SERIKALI ya Marekani imeimwagia sifa Zanzibar kutokana na mikakati yake kuhusu uhakika wa chakula na uimarishaji wa sekta ya kilimo.
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, Hilary Clinton amesema Zanzibar imeonesha utayari katika kusimamia mradi wa ‘feed the future’ unaojikita zaidi katika suala zima la kilimo cha mpunga kwa kumwagilia, kilimo cha kisasa cha mbogamboga na matunda.
Aidha, chini ya mradi huo pia suala la lishe kupitia chakula bora limezingatiwa ikiwa pamoja na kuongeza thamani ya mazao ya wakulima.
“Marekani imefurahishwa na utayari wa Zanzibar katika suala zima la uhakika wa chakula na mikakati yake katika kuendeleza kilimo…hatutawaacha peke yenu tutawasaidia na kuwaunga mkono katika juhudi zenu” alisema Waziri Clinton.
Waziri wa Kilimo na Maliasili wa Zanzibar, Mansoor Yussuf Himid alimweleza Clinton kuwa Zanzibar tayari inayo sera ya uhakika wa chakula na lishe,sheria ya uhakika wa chakula ambapo mkakati wake umekamilika.
Mansoor amemweleza Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Marekani kwamba katika kuthibitisha utayari wa SMZ, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ameanzisha Idara mpya ya uhakika wa chakula na lishe.
“SMZ imejiandaa kuona kwamba wakulima wetu wananufaika na kukifanya kilimo kuwa kimbilio la vijana, mipango madhubuti imeshawekwa ili kilimo kiwe na tija kwa wakulima wetu na ndio maana Rais, Dk. Ali Mohamed Shein mara kwa mara amesisitiza suala la kilimo bora” alifafanua Mansoor.
Waziri Mansoor amemwambia Waziri Clinton kuwa SMZ imejidhatiti na kuweka vipaumbele vyake katika sekta ya kilimo kwa sasa ni kuwa na uhakika wa chakula na kuongeza kasi ya uzalishaji ili sehemu kubwa ya chakula kizalishwe Visiwani Zanzibar na kupunguza uagiziaji.
Ujumbe wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani umekuja Tanzania pamoja na mambo mengine kuzindua mradi mkubwa wa kilimo ambao Zanzibar unatekelezwa katika kuimarisha sekta hiyo.
Chini ya mradi huo maeneo kadhaa yamepewa kipaumbele ikiwemo maeneo matatu ya kilimo ikiwemo kilimo cha mpunga, mahindi na mbogamboga huku ukibeba vipengele vidogo vidogo katika kuongeza thamani ya mazao kwa wakulima na mbinu za utafutaji masoko.
Katika kikao hicho kilichohudhuriwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Kilimo na Chakula wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Profesa Jumanne Maghembe na Waziri wa Kilimo na Maliasili wa Zanzibar mbali ya suala la kilimo, Waziri Clinton pia ameimwagia sifa Zanzibar katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria.
Amesema Zanzibar ni nchi ya kupigiwa mfano kusini mwa Jangwa la Sahara katika kupambana na Malaria ambapo Waziri Mansoor alitumia fursa hiyo kuelezea mikakati mbalimbali iliyochukuliwa na inayoendelea kuchukuliwa katika kudhibiti na kutokomeza ugonjwa huo.
Mansoor alisema kuwa kiwango cha ugonjwa wa Malaria kimepungua sana katika Visiwa vya Unguja na Pemba ambapo hadi mwaka jana ugonjwa huo umefikia asilimia 0.8.
No comments:
Post a Comment