Habari za Punde

WAZALENDO WASIYOJULIKANA

Na.Adeladius Makwega-DODOMA

Mkundi ya Mbaru ni miongoni mwa shule za msingi katika wilaya ya Lushoto, mkoani Tanga. Shule ipo katika kijiji ambacho mwaka 2017 kilikuwa na wakazi kati 650-700 kikiwa kijiji chenye usajiri uliokamilika lakini kikikosa sifa ya kuwa na wanakijiji 1250.

Idadi ya watu katika kijiji hiki inaonekana ilikuwa ikiongezeka kila mwaka, kwani nina imani sasa idadi hiyo 1250 imefikiwa.Kikiwa katika kata ya Mnazi yenye vijiji sita; Kwemkwazu (Mnazi yenyewe), Langoni A, Langoni B (vijiji venye Wamasai wengi), Kiwanja, Mkundi ya Mtae na Mkundi ya Mbaru.

Majina yote mawili ya MKUNDI YA MTAE na MKUNDI YA MBARU yana neno MKUNDI- aina ya miti yenye kivuli, mikubwa wenye majani membamba inayoota eneo hilo la tambalale. Wakati MTAE na MBARU ni majina ya kata zilizo mlimani mwa vijiji hivyo.

“Watu wa Mtae na Mbaru tangu enzi hushuka Mkundi kulima kutokana na hali ya hewa ya kuwa tofauti na ya Mkundi, mazao yanayolimwa mlimani ni tofauti na yale ya hapa bondeni na walikuwa wakilima na kurudi lakini kidogo kidogo wakaweka makazi yao.” Walinisimulia wanajijiji wa Mkundi ya Mbaru.

Kwa ramani ya Lushoto, Mkundi ya Mbaru ni kijiji cha mwisho kabisa cha wilaya hii kinachopakana na wilaya ya Same na Korogwe. Kwa mwaka 2017 eneo hilo lilikuwa kame mno, maji ya kunywa na zahanati zinapatikana umbali kilometa zaidi ya sita huko Karamba wilayani Same.

Maeneo haya wanalima mazao ya Nazi, Mpunga, Mbaazi, Ngwala,Tangawizi, iriki, nyanya, vitunguu na mkonge. Kwa jiografia ya Lushoto Ili mkazi wa eneo hilo aweze kutoka kwenda nje ya wilaya hiyo anaweza kutumia njia kubwa nne: Lushoto kupitia soni, Lushoto kupitia Dochi-Mombo, Lushoto Mlalo Kikumbi-Korogwe na Lushoto Mnazi Mkundi ya Mbaru.

Lushoto Mkundi ya Mbaru na Lushoto Kikumbi ni njia maarufu sana, kwa kuzitazama utaona ni njia zisizochangamka sana lakini serikali inapata mapato mengi huko kama ikisimamia vizuri maana huko kuna mifugo mingi hata Wamasai wa Lushoto wanapatikana ukanda huu.

Eneo hilo kuna msimu kuna misafara mikubwa ya malori yanayobeba mbolea ya samadi kutokana na kinyesi cha mifugo ambayo inasafirishwa kwenda Same kwa ajili ya kilimo cha bustani, tani moja kwa Halmashauri hii ilitoza shilingi 3000/- Kwa Tanzania yetu ni Halmashauri chache zenye chanzo hicho cha mapato.

Katika ukanda huu hakuna taasisi kubwa za umma tangu mkoloni taasisi zote zipo Lushoto Mjini, taasisi pekee kubwa ya umma ni Gereza la Mng’aro tu, kwa hiyo hata wakwepaji wa ushuru wanatumia njia hizo sana sana. Kuyakusanya mapato ya serikali kwa ustadi eneo hili ni lazima kuwa na watendaji waadilifu, wachapa kazi na wazalendo.

Kwa wakati huo watendaji wenye sifa hizo walikuwa wa aina mbili; kwanza wale walioanza kazi zamani wakati wa UJAMAA, wengi wao walikuwa ni watu wazima na pili ni wale watendaji vijana wapya. Matumizi ya watendaji vijana yalikuwa sahihi.

Kata ya Mtae alipelekwa binti mmoja anaitwa Mwanavua Chiligati, Binti mmoja jasiri anayejiamini mno na mzalendo. Japokuwa kata hiyo ilikumbwa na tukio la kuuwawa kwa mtendaji wake awali palikuwa tupu kwa muda, Binti Chiligati aliomba mwenyewe kupangiwa hapo.

“Jamani naombeni nipangiwe huko mimi ninaweza kufanya kazi kata ya Mtae vizuri sana.” Maswali yalikuwa mengi mtendaji aliyeuwawa alikuwa mwanaume, vipi huyu binti ataweza kufanya kazi ? Huku watumishi wengi wakiomba kuhama Mtae, lakini binti huyu aliweza kufanya kazi vizuri sana.

Nilipofuatilia kwa kina nilibaini kuwa Mwanamvua jina lake linahusianishwa na Kapteni John Chiligati. Iwe kweli au la leo ninamkumbuka kwa ule ujasiri wake katika utumishi wa umma na si nasaba yake.

“Siyo kwamba kila mtoto wa kiongozi ni kiongozi, lakini wapo watoto wa viongozi wachache sana ambao wanaonesha uhodari mkubwa katika uongozi.”Hilo nilijifunza nikiwa Lushoto.

Kijiji cha Mkundi ya Mbaru alipelekwa Bakari Mwanjano (Abuu Mzalendo). Kijana huyu anajiamini, anauwezo mkubwa wa kusimamia kazi za maendeleo vijijini, ni hodari mno na hakatishwi tamaa. Huyu  alikuwa anatambua matumizi mazuri vifaa wa kompyuta, eneo hilo lilihitaji kijana kama yeye kusimamia makusanyo ya serikali. Kumbuka wakati huo Rais wa awamu ya tano, John Magufuli alisisitiza sana matumizi ya mashine ya kukusanyia fedha.

Akiwa eneo hilo alisaidiwa kuifanya kazi hiyo kwa karibu kwa ushirikiano na Jeshi la Polisi wa kituo cha cha Mnazi, OSS Georgina Matagi na OCD Maziwa (marehemu) hasahasa kumpatia ulinzi madhubuti, maana pesa inahitaji ulinzi. Kazi zilifanyika vizuri mno na serikali ya wilaya ilijipatia mapato ya kutosha kwa uchapakazi wake.

Binafsi nilivutiwa na moyo wa kufanya kazi wa Bakari Mwanjano, nilikuwa na kiu ya kumfahamu zaidi. Nilibaini kuwa alizaliwa huko Mtimbwani Muheza (sasa ni Mkinga) Tanga. Baba yake ni Musa Mwanjano (Mtoza Ushuru wa serikali enzi Ujamaa) na mama yake Mahija Abdalla Binti Mshakangoto (Muuguzi hospitali ya Bumbuli).

Bakari alizaliwa Mtimbwani nakusomea hapo kwa kuwa mama yake alikuwa anafanya kazi za uuguzi chini ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini Mashariki enzi za Baba Askofu Sebastiane Kolowa, naye baba akikusanya ushuru wa kijiji, hapo ndipo wazazi wakaoana na kuzaliwa ndugu huyu . Mwaka 2015 serikali ilichukua zahanati ya Mtimbwani, Mahija Mshakangoto alirudi kwa mwajiri wake Hospitali ya Bumbuli wakati mumewe amefariki.

Nilibaini tabia ya Bakari ya kupenda watu inatokana na tabia ya mama muuguzi lakini ufuatiliaji mapato ulitokana na utoza ushuru wa baba yake, Akisoma sekondari shule ya Arafa Tanga na kusoma Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo

Kwa kuwa Mkundi ya Mbaru pana kituo cha kukusanya mapato ambacho kiliboreshwa ilipendekezwa na serikali ya wilaya mradi huo ufunguliwe na Mwenge wa Uhuru. Kamati za wilaya zilikagua mradi huo nakuona unafaa kuzinduliwa, lakini kamati za kimkoa zilichagua mradi mwingine kwa hoja lazima miradi uwe na pesa za serikali na nguvu za wananchi, kizuia kilikosa nguvu za wananchi. Kwa hiyo ukaingizwa mradi wa darasa la shule ya msingi Mkundi ya Mbaru.

Ujenzi wa darasa hilo ulipatiwa fedha kutoka mradi mmoja unaitwa Lipa kwa matokeo EP4R ambapo shule hiyo ilipewa milioni saba. Wananchi na serikali yao ya Kijiji wakichangia kwa kusuasua. Siku ya mwenge ilipofika kiongozi wa Mwenge wa Uhuru akaukagua mradi huo akaja na hoja ya bati kwa nini ni geji 30 badala ya kuweka bati za geji 28?

Awali mtendaji wa kijiji hicho alipambana na kukusanya michango ya wananchi katika, huku hali ya hewa ilikuwa mbaya na wananchi kukosa mazao na michango ikisusua mno. Mwanakwettu Mwenge wa Uhuru haukufungua mradi huo, lakini darasa hilo liliendelea kutumika kwa kuboresha kidogo kidogo. Wale darasa la kwanza sasa (2022)wapo darasa la sita na mwakani wanamaliza darasa la saba,

Jitihada za Bakari Mwanjano hazikukatishwa tamaa na maamuzi ya kiongozi wa Mbio za Mwenge, wanafunzi wale wa darasa la kwanza wa mwaka 2017 hawakutambua juu ya hoja ya geji 30 wala geji 28 iliyoibuka, wao waliendelea kuimba, kusoma, kuhesabu na kuumba herufi. Hilo hilo darasa lililokataliwa sasa limewawekea misingi ya kujua kusoma na kuandika hata leo wanaweza kuisoma matini hii.Mungu akitujalia uhai mwakani 2023 tutayaona matokeo ya darasa hilo ya mtihani wa darasa la saba.

Mwanakwetu upo?

Leo hii nimewakumbuka tu wazalendo hawa wawili Mwanamvua Chiligati na Bakari Mwanjano kwa hakika ni wazalendo wasiojulikana.

makwadeladius@gmail.com

0717649257.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.