Jamii kulitambua jeshi la hiyari la jamii katika kupambana na ukatili la SMAUJATA ili liwasaidie kuanzia ngazi za Mitaa na vijiji.

Pia amewataka Maafisa Ustawi wa Jamii kuhakikisha Miongozo ya Uanzishaji na Uendeshaji wa  Mabaraza ya Watoto na Madawati ya Ulinzi isambazwe kwa Maafisa Elimu wote ili iwepo shuleni kuimarisha mifumo ya kupeana taarifa kuanzia ngazi ya chini.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Ngwelabuz Lundingija amesema Serikali inatambua Maafisa Ustawi wa Jamii wanafanya kazi kubwa pamoja na changamoto zilizopo hivyo ameiasa jamii kuondokana na dhana kuwa mjini ndio kuna maisha mazuri hali inayochangia watoto wengi kukimbia nyumbani kwao matokeo yake wanatumikishwa isivyo halali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.