Habari za Punde

Kikosi cha KMKM Chakamata Karafuu Pemba.

Na salmin Juma Pemba

Afisa mdhamini wa Shirika la ZSTC Pemba Ndg.Abdalla Ali Ussi leo ametoa taarifa kwa vyombo vya habari juu ya kukamatwa kwa karafuu kavu katika bandari ya Tondooni Wilaya ya Micheweni Mkoa wa kaskazini Pemba zikiwa jumla ya magunia 21 yakiwamo magunia 18 ya karafuu na makonyo gunia 3.

Amesema magunia hayo yalikamatwa hapo juzi alfajiri yakiwa ufukweni tayari kwa ajili ya kusafirishwa, wakati walinzi wa kikosi cha KMKM wakiwa katika doria. 

Akithibitisha Kaimu Kamanda wa KMKM operesheni Karafuu Pemba Ndg. Saidi Ali, kwa niaba ya kamanda wa kikosi hicho amesema ni kweli walifanikiwa kukamata magunia hayo na tayari wameyafikisha ZSTC kwa ajili ya kuziuza ikiwa ni sehemu ya makubaliano baina ya wanaokamata karafuu na ZSTC.

Amesema kwa sasa ZSTC wameweka milango wazi kwa yeyote atakaekamata karafuu za magendo awe askari ama raia wa kawaida anaruhusiwa kuuza karafuu hizo na kuchukuwa pato lote kwa asilimia mia moja ikiwa kama sehemu ya kushajihisha  wananchi na vikosi kuweza kulihami zao hilo kutokutoroshwa nje ya nchi.

Mwandishi wa habari hizi alifanikiwa kufika katika kituo cha kuuzia karafuu huko Wete bandarini ambako karafuu hizo zilifikishwa leo hii na kushuhudia jumla ya magunia 21 yakiwasilishwa kituoni hapo.

Karafuu hizo zimearifiwa kuweza kufikia thamani ya shilingi milioni 18 iwapo kama zitakizi vigezo kwani mapema baada ya kufikiswa kituoni hapo ziligunduliwa kuchanganywa na unga wa karafuu pamoja na makonyo karibu nusu kwa nusu kitendo kilichofanywa na walanguzi hao jambo ambalo maafisa ununuzi kutoka katika kituo hicho wamesema linaweza kushusha thamani yake kwa asilimia kubwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.