Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, katikati akifafanua jambo wakati wa semina ya kuwajengea uelewa viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakiwemo Mawaziri, Naibu Mawaziri na Makatibu Wakuu wa SMZ, kuhusu matumizi ya Baiteknoloji ya Kisasa. Kulia kwa Makamu ni waziri katika Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe. Harous Said Suleiman na Kushoto ni Katibu Mkuu Kiongozi Zena Ahmed Said. Katika Semina hiyo Mhe. Othman alimuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwenyi imefanyika Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakili Kikwajuni mjini Zanzibar leo Tarehe 27.12.2022.
Picha na Ofisi ya Makamu
wa Kwanza wa Rais Kitengo cha Habari.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mpinduzi Mhe. Dk. Hussein Mwinyi, amesema kwamba dunia imekabiliwa na
changamoto kubwa ya kutojitosheleza kwa mahitaji ya chakula kutokana na
ongezeko la idadi ya watu na mabadiliko ya tabia nchi ambayo yanaathiri
uzalishaji.
Mhe. Rais Mwinyi ameyasema hayo
katika hotuba iliyosamwa kwa niaba yake na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud
Othman, alipomuwakilisha Rais katika ufunguzi wa semina ya kuwajengea uwelewa
kwa viongozi wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhusu matumizi ya
Bioteknolojia ya kisasa huko katika ukumbi wa sheikh Idrisa Abduliwakili
Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Aidha Dk. Mwinyi amesema kwamba idadi ya watu Barani
Afrika ikiwemo Tanzania na Zanzibar inategemewa kuongezeka maradufu ifikapo
2050 na kwamba hali hiyo itasababisha usalama wa chakula kuwa na changamoto
kubwa iwapo hatua sahihi hazitachukuliwa
mapema ili kuzuia hali hiyo isiwe janga.
Hivyo Mhe. Rais amesema kwamba
matumizi ya biteknoloji ya kisasa ni elimu inayowezesha kufanyika mabadiliko ya
vijinasaba (DNA) kwa kuvumbua mambo mbali mbali katika nyanja za Afya , Uchumi
wa bluu, Kilimo , Ufugaji , Mazingira na bidhaa za viwandani.
Aidha Dk. Mwinyi amefahamisha
kwamba Biteknolojia ya kisasa iwapo itatumika kwa usahihi na ufanisi inaweza
kuchangia katika kuleta maendeleo
endelevu ya kiuchumi na kijamii kwa haraka kama ilivyofanyika katika
upatikanaji wa chanjo ya maradhi ya Uviko 19 iliyopatikana kwa muda mfupi sana.
Sambamba na hayo Mhe. Mwinyi
amesema kwamba katika Nyanja ya afya biteknoliji ya kisasa pia inatumika katika
kuzalisha dawa na chanjo mbali mbali , kutambua magonjwa na kutengeneza vyakula
vyenye virutubisho ili kukabiliana na matatizo ya utapia mlo.
Mbali na hayo pia Rais Mwinyi amesema
kwamba teknolojia ya kisasa inaweza
kutumika katika kusafisha mazingira hasa katika kuondoa mabaki ya sumu zinazotokana na taka za viwandani na kupunguza matumizi ya viuwatilifu na hivyo kuchangia katika kutunza hifadhi ya
mazingira pamoja na afya za binaadamu na wanyama.
Aidha amesema kwamba teknolojia hii
ni muhimu katika maendeleo ya sekta ya viwanda kwa uzalishaji wa bidhaa kama za
nishati mbadala ya biogesi, kutengeneza vyakula vya mifugo dawa za kusafishia
vipodozi vya binaadamu .
Akiwasililisha mada kuhusu Bioteknolojia ya Kisasa, Matumizi, Fursa,
Faida na changamoto zake Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dk. Aly
Mahadhy, amesema kwamba kuwepo kasi ya ongezoke la idadi ya watu, mabadiliko ya
tabia nchi na ardhi kuliwa na bahari
kutasababisha kukosekana kwa eneo la kilimo na hivyo kusababisha uhaba
mkubwa wa chakula.
Aidha amefahamisha kwamba kuwepo
kwa magonjwa ya mazao ya kilimo kama vile mpunga , muhogo na migomba ambacho ni
chakula muhimu kwa wananchi kunahitajika juhudi kubwa za kiutafiti ili kuweza
kuzalisha mbegu mbadala na vifaa tiba na chanjo za magonjwa mbali mbali kupitia
teknolojia ya kisasa ili kukabiliana na hali hiyo.
Mapema Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu
wa Kwaza wa Rais Zanzibar Dk. Omar Dadi Shajak, amesema kwamba mafunzo hayo ni
muhimu katika kufanya tathmini ya masuala yanayohusu matumizi ya teknolojia ya
kisasa na kusaidia Zanzibar katika
uandaaji wa sera na sheria ili kuweka muongozo sahihi wa matumizi ya teknolojia
ya kisasa.
Semina hiyo ya siku moja
imeandaliwa kwa pamoja na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Tume
ya Mipango na kudhaminiwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia ya Tanzania Bara na
kuwashirikisha Mawaziri , Naibu Mawaziri
, Makatibu Wakuu pamoja na Manaibu Katibu wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar.
Imetolewa na ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Kupitia Kitengo chake cha habari leo tarehe 27.12.2022.
No comments:
Post a Comment