Habari za Punde

Balozi Mdogo wa Oman Zanzibar Azungumza na Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Zanzibar.

BALOZI Mdogo wa Oman anayefanya kazi zake Zanzibar Dk. Ahmad Hamood Al Habsy (Kulia), akizungumza na wanafunzi wanaosomea fani ya Diplomasia na Mahusiano ya Kimataifa, wakati walipofanya ziara kwenye ofisi za ubalozi huo zilizopo Migombani mjini Zanzibar.
BALOZI Mdogo wa Oman anayefanya kazi zake Zanzibar Dk. Ahmad Hamood Al Habsy (Kulia), akizungumza na wanafunzi wanaosomea fani ya Diplomasia na Mahusiano ya Kimataifa, wakati walipofanya ziara kwenye ofisi za ubalozi huo zilizopo Migombani mjini Zanzibar.
DK. Ahmed Hamood Al Habsy, Balozi Mdogo wa Oman visiwani Zanzigar (Kulia) na Mhadhiri wa somo la Diplomasia na Mahusiano ya Kimataifa katika Chuo Kikuu Zanzibar kilichoko Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja, Mohammed Yussuf.

WANAFUNZI, wahadhiri na baadhi ya maofisa wa Ubalozi Mdogo wa Oman mjini Zanzibar, wakiwa katika picha ya pamoja na Balozi Mdogo Dk. Ahmad Hamood Al Habsy nje ya jengo la ubalozi huo Migombani, Zanzibar baada ya ziara ya wanafunzi hao iliyolenga kubadilishana mawazo na kujifunza shughuli za Kidiplomasia na Mahusiano ya Kimataifa. (Picha na Haroub Hussein )

Na Salum Vuai

JUKUMU la mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao katika mataifa ya nje, ni kuwaunganisha wananchi na sio kuwa karibu na serikali na viongozi pekee.
Kauli hiyo imetolewa na Balozi mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar Dk. Ahmad Hamood Al Habsy, alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Zanzibar Tunguu wanaosomea diplomasia na uhusiano wa kimataifa walipomtembelea ofisini kwake Migombani mjini Unguja.

Balozi huyo alieleza kuwa, kwa kutambua hilo, amefungua milango ya ofisi yake kutoa fursa kwa wananchi mbalimbali wa Zanzibar pamoja na viongozi, kwenda kujifunza masuala muhimu kwa lengo la kuimarisha mahusiano ya kihistoria kati ya nchi yao na Oman.

Alisema, baadhi ya watu wanadhani kwamba kufanya kazi katika ofisi za kibalozi kuna mipaka inayowatenganisha mabalozi na wananchi wa kawaida, jambo alilosema sio sahihi.

Dk. Al Habsy alisema licha ya mabalozi kuwajibika kiserikali katika mataifa wanayopelekwa kufanya kazi, pia wanapaswa kuwa karibu na wananchi wa nchi za nje wanazokuweko, wakitambua kuwa nayo ni sehemu ya majukumu yao.

“Kwa kuwa balozi huwa anapeperusha bendera ya nchi yake ugenini, anapaswa kujua kwamba wenyeji wake sio serikali na viongozi pekee, bali wananchi wana haki ya kuwa miongoni mwa wahudumiwa wake kwa mambo mbalimbali,” alieleza.

Balozi huyo alieleza kufurahishwa kwake na ziara ya wanafunzi hao iliyolenga kubadilishana mawazo pamoja na kujifunza juu ya shughuli za kidiplomasia, akiwataka pia kujibidiisha katika kusoma lugha mbalimbali za kimataifa ikiwemo Kiarabu.

Alisema kutokana na uhusiano wake na Oman uliodumu kwa zaidi ya karne mbili sasa, Wazanzibari hawana sababu ya kutokujua lugha ya Kiarabu ambayo pia ndiyo msingi wa dini ya Kiislamu inayofuatwa na asilimia kubwa ya wananchi.

Kwa upande mwengine, alisema mahusiano ya Zanzibar na Oman sio ya kirafiki ambao unaweza kufa, bali ni ya udugu wa damu utakaobaki milele hadi mwisho wa dunia.

“Oman inasaidia nchi nyingi lakini kwa Zanzibar  ina msaada wa kipekee kwani watu wa nchi hizi ni ndugu wa damu na hilo haifutiki. Ziara kati ya nchi zetu zimeongezeka sana, hata nafasi za ndege kati ya Muscat na Zanzibar au Tanzania, zinakuwa shida kutokana na wingi wa wasafiri,” alifafanua Dk. Al Habsy.

Kwa hivyo, alisema ofisi yake itahakikisha inatanua fursa mbalimbali za kuisaidia Zanzibar hasa katika uwanja wa elimu, ili kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kijamii kwa manufaa ya watu wa pande mbili hizo.

Mapema, Mhadhiri wa somo la diplomasia na mahusiano ya kimataifa katika Chuo Kikuu cha Zanzibar Tunguu Mohammed Yussuf, akitoa shukurani kwa ubalozi huo alisema, ziara hiyo imewafunza mengi yenye tija.

Aidha alisema ziara kama hizo katika ofisi za kibalozi, ni sehemu ya mafunzo yanayoweza kuwaongezea maarifa wanafunzi wa fani hiyo ambao ndio mabalozi wa miaka ijayo.

“Namna wewe Mhe. Balozi unavyofanya kazi ya kuwaunganisha wananchi wa Oman na Zanzibar, ni darsa tosha kwetu na hasa wanafunzi hawa, kujua nidhamu inayohitajika kwenye kazi hii ya kidiplomasia,” alisema Mhadhiri huyo.

Kwa upande wao, wanafunzi hao walieleza kufarijika kwa mapokezi waliyopata, na kusema wana matumaini makubwa ziara hiyo itafungua milango zaidi ya ushirikiano kati yao na ubalozi huo.

Aidha walimuomba balozi huyo mambo mbalimbali, ikiwemo kuangalia uwezekano wa kuwatafutia Chuo Kikuu chochote nchini Oman kitakachokuwa tayari kuanzisha urafiki na chuo chao, na hatimaye kujenga utamaduni wa kutembeleana kwa lengo la kujifunza.

Halikadhalika, walishauri kusaidiwa njia za kujiendeleza katika lugha ya Kiarabu ambayo pia wanafundishwa katika chuo chao, kuwaandaa kumudu kazi ya kidiplomasia.

Balozi mdogo Dk. Al Habsy, aliahidi kuangalia namna ya kuyatafutia majibu maombi yao, huku akiutaka uongozi wa chuo hicho kuyawasilisha rasmi kwa barua ili yafanyiwe kazi kadri itakavyowezekana.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.