Na Muhammed Khamis
Wakati zoezi la uchukuaji wa fomu na
kurejesha kwa nafasi ya Urais Zanzibar kupitia chama cha Mapinduzi (CCM) likifikia
tamati, Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) Zanzibar
kinawapongeza kwa dhati wanawake wote waliojitokeza kuomba ridhaa ya kuteuliwa
kuwa wagombea wa kiti cha Urais Zanzibar kupitia Chama hicho.
Katika mchakato wa kutafuta nafasi ya
mgombea Urais Zanzibar ulioanza Juni 15, mwaka huu, jumla ya wanachama 32
wamejitokeza kwenye kinyanganyiro hicho ambapo wanachama watano (5) sawa na asilimia
15 walikuwa ni wanawake.
Wanawake hao ni pamoja na Mwantum Mussa, Hassna
Attai, Fatma Kombo, Mgeni Hassan na Maudline Castico.
Ikumbukwe kuwa hii ni mara ya kwanza
kwa Zanzibar kujitokeza wanawake kugombea katika nafasi hiyo ya juu ya nchi
kutokana na mifumo dume ambayo inamtenga mwanamke katika kuwania nafasi za
maamuzi sambamba na mwenziwe mwanamme.
Hadi miaka ya 1940 ilionesha kuwa mwanamke
alikatazwa kuhudhuria hata skuli, nyenzo muhimu katika kukwaa ngazi za kisiasa
na kijamii kwa madai kuwa anaweza kupoteza ujanajike wake.
Hali hii ilirejesha nyuma sana
maendeleo ya wanawake na nchi kwa jumla kwa vile wanawake ni zaidi ya asilimia
50 ya wakaazi wa Zanzibar kwa mujibu wa Sensa ya 2012 na makisio ya idadi ya
watu yaliyofuata.
Tafiti duniani kote ikiwemo na
Zanzibar zinaonesha kuwa wanawake ni watendaji wazuri, waaminifu, waadilifu na
wanaofanya maamuzi kwa njia ya ushirikishi na hivyo wakiwa kwenye uongozi
huharakisha sana maendeleo ya nchi.
TAMWA ZNZ inapenda kukipongeza CCM kwa kuwawezesha
wanawake hao kutoka chama hicho kuweza kugombea hadi katika hatua hiyo ya
uongozi.
Tunaamimi sasa wakati umefika kwa jamii wakiwemo
wanasiasa kulichukulia suala hili kwa uzito unaostahiki na hivyo kuwapa nafasi
wanawake kuonesha uwezo wao wa kuongoza katika nyanja mbali mbali.
Tunatamani pia CCM itachagua mmoja kati ya
wanawake hao ili kuweza kupeperusha bendera ya Chama hicho katika uchaguzi mkuu
ujao wa mwaka 2020.
TAMWA Zanzibar inaamini kwamba
ujasiri huo ulioonyeshwa na wanawake hao waliojitokeza utasaidia kuongeza
hamasa zaidi kwa wanawake vijana
kuendelea kujiamini na kuona kuwa wanayo nafasi sawa ya kushiriki katika ngazi
zote za maamuzi kwa mstakabali wa taifa lao.
TAMWA Zanzibar inawaomba wanawake wa
vyama vyengine vyote kujitokeza katika kugombea nafasi mbali mbali ili kuongeza
mabadiliko haya ya wanawake katika ngazi za maamuzi itakayopelekea pia kutatuka
kwa matatizo mbali mbali yanayowaaathiri kiuchumi na kijamii.
Dkt Mzuri
Issa
Mkurugenzi,
TAMWA
Zanzibar
No comments:
Post a Comment