Habari za Punde

Serikali kuwawekea mazingira mazuri wajasiriamali

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwawekea mazingira mazuri wajasiriamali ili waweze kuuza bidhaa zao Ndani na Nje ya Nchi.

Mhe. Hemed Ameyasema hayo katika shughuli ya kukabidhi vifaa vya ufugaji nyuki kwa Wakuu wa Mikoa ya Unguja iliyofanyika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar.

Amesema azma ya Serikali ya Awamu ya Nane ni kuwawezesha wananchi kiuchumi ambapo jitihada nyingi zimechukuliwa kuona wananchi wanakomboka kiuchumi hususan baada ya mripuko wa Janga la Uviko 19.

Ameeleza kuwa Jumla ya Shilingi Bilioni Moja, Milioni Mia nne Thalathini na Nane, Laki mbili na Elfu Sita, Mia Mbili na Hamsini zimetengwa kwa ajili ya wajasiriamali wa ufugaji wa Nyuki.

Aidha ameeleza kuwa Mradi huo umenufaisha Vikundi 85 kwa kupewa mafunzo ya ufugaji wa Nyuki na kuwataka wanufaika wa Mafunzo hayo kuyatumia vyema mafunzo waliyoyapata.

Mhe. Hemed ameeleza kuwa Mradi huo umelenga kuwasaidia Vijana na wanawake utasaidia kuongeza thamani ya zao la asali na kulipatia soko la uhakika na hatimae kuinua hali za Maisha ya wananchi wa Zanzibar.

Pamoja na hayo Mhe. Hemed ameeleza kuwa Shughuli za ujasiriamali katika Karne ya sasa zimechukua sehemu kubwa ya maendeleo ya watu ambapo Idadi kubwa ya jamii mijini na vijijini kipato chao kinategemea shughuli hizo na kuongeza kuwa asilimia kubwa ya walioinuka kibiashara na kimaisha walitokea katika shughuli za Ujasiriamali.

Aidha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  ametumia fursa hiyo kuwataka wanufaika wa Mradi huo kuendelea kuunga Mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Nane kwa kuinua ujasiriamali na kutovunjika Moyo na kuwataka wawe waadilifu katika uzalishaji wa asali na kuzingatia vigezo na ubora wa Soko la Dunia.

Aidha amewataka kuvitunza vifaa walivyokabidhiwa ili viwafae kwa kuzalisha asali yenye viwango itakayouzika na kuwataka kurejesha Mkopo walipatiwa ili kuufanya mradi huo uwe endelevu.

Sambamba na hayo Mhe. Hemed amewataka wataalamu wa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo kushirikiana na Wataalamu wa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi kiuchumi kuhakikisha wanafatilia matumiizi sahihi vifaa hivyo na kuwapatia wajasiriamali ushauri wa kitaalamu.

Nae Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Kazi Uchumi na Uwekezaji Mhe. Mudrik Ramadhan Soraga ameeleza kuwa Serikali imejenga vituo viwili vya kusanifu asali Kizimbani kwa Unguja na Pujini Pemba kwa lengo la kusaidia kuongeza ubora wa asali inayozalishwa Zanzibar. 

Ameeleza kuwa Programu hiyo ni chachu kwa wadau wengine wa ufugaji Nyuki kuona juhudi za Serikali na wao kupata mafunzo ili kukuza uzalishaji wa asali Nchini.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Wakala wa Uwezeshaji Wananchi kiuchumi Zanzibar Bwana Juma Burhan Muhamed amemuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa watawasimamia wanufaika hao kuvitumia ipasavyo vifaa hivyo pamoja na kuhakikisha wanarejesha Mkopo huo kwa lengo la kuwaendeleza wafugaji wengine..

Akisoma Risala kwa niaba ya wanakikundi ndugu Latifa Faraja Ali ameeleza kuwa mafunzo ya kuwaendeleza wajasiriamali wa ufugaji wa nyuki yaliyochukua wiki mbili yamewasaidia kuwaongezea ujuzi pamoja na kujua namna ya kutengeneza mizinga ya kisasa na nta ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa wafugaji wa nyuki.

Aidha ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa Jitihada zake katika kuinua shughuli za ufugaji wa Nyuki hasa kwa kujenga vituo vya Kisasa vya  usanifu asali Unguja na Pemba ambavyo vitasaidia kukuza na kuboresha zao hilo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.