Habari za Punde

Kuwa na sheria moja ya Kiislam itakayosimamia masuala yote ya familia kutaisaidia upatikanaji wa haki kwa wanawake na Watoto Zanzibar


 

Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA - ZNZ) kwa kushirikiana na asasi za kiraia zinazotetea haki za Binadamu kesho Jumapili ya tarehe  27/11/2022 wataadhimisha siku 16 za kupinga ukatili dhidi ya wanawake kwa kuwasilisha ripoti ya mapungufu yaliyopo katika sheria ya Mahakama ya Kadhi  inazosimamia masula ya mirathi na talaka kwa lengo la  kupatikana kwa sheria moja ya Kiislam itakayosimamia masuala ya kifamilia na itakayotoa haki na usawa kwa wanawake na Watoto.

 

Maadhimisho hayo yatafanyika kesho  katika ukumbi wa ZURA ulipo Maisara ambapo itahusisha washiriki muhimu kutoka katika taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali ambazo zinazojihusisha na masuala ya kisheria, haki za binadamu na wanamtandao wa kupinga vitendo vya udhalilishaji.

 

Miongoni mwa sheria hizo ambazo zimepitiwa na kuonekana kuwa zina mapungufu ni Pamoja na Sheria ya Mahakama ya Kadhi Na.9 ya mwaka 2017, Sheria ya Mufti Na 4 ya mwaka 2021, Sheria ya Wakfu na Mali Amana ya mwaka 2007, na Sheria ya Mtoto ya mwaka Na. 6 ya mwaka 2011. Sheria hizo zinaonekana kuwa na mapungufu yanayopelekea kuwanyima haki  wanawake na watoto hasa katika suala la mgawanyo wa mali, haki ya mwanamke baada ya talaka na matunzo ya watoto baada ya kuachana jambo ambalo hupelekea utelekezwaji na udhalilishwaji kwa  watoto kwa kukosa haki zao za msingi ikiwemo haki ya kulindwa, kupata elimu jambo ambalo hupelekea kuongeza idadi ya watoto wa mitaani kwa kukosa malezi bora ya wazazi.

 

Sambamba na hilo, pia Sheria ya Wakfu na Mali ya Amana  ambayo haikuweka bayana kuhusiana na mirathi  na hivyo hupelekea mirathi kuchelewa kugawiwa kwa wahusika hali inayosababisha kukosa haki zao mapema na kulazimika kukatisha ndoto zao kama vile kuwapatia elimu  watoto wao.

 

Licha ya changamoto zilizoko katika sheria hizo juu ya haki za mwanamke, ziko sheria ambazo zimetambua nafasi ya mwanamke katika mambo mbali mbali Kwa mfano Sheria ya Mahakama ya Kadhi Namba 9/2017, Kifungu cha 5(1)(f) ambacho kimewapa nafasi wanawake katika kupeleka malalamiko yao juu ya ugawaji wa mali. Hii ingesaidia kuondosha uonevu wa muda mrefu na umasikini kwa wanawake ambao mara nyingi huachwa na kunyang’anywa kila kitu na kuwalazimu kuanza upya maisha pamoja na nguvu nyingi alizotumia katika kutengeneza utajiri wa familia.

 

Hata hivyo, kifungu hicho katika sheria ya Mahakama ya Kadhi hakimsaidii mwanamke kwani bado utekelezaji wake unafuata matakwa ya Kadhi mwenyewe.  Kwenye sheria hiyo,  mchango uliozungumziwa ni  ule wa kutoa pesa na kuwa na risiti na kuacha mchango mkubwa wa hali na mali na usio wa pesa ukiwemo wa kushughulikia nyumba, watoto, baba, wazee na wagonjwa wakati mwenza wake yuko kazini.

 

Wakati Siku 16 za kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia zikiadhimishwa duniani kote, bado kuna changamoto nyingi zinazowaandama wanawake na watoto zikiwemo kuendelea kwa vitendo vya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia vinayochangiwa na kutokuwepo kwa mifumo imara ya kuwalinda na kuwapatia haki zao waathirika  kwa wakati muafaka.

 

Kauli mbiu ya asasi  hizo kwa mwaka huu ni  “Tuungane kumaliza vitendo vya udhalilishaji na Ukatili wa Kijinsia”.  Kauli mbiu hii inakwenda sambamba na kauli mbiu ya kitaifa isemayo “Tuungane kumaliza ukatili na udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto”  ambapo kauli mbiu zote zinasisitiza juu ya umuhimu wa kuchukua hatua katika kumaliza kabisa vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.

 

Miongoni mwa Asasi  za kiraia zilizosimama pamoja katika maadhimisho haya ni pamoja na; Umoja wa Watu wenye Ulemavu Zanzibar (UWZ), Kituo cha Msaada wa Huduma za Kisheria Zanzibar (ZLSC), Chama cha Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA),Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Zanzibar Gender Coalition (ZGC), Umoja wa Wanawake wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA), ZAFAYCO,  ZAPAO, Mtandao ya Kupinga Vitendo vya Udalilishaji Zanzibar, Kijiji cha Watoto SOS, Milele Zanzibar Foundation, Jumuiya ya Vijana na Elimu Kaskazini (JUVIEKA) na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA, ZNZ).

Maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake  ni kampeni maalumu ya kimataifa kufuatia mauaji ya kinyama ya wanawake  yaliyotokea Jamhuri ya  Dominika mwaka 1960. Umoja wa Mataifa ulizitenga Siku hizi 16 kendesha kampeni ya Kupinga Ukatili dhidi ya Wanawake. Maadhimisho haya huanza tarehe 25 ya Novemba ya kila mwaka na hufikia kilele chake tarehe 10 Desemba ambayo ni Siku ya Kimataifa ya Kuadhimisha Tamko Rasmi la Haki za Binadamu, ikiwa ni ishara ya kuhusisha ukatili dhidi ya wanawake na haki za binadamu na pia kuweka msisitizo kwamba ukatili wowote wa kijinsia ni uvunjwaji wa haki za binadamu.

 

Imetolewa na TAMWA - ZNZ kwa kushirikiana na Asasi za kiraia zinazotetea haki za Binadamu, Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.