Habari za Punde

Mjomba ni Mama na Shangazi ni Baba.

 Na.Adeladius Makwega-MANG’ULA LUSHOTO

Mwaka 1961 wakati Tanganyika inapata uhuru, babu yangu mzaa baba Fidelis Makwega alikuwa akisomesha Shule ya Msingi Mikwemeni (sasa ni Mbagala Kuu) Jijini Dar es Salaam, naye bibi yangu Edwiki Binti Omari alikuwa ni muokota mayai katika banda la kuku la bibi mmoja wa kizungu aliyefahamika kama Bi Sara (maarufu kama Bi Sela kama ilivyoitwa na Wazaramo wa Mbagala wa wakati huo).

Maaelezo ya TANU kwa wananchi wa Tanganyika ilikuwa,

“Anaondoka mkoloni na mtawala wa Tanganyika huru anakuwa mjomba ambaye ni miongoni mwa ndugu zetu.”

Mtawala anapokuwa mjomba wako, utamuogopa kumwambia ukiwa na jambo la kumueleza au kumshauri? Majibu ya Watanganyika wengi yalikuwa,

“Hatuwezi kushindwa kumwambia mjomba na hata shangazi kwa kuwa mjomba ni mama na shangazi ni baba.”

Somo hilo liliwaingia vizuri Watanganyika na TANU yao kuungwa mkono kila kona. Kweli mwaka 1961 Tanganyika huru ikaongozwa na mjomba naye ni ndugu Julius Nyerere. Hapo mkoloni akaondoka na majoho yake na kumuacha ndugu katika kiti. Tangayika huru ikaungana na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 akazaliwa Tanzania.

Wajomba wakaendelea kushika nafasi hizo kwa Urais na Uwaziri Mkuu, Kipenga cha safari za wajomba kikaanza. Mwaka 1977-1980 Waziri Mkuu alikuwa ndugu Edward Sokoine,1980-1983 akiwa ndugu Cleopa Msuya, Februari 24, 1983 hadi Aprili 12, 1984 tena ndugu Edward Sokoine.

Aprili 24, 1984 hadi Novemba 5, 1985 Waziri Mkuu akawa Salimu Ahmed Salimu. Wajomba waliendelea kushika hatamu kwa nafasi kadhaa tangu kijiji hadi taifa, ilipofika Novemba 5, 1985 alichaguliwa ndugu Joseph Warioba ambaye alifanya kazi hiyo hadi Novemba 9, 1990.

Joseph Warioba kabla ya kuwa Waziri Mkuu alipitia nafasi mbalimbali kama mwanasheria wa serikali, mwanasheria wa jiji la Dar es Salaam na baadaye Mwanasheria Mkuu. Joseph Warioba, John Malecela, Cleopa Msuya (tena), Fredrick Sumaye, Edward Lowassa, Mizengo Pinda na sasa ni Kassim Majaliwa Majaliwa.

“Halimashauri hii ni shamba la bibi na wale wanaoshangilia wengi hawajui kinachoendelea, huku juu mmejipanga mnafanya mnavyotaka, mnasahau kuwa serikali inakuona popote ulipo, inajua unachofanya popote ulipo, popote ulipo tupo, mnaendesha mambo hapa, mnaendesha biashara zenu, madiwani mnaambiwa hautakiwi kuwa na biashara, kama wewe ni mdau katika eneo hilo.

Wakuu wa idara mnafanya biashara na mnaambiwa kabisa hamtakiwi kufanya biashara, kwa sababu ya conflicts of interest lakini nyinyi mnaendelea kufanya biashara na halimashauri zenu, pamoja na nyinyi kujificha katika makoti lakini na nyinyi tumewakuta katika makoti hayo humo ndani. Tunaposema halimshauri zenu zinanuka rushwa ni pamoja katika eneo hili.

Niwape mfano mmoja nyie mmekiuka sheria ya matengenezo ya magari, mmeamua kutafuta watu wenu ambapo sio rejestered kama taasisi au chombo kinachofanya kazi unayotakiwa kuipa, lakini bado unaipa na unailipa… kwanini aandikiwe hundi Umbira? Kamanda wa TAKUKURU upo? Kamanda wa TAKUKURU, umewaona hawa?(ndiyo) ukimuacha mwenyekiti ambaye ameshawaruka, Kaimu Mkurugenzi, huyu ambaye hayupp Remmy, Mweka Hazina na Mwandika Hundi Chomola(Chomoka). Hawa ninakukabidhi na kwa mujibu utumishi nikiwaleta kwako wanasimama kazi mpaka tutakapothibitishwa kuwa katika hili hawahusiki.”

Haya ni maagizo ya Waziri wetu Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa(Mjomba) akiwa Halimashauri ya Mbozi, mkoa wa Songwe mwaka 2017/2018 alipokuwa na ziara yake ya kikazi.

Matukio kama haya yameendelea kujirudi sana katika ziara za viongozi wetu wakuu. Binafsi nimekuwa nikijiuliza swali hivi ni kwanini sasa katika taifa letu kumekuwa na hali hii ya kufukuzwa na kusimamishwa kwa wingi kwa Wakurugenzi Watendaji na watumishi wa Wilaya kila mara?

Jambo hilo halionekana kushamiri kwa Makatibu Tawala wa Wilaya, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Mikoa, Makatibu Wakuu na Mawaziri ambao wote wanateuliwa na rais.

Nina fahamu fika Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa kitaalumu ni mwalimu na mwalimu mara zote ni mtu mwenye upendo kwa wanafunzi na jamii yake. Upendo huo pia ni kwa wananchi kwani nia yake zuri akitaka halimshauri zetu ziweze kuwa zinaendeshwa vizuri na wananchi wapate maendeleo.

Pia nina hakika ndugu huyu huwa anapofanya maamuzi huwa hana nia ya kumuonea mtu na ndiyo maana akiagiza huwa aingilii uchunguzi anawaacha vyombo wafanye uchunguzi wao wa haki na kama kuna kosa linapelekwa mahakamani nao watalifanyia uamuzi.

Shauri hilo la Mbozi mwaka 2019 ilibainika watumishi hao hawakuwa na kosa walirejeshwa kazini. Nina hakika hakuna upande wenye malaika tu na upande mwingine wenye mashetani, tabia ya binadamu zinafanana penye kundi lolote lile wapo wazuri na wapo wabaya wa tabia.

Mwanakwetu kwa leo nashauri yafuatayo;

Katika kila ziara za viongozi wakuu wanapofanya vikao vya ndani visirushwe moja kwa moja na vyombo vya habari bali yale maamuzi ndiyo yatangazwe kwa muhtasari wake hasa hasa na maafisa habari. Hilo litatoa nafasi kwa taasisi zingine kutimiza wajibu wao baada ya maagizo hayo na kuondoa dhana ya kuchafuliana majina baada ya uchunguzi au mahakama kuamua vinginevyo

Mara baada ya uchunguzi wale wanaoshinda warudishwe katika nafasi zao ili kuondoa malalamiko ya kuona kuwa wameonewa na kiongozi fulani.

Mijadala yote juu ya mapato, matumizi na makusanyo ya pesa za halimashauri huwa ni ajenda katika vikao vya kiwilaya ikiwamo Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya, mkurugenzi akialikwa tu. Hapa nashauri Mkurugenzi Mtendaji na kamanda TAKURURU wa wilaya wawe wajumbe wa kamati hii siyo kualikwa na jaenda zingine za kikao hicho hawazifahamu hilo linaleta  majungu na fitna miongoni mwa viongozi.

Kama kuna shida ifahamike na wote na kama kuwajibika wajumbe wote kamati za kiwilaya na kimkoa wawajibike.Wote wamepewa  dhamana iwe ya wilaya au mkoa maana jahazi likizama linazamo na wote waliomo ndani  yao. Hiyo itajenga dhana ya umoja katika kazi na udugu miongoni mwa viongozi kama ule udugu wa TANU.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.