Habari za Punde

Kilele cha Siku 16 za kupinga ukatili kwa asasi za kiraia Pemba.

Afisa mdhamini Wizara ya Afya, Khamis Bilali akizungumza wakati wa kongamano la kilele cha Siku 16 za kupinga ukatili kwa asasi za kiraia Pemba.

Wadau walioshiriki kongamano hilo wakiendelea na mdahalo wa kujadili mwenendo wa matukio ya udhalilishaji Zanzibar.

Mjumbe wa kamati ya kampeni ya maadhimisho hayo kwa asasi za kiraia,Tatu Abdalla Msellem, akiwasilisha ripoti ya utekelezaji wa kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili katika jamii.
 

JAMII imeshauriwa kuacha muhali na badala yake waripoti kwa wakati matukio ya udhalilishaji yanapotokea kwa lengo la kutoa fursa kwa vyombo vya sheria kutekeleza wajibu wake na kuchukua hatua za haraka dhidi ya watuhumiwa wa vitendo hivyo.


Hayo yametolewa na wadau wa kupinga udhalilishaji katika kongamano la kilele cha kampeni ya SIku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto wa kike lililoandaliwa na asasi za kiraia Pemba kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Zanzibar.


Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa Wilaya ya Chake chake, Afisa mdhamini Wizara ya Afya, Khamis Bilali alisema tatizo la vitendo vya udhalilishaji bado ni kubwa katika jamii ambapo nguvu ya ziada inahitajika kukabiliana nalo.


“Vitendo vya udhalilishaji bado ni tatizo kubwa katika maeneo yetu na vinaendelea kuriootiwa kila siku, kwahiyo ifike pahali kwapamoja tuseme ukatili sasa basi kwa nguvu zetu wote kwasababu vitendo hivi vinaacha athari kubwa kwa jamii kiuchumi na kitamaduni,” alieleza.


Katika hatua nyingine amezitaka mamlaka zinazoshughulikia kesi hizo kuongeza nguvu katika uzimamizi wa kesi ili watuhumiwa wanaobainika na hatia wachukuliwe hatua kwa wakati.


Alifahamisha, “naziomba taasisi zinazosimamia kesi hizi ziongeze nguvu katika ushughulikiaji wa kesi hizi ili kuimarisha na kurejesha imani kwa jamii juu ya taasisi hizi katika kesi za udhalilishaji kwani kesi zinapocheleweshwa kuchukuliwa hatua malalamiko kwenye jamii.”


Mapema mjumbe wa kamati ya kampeni ya maadhimisho hayo kwa asasi za kiraia,Tatu Abdalla Msellem alieleza asasi zimetumia siku hizo kutembelea shehia mbalimbali kutoa elimu kwa makundi tofauti na kuhamasisha jamii juu ya athari za matukio hayo.


"Katika siku hizi 16 za Kupinga Ukatili,  sisi asasi za kiraia Pemba tumezitumia kwa kufanya shughuli mbalimbali kupitia utoaji wa elimu ya Kupinga Udhalilishaji katika makundi tofauti ambapo tulifanikiwa kutoa elimu hiyo katika madrasa,  skuli na kwenye mikutano katika shehia Uwandani, Shungi, Shumba mjini pamoja Wesha," alieleza mjumbe huyo.


Aliongeza kuwa kupitia mikutano ambayo imefanyika kwenye jamii, wanajamii wameshauri kuwepo na ufuatiliaji wa kina kwenye kesi hizo kutokana na kubainika kwamba kuna baadhi ya watu wameonekana kuchukulia udhalilishaji kama fursa ya kujiingizia kipato ama kulipiziana visasi pale wanapokuwa wamekosana kwa mambo mengine.


Nae Mratibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) ofisi ya Pemba, Fat-hiya Mussa alisema kutokana na juhudi ambazo wadau wa kupambana na vitendo hivyo wamezichukua, mwamko wa jamii kuripoti matukio hayo umeongezeka.


Alisema changamoto iliyopo kwasasa ni uchelewaji wa waathirika kuripoti tukio linapotokezea kwa wakati jambo ambalo linasababisha kuharibu baadhi ya ushahidi muhimu unaohitajika wakati wa uendeshaji wa kesi.


Alisema, “Kwasasa kesi nyingi zinaripotiwa lakini changamoto iliyopo baadhi ya kesi zinacheleweshwa kuripotiwa kwa wakati sahihi jambo ambalo linapelekea kutoa mwanya kwa watuhumiwa kukimbia na wakati mwingne kuharibika kwa baadhi ya ushahidi muhimu.”


Akizungumza katika kongamano hilo, Sheikh Maulid Abdalla Nassor ambaye ni kiongozi wa dini Pemba, alihimiza jamii kurejea misingi na maelekezo ya dini kwenye malezi ya watoto ili kuwalinda dhidi ya vitendo vya udhalilishaji.


"Dini imetuelekeza wazazi kuzungumza na watoto wetu muda wote, lakini siku hizi watoto hatuzungumzi nao na kuwaelekeza maadili mema. Hili ni tatizo na ili tuweze kuondosha vitendo hivi lazima wazazi tubadilike," alieleza Sheikh Maulid Abdalla Nassor, kiongozi wa dini.


Kwa upande wake mjumbe wa kamati ya maadili na Mwenyekiti wa Walei Kanisa Katoriki Chake chake Pemba, Robert Miguwa alishauri kutungwa kwa sheria kali inayowadhibiti wanaofanya vitendo hivyo ili kukomesha kujirudia kutekeleza matukio hayo.

 

Alieleza, "wale wanaobainika kufanya vitendo hivi sioni kama kuna haja ya kuwafunga kwasababu hata wakifungwa miaka 30 bado athari ipo pale pale na hawaogopi tena kufungwa. Kuna haja ya kuweka sheria ambayo mtu akifanya hasa hawa watu wazima basi wahasiwe na warudi kuendelea na malezi ya familia kwasababu akihasiwa hawezi kufanya tena.”


Kongamano hilo la Siku 16 za kupinga ukatili wa Kijinsia liliratibiwa na Asasi za kiraia Pemba ambazo ni Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ), Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar, KUKHAWA, Jumuiya ya ajili ya watu wenye Ulemavu wa Akili Zanzibar, Jumuia za wasaidizi wa sheria za wilaya nne za Pemba, PEGAO, TUJIPE, ZYCO, MY HOPE FOUNDATION pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Zanzibar.


Katika kongamano hilo, wadau mbalimbali kutoka asasi za kiraia, mashirika na taasisi za Serikali walishiriki wakiwemo maafisa kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa mashtaka, Dawati Polisi, Mahakama, Ustawi wa Jamii, pamoja na Mitandao ya Kupinga Udhalilishaji wilaya za Micheweni, Mkoani, Wete na Chake chake ambapo kwa pamoja walipata fursa ya kutathimini hali ya matukio hayo Zanzibar na kujadili mikakati ya kuimarisha ili kukabiliana na vitendo hivyo katika Jamii.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.