Habari za Punde

Kabadi Yasherehekea Miaka Minne ya Dk.Mwinyi kwa Kuandaa Ligi ya Kwanza ya Mchezo Huo

 

Ofisa michezo kutoka  idara ya michezo chini ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Saleh Hashim, akizungumza  wakati akizindua ligi ya mchezo ya kabaddi muhula wa kwanza katika viwanja vya New Amaan Compex. (Picha na Mpiga Picha Wetu).

NA FAUZIA MUSSA

Katika kuadhimisha miaka minne ya Dk. Mwinyi, shirikisho la kabadi Zanzibar limeandaa ligi ya mchezo huo msimu wa kwanza ambapo kufanyika kwa mashindano hayo kutasaidia kuutangaza mchezo huo ndani ya  jamii.

Hayo yameelezwa na ofisa michezo kutoka  idara ya michezo chini ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Saleh Hashim wakati akizindua mashindano hayo yatakayodumu kwa siku tano katika viwanja vya New Amaani Compex.

Alisema uzowefu unaonesha kuwa mchezo huo bado ni mgeni kwa jamii hivyo aliwaomba vijana kujifunza  kupitia mashindano hayo.

Alieleza kuwa Wizara inafarajika kuona michezo mbalimbali  inaongezeka hali inayosaidia kuitangaza nchi na kusema kuwa wizara itaendelea kuchukua juhudi za makusudi kuhakikisha mchezo huo unatambulika na kuendelezwa.

Alifahamisha kuwa hatua hiyo pia inaonesha wazi maendeleo ya mchezo huo ulioanzishwa miaka miwili iliyopita, na kuwaomba wadau wa michezo kuongeza nguvu katika mchezo huo ili kuupa thamani  na kuutambulisha kwa watu.

Mkurugenzi  wa maendeleo  ya michezo wa shirikisho la chama cha kabadi Zanzibar,  Abdalla Juma Abeid na Makamu Mwenyekiti wa  mchezo huo,  Ali Seif Juma, walisema historia inaandikwa kwa kuzindua mashindano hayo kwani haijawahi kufanyika tangu kuanza kuchezwa kwa mchezo huo visiwani Zanzibar.

Walieleza kuwa kuimarika na kuongezeka kwa  michezo kunaenda sambamba na  juhudi za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza La Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi  za kuwekeza katika sekta ya michezo, na kusema kuwa ligi hiyo ni maalum kwaajili ya kumpongeza kiongozi huyo kwa mageuzia makubwa aliyoyafanya katika sekta ya michezo.

Walifahamisha kuwa timu 12 zitashiriki katika michuano ya mchezo huo zikiwemo timu nne za wanawake ambapo mara baada ya  ufunguzi timu ya KMKM wanawake watachuana na Lumumba wanawake, na kwa upande wa wanaume timu ya KMKM na Lumumba zitapimana nguvu.

Viongozi hao walilishukuru Baraza la michezo kupitia Wizara ya Habari kwa msaada wao uliyofanikisha michuano hiyo Kufanyika katika viwanja hivyo na kusema kwao ni fursa ya kuutangaza.

Naifat Ame Hassan na Samir Mubarak Sururu wa timu ya kabadi KMKM  walisema wanatarajia kupata ubingwa katika ligi hiyo kwani suala hilo sio geni kwao na wameshafanikiwa katika michezo mingi iliyopita na kupata vikombe.

Aidha wachezaji hao waliahidi kutomwangusha Dk. Mwinyi kwa kuiwakilisha vyema nchi wanaposhiriki  mchezo huo ndani na nje  ya nchi.

Adam Makame Hamad na Sina Mussa wa timu ya kabadi Lumumba  walimshukuru Rais wa Zanziba na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa mchango wake unaosaidia kuitambulisha  michezo mbalimbali ikiwemo kabadi  na kuwashauri vijana kujiunga na mchezo huo kwani utawasiadia kuwatoa kimaisha, na kuimarisha afya zao.

Watazamaji wa michuano hiyo  akiwemo Ahlam Khamis walionesha kufurahishwa na mchezo huo na kusema kuwa wanatamani kujiunga.

Michuano hiyo inakwenda sambamba na kauli mbiu " miaka minne ya Dk. Hussein kabadi inajieleza"

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.