Habari za Punde

Mahakimu watakiwa kuwa makini wanapotekeleza majukumu yao

Na Miza Kona Maelezo Zanzibar      
Mahakimu nchini wametakiwa kuwa makini na kufuata maadili wakati wa kutekeleza majukumu yao kwa kuepuka maslahi binafsi hasa wanapotoa maamuzi ya kesi za dawa za kulevya.
Mwenyekiti wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma Asaa Ahmad Rashid aliyasema hayo huko Mnazi Mmoja wakati akifunga mafunzo ya udhibiti wa dawa za kulevya kwa Mahakimu wa Wilaya na Mikoa ya Unguja.
Amesema utekelezaji wa maadili ni msingi muhimu katika utendaji wa haki kwa kufuata maadili na sheria zilizowekwa katika kutoa maamuzi.
Amesema jamii inaweza kunusurika na athari ya utumiaji wa dawa za kulevya kwa kutumia vyema mamlaka waliyopewa kwa kutenda haki na kutekeleza wajibu  katika utoaji wa maamuzi ili jamii iweze kuwa na Imani na vyombo vya kutoa maamuzi na kuepuka migogoro na jamii.
“Mahakimu wana mamlaka ya kufanya maamuzi katika utekelezaji wa majukumu yao na matarajio ya wananchi ni kwamba maamuzi yazingatie maslahi ya jamii na sio maslahi binafsi”, alifahamisha Mwenyekiti Asaa
Aidha amesisitiza kuepuka rushwa wakati wa wanapotekeleza majukumu yao kwani rushwa ndio kichocheo kikiubwa cha uzoroteshaji wa upatikanaji wa kutoa haki kwa jamii katika utoaji hukumu wa kesi hizo.
“Wale wanaojihusisha dawa za kulevya ni watu wenye uwezo wa kila aina wana uwezo wa kifedha, wana uwezo wa ushawishi, uwezo wa madaraka na hata wale wasiokuwa na madaraka wanawatumia wenye madaraka ili kufanikisha malengo yao ni eneo lenye changamoto kubwa sana na eneo kubwa sana tukishindwa kutekeleza majukumu yetu hawa wote wenye uwezo watatununua”, alieleza
Nae Jaji Aziza Idd Suweid kutoka Mahkama Kuu akiwasilisha mada kuhusu Namna ya Kuendesha Kesi za Dawa za Kulevya amesema ni lazima kufuata sheria na kanuni zilizowekwa katika uendeshaji wa kesi hizo ikiwemo kupata  ushahidi na vielelezo vya uhakika kutoka kwa mchunguzi wa serikali na kufuata muda ambavyo vitaweza kuthibitisha na kuweza kuzitolea hukumu bila ya kujali utashi binafsi ili kudhibiti dawa hizo.
“Ili ushahidi uweze kukubalika mahakani kielelezo ni kitu muhimu na kihakikishwe kuwa kielelezo hicho ndicho alichokamatwa nacho mtuhumiwa na sio chengine ili kisijekuharibu kesi pamoja kuandika muda uliotokea tukio kabla ya kupelekwa Mchunguzi kutokana na baadhi ya watuhumia hutumia vielelezo sio vyao”,alifahamisha Jaji Aziza.
Nao washiriki wa mafunzo hayo wameeleza kuwa kucheleweshwa upelelezi na vielelezo kutoka kwa mchunguzi ndio sababu kubwa zinazopelekea kuzorotesha uendeshaji wa kesi hizo hivyo wameomba kufanyiwa haraka hatua hizo ili kuweza kuepuka mrikano wa kesi za dawa kulevya ili kuweza kudhibiti janga hilo na kuinusuru jamii.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.